domingo, 12 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 15 YA MWAKA-B

JUMAPILI  YA 14 YA MWAKA-B
12/7/2015
Somo I: Amo: 7:12-15
Zab: 84:9-14
Somo II: Efe 1:3-14
Injili: Mk 6:7-13
Nukuu:
Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli,” Amo 7:14-15 

Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake,” Efe 1:5

Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake,” Efe 1:7

“Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:10b-11

Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye,” Efe 1:13

akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili,” Mt 10:8-9

Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale,” Mt 10:10

Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao,” Mt 10:11 

TAFAKARI: “Hatupo kwa ajili yetu wenyewe, yote ni kwa neema ya Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kile ulicho na  yale yote uyafanyayo si kwa ajili yako mwenyewe, bali yamekuwa kama yalivyo kwa neema Mungu. Hakika hatuna kitu chochote tunachoweza kujivunia kama mali yetu binafsi. Vyote tumepewa kwa muda tu, na kama uangalizi. Ndugu yangu, fursa uliyonayo leo si bahati mbaya, ila kwa kupitia wewe Mungu ajulikane kwa wengine. Tunapotambua ukweli huu Mungu kamwe hatoacha kututumia kama apendavyo. Hivyo Nabii Amosi anatambua ukweli huu na kusema, “Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli,” Amo 7:14-15. Ukweli huu pia utunyenyekeza.

Wapendwa wana wa Mungu, yale yote tufanikiwayo na yenye mwono wa Mungu, ni uchanguzi wake Mungu mwenyewe na wenye mwelekeo wa ukombozi pale ulipo na umilele kwa kile ukitarajiacho. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake,” Efe 1:5. Je, najitambua napoyaona mafanikio yangu kuwa ni mkono wa Mungu anayetaka kuyafanya hayo kwa wale wanaonizunguka kupitia Yeye Mwenyewe? Ukombozi wetu bila Kristo ni ndoto isiyowezekana. Hakuna yeyote awezaye kutukomboa isipokuwa Yesu mwenyewe. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake,” Efe 1:7. Ni kupitia Kristo tunapata masamaha wa dhambi zetu na kuwa huru kutoka utumwa wa dhambi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, leo hii tu warithi wa ufalme wa Mungu kwa sababu tumekombolewa kwa damu ya Kristo. “Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:10b-11. Kwa warithi wa ufalme wa Mungu ni kuwa na uhakika wa kuishi milele. Jambo hili kwa upande mwingine haliwezi kutokea kama hatutatimiza wajibu wake. Kila mmoja wetu kwa ukiri wake mbele ya Kristo yampasa kuishi kadiri ya ahadi zetu za ubatizo.

Kwa ukombozi tulioupata kupitia Kristo sisi sote tumepewa muhuri wa Roho Mtakatifu. Ukweli ndiyo utakao tuweka huru na kweli hiyo ndiyo kielelezo cha yale yote tuyafanyayo. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye,” Efe 1:13. Tupo huru ndani na katika Kristo. Imani yetu bila Kristo ni sawa na kurusha ngumi kwenye upepo.

Tunapoyaishi haya katika uhasilia wake, maisha hayo yote yanatulazimu kufanya kinyume cha yale tuliyoyazoea. Yesu akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili,” Mt 10:8-9. Fimbo ni ishara ya mamlaka ambayo kwayo tumepewa na siyo kujitwalia wenyewe. Mamlaka haya si katika nguvu na kutawala, ila nguvu zitokanazo na maadili mema. Na katika kutenda kwetu, yatupasa kufanya jambo moja kwa wakati na siyo kujichanganya kwa mambo mengi kwa wakati mmoja. Yesu Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale,” Mt 10:10. Katika utume wetu, yatupasa kufanya kile tulichokusudia kukifanya bila kujibakiza. Tulifanyalo jambo hilo kwa uaminifu mambo hayawezi kwenda sawa kila wakati. Tutegemee upinzani wakati mwingine na hata kukataliwa. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao,” Mt 10:11. Tendo hili la kukung’uta mavumbi ya miguu la maanisha kwamba waliotufukuza au kutokupokea yale tuliyowaambia yaliyo kweli, ni kweli hiyo hiyo itakayowahukumu.

Ndugu yangu, tupo kwa ajili ya wengine na kile tulicho si kwa sababu yetu wenyewe.


Tumsifu Yesu Kristo!

No hay comentarios:

Publicar un comentario