JUMAMOSI WIKI YA 14 YA MWAKA-B
11/7/2015
Somo: Mwa 49:29-33, 50:15-26
Zab: 104:1-4, 6-7
Injili: Mt 10:24-33
Nukuu:
“Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa,
walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda,”
Mwa 50:15
“Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama,
sisi tu watumwa,” Mwa 50:18
“Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa
mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo,” Mwa 50:20
“Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu
atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia
Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo,” Mwa 50:24
“Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika,
ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana,” Mt 10:26
“Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali
mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28
“Msiogope basi; bora
ninyi kuliko mashomoro wengi,” Mt 10:31
“Basi, kila mtu
atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele
ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 10:32-33
TAFAKARI: “Msiwaogope wauuao
mwili, wasiweze kuiua na roho.”
Wapendwa wana wa Mungu, hofu inapokutawala huaribu kabisa
mfumo wa kufikiri na kukujaza taswira zenye kukuzidishia wasiwasi. Ndugu zake
Yusufu wanajawa na hofu kwa yale waliyomtendea. Mtetezi wao alikuwa Baba yao.
Baada ya kifo chake, usalama haupo tena. “Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa,
walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda,”
Mwa 50:15. Kwa tendo walilomfanyia Yusufu mfanano wake ni sawa na kuwa mtumwa. “Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu,
wakasema, Tazama, sisi tu watumwa,” Mwa 50:18. Ndugu yangu utendapo jambo baya
kwa yeyote yule yakupasa kuomba radhi na kuponyesha pale ulipopaumiza. Yusufu
akawaambia nduguze, “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa
mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo,” Mwa 50:20
Mara nyingi tutendewapo maovu kwa hulka yetu ya kibinadamu
hupenda kulipa lililo ovu. Kupitia Yusufu tunajifunza tunajifunza moyo wa
kusamehe na kuanza upya pasipo kuwa na hofu. Naye Yusufu anawabariki ndugu zake na kuwatakia
mema. “Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa,
lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi
aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo,” Mwa 50:24. Ndugu, tunapomfuata
Kristo kwa ukaribu, twakumbushwa kuishinda hofu na woga. Tunayepaswa kumwogopa
ni Mungu mwenyewe. “Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika,
ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana,” Mt 10:26. Ndugu yangu hata kama leo tutafinywa uhuru wetu tunapoishi
imani yetu, kweli hiyo ipo siku itajulikana wazi kwa watesi wetu. “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na
roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika
jehanum,” Mt 10:28
Tunapolishinda giza kwa matendo yetu ya mwanga, kutatutaka
kila mara kusimama katika kweli na kumshuhudia Kristo pasipo haya. “Basi, kila
mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye
mbinguni. Bali mtu ye yote
atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye
mbinguni,” Mt 10:32-33. Maisha yetu na ukiri wetu mbele za watu kuhusu Kristo
ndiyo ukweli huo utakao jidhihirisha mbele za Mungu siku ya hukumu ya mwisho.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUPE UJASIRI WA KUISHI USHUHUDA WA KWELI
No hay comentarios:
Publicar un comentario