IJUMAA WIKI YA 15 YA MWAKA-B
17/7/2015
Somo:
Kut 11:10-12:14
Zab:
115:12-13, 15-18
Injili:
Mt 12:1-8
Nukuu:
“Musa na Haruni
walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa
mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake,” Kut 11:10
“Lakini nawaambieni,
kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu,” Mt 12:6
“Lakini kama mngalijua
maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na
hatia,” Mt 12:7
TAFAKARI:
“Mungu anayathamini maisha yako kuliko kitu kingine chochote.”
Wapendwa
wana wa Mungu, mara nyingi katika tafakari zangu nanyi nimekuwa nikikuambia
kwamba wewe si bahati mbaya. Mungu wetu huyu, “anayathamini maisha yako kuliko
kitu kingine chochote.” Mungu kwa kulifanya hili katika dhamiri iliyo safi,
huthamini sana maisha yetu kwani yanachapa yake. Yeye ametuumba kwa sura na
mfano wake. Hawezi kamwe kutupoteza kwa jambo lolote lile. Lakini kwa
kutufundisha, mara nyingine husababisa ugumu wa kufikia lengo lile kwa
kusababisha ugumu fulani. Mungu anachotaka tujifunze kutoka kwake ni hiki:
“Maisha yako ni ya thamani kubwa sana. Maisha yako ndiyo utajiri wako. Huwezi
kupanga wala kuwa karibu na Mungu wako kama maisha yako ni mgogoro. Ukiwa na
afya njema waweza kusali vizuri na hata kuyaboresha maisha yako kama yamekwenda
kombo.” Pili tunaimarishwa katika taabu na dhiki. Hivyo jambo hili linatokea
kwa Musa. “Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana
akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi
yake,” Kut 11:10. Hapa kwa tendo hili, wana wa Israeli wanaandaliwa kwa lile
lililo jema zaidi mbele ya safari.
Wapendwa
wana wa Mungu, Mungu hapendi sadaka zetu zisizo na uhusiano wa maisha yetu na
thamani yake. Mungu wetu hupenda rehema na neema anazotujalia pale tunapoziishi
kuliko kile tumtoleacho kama sadaka. Yote tumtoleayo ni mali yake. Vyote vipo
chini ya mamlaka yake. Hivyo Yesu anasema, “Lakini kama mngalijua
maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na
hatia,” Mt 12:7. Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka kutokana na mila na desturi
zetu, wakati fulani tulilazimika kufanya mitambiko na hata kutolea sadaka za
kuteketezwa zisizo na uhusiano na imani yetu. Kwa kufanya hivi tunapoteza dira
na mwelekeo wa Kimungu katika maisha yetu. Je, naweza kuwa huru hata kama
naishi katika mila na desturi hizi?
Tumsifu
Yesu Kristo.
EE
YESU, TUWEZESHE TUYAONA MAISHA YETU KAMA MALI YA MUNGU NA ZAWADI YA MUNGU.
AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario