sábado, 18 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 16 YA MWAKA-B

JUMAPILI  YA 16 YA MWAKA-B
19/7/2015
Somo I: Yer 23:1-6
Zab: 22:1-6
Somo II: Efe 2:13-18
Injili: Mk 6:30-34
Nukuu:
Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana,” Yer 23:2 

Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana,” Yer 23:4

Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 23:6

Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya  amani,” Efe 2:15

Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba,” Efe 2:16 

Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja,” Efe 2:18
Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,” Mk 6:31 

TAFAKARI: “Makusudi ya Mungu: “asipotee hata mmoja wa wale aliowaumba kwa sura na mfano wake.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha yetu leo hapa duniani ni kulisadifu lile alilolianzisha Mungu na kulikusudia. Kwa maana hiyo, “Makusudi ya Mungu: “asipotee hata mmoja wa wale aliowaumba kwa sura na mfano wake.” Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba maisha unayoishi kadiri ya wito wako, wewe ni kielelezo cha kusudio la Mungu katika uumbaji wake. Hapo ulipo, uwe mkleri, mtawa au mlei, uliokabidhiwa asipotee hata mmoja. Ni kosa kubwa sana kufanya hujuma kwa wale ambao Mungu ametukabidhi. Hivyo Mungu kwa kupitia Nabii Yeremia anasema, “juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana,” Yer 23:2. Mpendwa katika Kristo, kama wewe ni kiongozi kwa ngazi yoyote ile, elewa kwamba wewe ni jalala la kila kitu. Hivyo yote uyapokeayo na kuambiwa na watu yachunguze kwa makini sana, na utoapo neno la mwisho lilenge katika kuwapata wale waliochini yako na siyo kuwapoteza.

Ndugu yangu, huyu tunayemwabudu na kumtumikia ni Mungu mwenye haki. Mungu wetu si Mungu wa visasi, bali ni Mungu anayetutaka tuishi katika haki na upendo.  Na Mungu anasema hivi; Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 23:6. Yatupasa kuwa watu wa haki hata kama kwa kutenda haki tunaumizwa.

Wapendwa, Mungu wetu anatutakia mema siku zote, na hivyo kwa njia ya msalaba kupitia mwana wake mpezi, licha ya kwamba ni kifo cha aibu kutokea katika historia ya mwanadamu, anaonyesha upendo wake mkuu usio na kipimo kwetu. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya  amani,” Efe 2:15. Amani hii tuipatayo ni tunda la kifo cha msalaba wa bwana wetu Yesu Kristo, Ndugu yangu, maisha yako kama mfuasi wa Kristo hayawezi kutenganishwa na msalaba wa Bwana wetu Yesu. Ni katika msalaba tunapata utukufu. Hivyo, Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba,” Efe 2:16. Hakika Mungu anatupenda upeo!

Ndugu yangu, tunapoutambua ukweli huu, tujue kabisa tupo karibu na Roho wake Mtakatifu ambaye kwa kupita yeye tunapata maondoleo ya dhambi zetu, na kutufunulia yale yaliiojificha katika umilele wa Mungu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja,” Efe 2:18. Je, ni nani atakayetutenganisha na upende wake Kristo? Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika,” 1Kor 13:8-10. Upendo wa Mungu kati yetu hutufanya kile tulicho katika kweli na kile Mungu alichokusudia katika maisha yetu.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, Mungu anatutakia mema kila dakika. Na katika jambo hili ni vyema kuwa na muda wa kutosha katika kuyatafakari mambo makuu ya Mungu anayotutendea kila siku ya maisha yetu. Jiwekee utaratibu wa kuyatafakari makuu haya ya Mungu, hata mara moja kwa mwaka. Mfano wewe na mwenzi wako wa ndoa, wewe kama mkleri, na hata mtawa, nje ya utaratibu wa kawaida uwe na muda binafsi wa kuyatafakari hayo. Ikiwezekana hata kwa wiki moja ukiwa katika sehemu tulivu na  ya sala. Hivi ndiyo Bwana wetu Yesu Kristo awatakavyo wanafunzi wake wafanye. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,” Mk 6:31. Mara nyingi tumekuwa kama bomba lenye kumwaga maji na kujisahau lenyewe na kuleta ukavu pale liliposimikwa.

Ndugu yangu, naomba nikupe mfano huu: kuna aina nne za watu. Lakini leo nitasema aina moja ya watu inayoendana na injili na masomo yetu ya leo. Miongoni mwetu, wapo watu ambao wapo tayari kufanya jambo lolote la huruma kwa yeyote wanayemsikia bila kujibakiza.

Mtu wa mtindo huu namfananisha na bomba yetu ya kawaida ambayo ukitaka maji yakupasa kuifungua na kutoa maji kadiri ya kiwango utakacho. Bombo hilii la maji ni lile tuitumiayao mabafuni mwetu. Hutoa maji yake kwa mpango mzuri sana. Kitu cha kushangaza ni kwamba pamoja na umakini wake, juu ya bomba hii huwa pakavu sana. Hata kama tupo mstari wa mbele kwa kuwahudumia watu kadiri ya upendo na ukarimu wetu, yatupasa kujikumbuka wenyewe. Hatupaswi kujisahau nafsi zetu. “Ukarimu huanzia nyumbani.” Iweje nimwone Yesu kwa wengine na kumsahau Yesu kwa wale ninaoishi nao kila siku? Hivyo, pamoja na huduma tuzitoazo kwa watu wengine zisizokuwa na shaka yoyote, hatupaswi kujisahau wenyewe.

Tumsifu Yesu Kristo!


MUNGU ANAKUPENDA UPEO, NA KWA SABABU HIYO HAPENDI UPOTEE. AMINA.

No hay comentarios:

Publicar un comentario