martes, 7 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 14 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 14 YA MWAKA-B
8/7/2015
Somo: Mwa 41:55-57; 42:5-7,17-24a;
Zab: 32
Injili: Mt 10:1-7
Nukuu:
Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote,” Mwa 41:57

Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani,” Mwa 42:5

Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao,” Mwa 42:7a

Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata,” Mwa 42:21

Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt 10:1

Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti,” Mt 10:4 

Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli,” Mt 10:5-6

Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7

TAFAKARI: “Na tushinde ovu kwa wema.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni wachetu tu kati yetu tunapotazama historia ya maisha yetu na kuona kwamba hatujaumizwa, na wala hatuna maumivu ya ndani. Hata hivyo ili chuma kiwe imara na thabiti katika kuhimili mishindo na mitikisiko ya hali kimazingira, yakipasa chuma kile kiwe kipite katika moto mkali. Chuma kuwa imara ni ishara kwamba chuma kile kimepita katika moto mkali sana ambao umekipa chuma mwono huo.

Mfano huu wa chuma imara hauna tofauti na maisha ya kiroho yenye ukomavu. Ukomavu wa maisha ya kiroho ni utambuzi ule wa kuona mbele zaidi hasa kwenye uzuri na malengo ya maisha yako na wale wanaokuzunguka. Ni kuelewa kwamba upo hapa nduniani kwa malengo maalumu. Ni kuwa na ufahamu kwamba ulikuwepo jana, upo leo na kesho, na siku zote za maisha yako hapa duniani kama ‘mmisionari.’ Unapo fahamu jambo hili kwa kina chake, kamwe huwezi kuongozwa na vionjo wala ulipizaji wa visasi ambavyo hapo mwanzo vilikutesa na kuwa sababu ya kutokuwa na mwelekeo chanya wa maisha.

Tulitazamapo somo letu la kwanza na kulitafakari tunaweza kugundua ni kwa namna gani Yusufu alivyoumiazwa kwa kutoswa na ndugu zake ikiwa sababu kubwa ya maumivu hayo ni wivu. Yusufu aliuzwa utumwani, na baadaya kuwa na nafasi kubwa ya kuwaudumia watu kama leo cheo cha Waziri Mkuu. Tunaona tatizo la njaa linakuwa sababu ya kukutana na ndugu zake. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote,” Mwa 41:57. Hakika kama waswahili wasemavyo njaa haina adabu, ndivyo ilivyotokea kwa ndugu zake.

Mara nyingi Mungu anapotufundisha tuushinde uovu kwa wema, hutukutanisha na wenzetu kwenye matukio ya kuhusunisha kama vile kifo, majanga ya asili, na matukio ya magonjwa tusiyoweza kuyamudu na wala kuyafahamu. Hivi ndiyo Yusufu alivyo ushinda uovu kwa wema kwenye tukio la njaa lililotokea nyakati zake. Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani,” Mwa 42:5. Hakika hii ilikuwa nafasi nzuri sana ya Yusufu kulipiza kisasi kwa kile ndugu zake walichomtenda. Yusufu alichokifanya ni hiki: “Akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao,” Mwa 42:7a. Yusufu anakaa kimya kuwapa ndugu zake nafasi ya kujirudi na kuzisoma alama za nyakati. Baada ya kuchomwa na dhamiri zao, ndugu zake wanatambua walichokitenda kwa Yusufu na kusemezana wenyewe kwa wenyewe: “Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata,” Mwa 42:21. Je, waswahili walikosea waliposema kufanya kosa si kosa ila kurudia kosa ni kosa?

Ni vizuri kutambua pale tulipowaumiza wenzetu, au mwenzako na kujaribu kwa namna yoyote ile kupaponyesha. Hili ni jambo la muhimu sana tunapoishi kama familia, au jumuiya yoyote ile ya Kikristo. Kutambua kosa na kufanya juhudi ya kuleta uponyaji, kitendo hicho hutuponya pia. Agizo la Yesu kwenye injili ya leo linatupa fursa ya kupambana na uovu bila kushindwa.  Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt 10:1. Hapa pia tunaalikwa kuushinda uovu kwa kutenda mema. Kama asemavyo Mt. Agustino; “ovu ni kutokuwa na mafaa,” kushinda lililo ovu ni kutenda lililo jema.

Ndugu yangu unayesafiri nami sasa, ‘misioni’ yetu hapa duniani kama watu wenye hofu ya Mungu ni kuwarudisha kundini wale waopotea au kukwazika kutoka na utendaji wetu wa awali au sasa. Ni mwaliko pia wa kujisahihisha pale tunapokosea. Yatupasa sana kuepuka kishawishi kile cha kusema ‘mkubwa na mwenye madaraka au cheo hakosei.’ Kasumba hii ni saratani mbaya sana katika utume wetu kama Kanisa mahalia. Kama sisi ni binadamu, na ndivyo tulivyo, basi kukosea kupo. Kama kukosea kupo, kutambua na kujirekebisha ndipo kunakotuhesabia haki mbele ya Mungu juu ya utendaji wetu na dhamana tuliyopewa na Mungu mbele za watu na kondoo wa malisho yake. Hivyo Yesu anawatuma,  na kuwaagiza, akisema, “Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli,” Mt 10:5-6. Yesu analifanya hili kwa Thenashara wote ili hali akijua mmoja wao atamsaliti.  Hivyo,Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti,” Mt 10:4. Je, twaweza kuushinda uovu kwa kuzidi kutenda lililo jema na hata kuendelea kuona uzuri kwa wenzetu hata kama tumegundua njama na hila zao? Katika jambo hili bila shaka Yesu anatukumbusha thamani ya mtu na utu wake. Mt. Agustino anasema hivi: “usimchukie mtu yeye, bali zichukie tabia zake mbaya.”

Mwisho kauli mbiu yetu: jana, leo, na kesho na iwe kuhubiri kusiko kikomo kwamba ufalme wa mbinguni umekaribia. Tunalisema hili iliwa ndiyo kauli mbiu ya Kanisa kama sakramenti ya wokovu wetu. Tunalihubiri hili kwa wengine tukijua kwamba ndani yetu na nafsini mwetu twauona na kuuonja ufalme huo. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE NEEMA YA KUSHINDA UOVU KWA KUTENDA MEMA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario