IJUMAA WIKI YA 13 YA MWAKA-B
3/7/2015
Somo: Mwa 23:1-4, 19; 24:1-8, 62-67
Zab: 105:1-2, 3-4a, 4b-5
Injili: Mt 9:9-13
Nukuu:
“Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu,
na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako
nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke
tokea huko; na yule mwanamke
asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini
usimrudishe mwanangu huko,” Mwa 24:7-8
“Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara,
akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa
kwa mamake,” Mwa 24:67
“Naye Yesu alipokuwa
akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia,
Nifuate. Akaondoka, akamfuata,” Mt 9:9
“Naye aliposikia,
aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12
“Lakini nendeni,
mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana
sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mt 9:13
TAFAKARI: “Nawe umeitwa
kutukumika kwa ajili ya ufalme wa Mungu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa namna ya pekee tujikumbushe sababu ya kuumbwa kwetu, kadiri
ya katekesi tuliyoipata katika hatua za awali za ukristo wetu. Mafundisho haya
ya Kanisa yanatufundisha kwamba “tumeumbwa ili tumjue, tumpende, tumtumikie na
mwisho turudi kwake mbinguni.” Hii ndiyo sababu ya kuumbwa kwetu, na ndiyo
sababu ya uwepo wetu hata dunia.
Ibrahimu
anafahamu vizuri sababu ya kuumbwa kwake na ahadi zote Mungu alizofanya naye
katika maisha yake yote. Pamoja na umri wake kusongea, Ibrahimu kamwe hakuweza
kusahau maagano ya Mungu. Mke wake keshafariki, nawe amebaki na mwanawe Isaka.
Isaka umri wa kuwa na mji wake umewadia. Ibrahimu kama Mzazi anayejali na
kuwajibiki, anakuwa makini sana kumtafutia mtoto wake mke. Ibrahimu anayafanya
haya yote kwa kutambua sababu ya uwepo wake. Naye anasema, “Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika
nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema,
Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe
utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na
yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki;
lakini usimrudishe mwanangu huko,” Mwa 24:7-8. Hii ni changamoto kubwa kwa
wazazi wetu wa leo. Familia zetu leo zinajiendea zenyewe kama saa za “SEIKO,”
yaani ukishaijaza ufunguo unaiacha ijiendee yenyewe. Je, wewe kama Baba au Mama
katika familia unakaa na watoto wako waliopevuka na kujua mahangaiko yao? Ni
vyema kama mzazi ukatumia angalau nusu saa kila wiki kwa kuongea tu na watoto
wako. Ni vizuri watoto wako kutofahamu ratiba hii. Yakupasa kama mzazi
kuongelea mambo yale ya kawaida tena yanayozunguka jamii yako.
Isaka anapata jiko na huzuni aliyokuwa nayo kuhusu kufariki
kwa mama yake Sara inatoweka. “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara,
akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa
kwa mamake,” Mwa 24:67. Huu ndiyo ule mkamilishano tunaouona katika fumbo la
ndoa. “Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa
yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa
katika mwanamume. Kwa hiyo
mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao
watakuwa mwili mmoja,” Mwa 2:23-24
Wapendwa wana wa Taifa ya Mungu, kila mmoja wetu kadiri ya
wito wake, anapoishi hapa duniani yampasa kujua sababu ya kuumbwa kwake.
Tunapojua sababu ya kuumbwa kwetu ni kwa namna hiyo twafahamu kuwa maisha ya
kila mmoja wetu ni wito maalumu. Maisha kama wito, yanatudai kujitoa sadaka kwa
kile tulichochagua kuishi kwa kuwezeshwa na Mungu mwenyewe. Leo katika Injili
tunaona namna Mathayo alivyochaguliwa na mara kuacha mpangilia wa maisha yake
ya zamani. Kuujua wito wako ni kuanza mpangilia mpya wa maisha yako. Hivyo, “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi
forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata,” Mt 9:9.
Ukweli ni kwamba tendo hili la kumfuata Yesu katika mazingira aliyokuwa nayo
Mathayo, linamlazimu muhusika kujimamanua kutoka yale aliyojifungamanisha nayo.
Mathayo anaamua kuiacha kazi yake ya ukarani na kumfuata Yesu ambaye hana
chochote katika maisha linganishi, ila uzima wa milele. Yesu anasema, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana
wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kumfuata Yesu kwa ukaribu na
uthabiti, kunatualika kuitafakari changamoto hii.
Kitendo
cha Yesu kumchagua Mathayo kuwa mmoja wa Mitume wake na kula pamoja na wenye
dhambi kinawakasirisha sana Mafarisayo. Yesu anawajibu Mafarisayo kwa kulenga
sababu ya uwepo wake hapa duniani: “Wenye afya hawahitaji
tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12. Yesu amekuja kwa sababu ya wale wenye
uhitaji wa mwili na roho. Yesu amekuja kwa ajili ya wadhambi na wale wote wenye
moyo wa hofu ya Mungu. Hili ndilo fumbo tunalotakiwa kulitafakari kila siku.
Pili, ni Mungu peke yake wenye kutuhesabia haki. Hivyo, “Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka
rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye
dhambi,” Mt 9:13. Ndugu yangu, embu ona Yesu anavyokupenda kupita upeo.
Kuuthaminisha upendo huu ni kuishi kadiri ya mpango wa Mungu na yale yote
Mwanaye Mpendwa aliyotufundisha.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE YESU,
NIONGOZE NA KUNILINDA KATIKA WITO ULIONIITIA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario