JUMANNE WIKI YA 15 YA MWAKA-B
14/7/2015
Somo: Kut 2:1-15a
Zab: 68
Injili: Mt 11:20-24
Nukuu:
“Mtoto akakua, naye
akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni
kwa sababu nalimtoa majini,” Kut 2:10
“Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea
ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo
wa ndugu zake. Basi akatazama huko
na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani
ya mchanga,” Kut 2:11-12
“Basi Farao alipopata
habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa
katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima,” Kut 2:15
“Ole wako, Korazini!
Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika
katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu,” Mt
11:21
“Walakini nawaambieni,
itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko
wewe,” Mt 11:24
TAFAKARI: “Sikio la kufa halisikii dawa.”
Wapendwa wana wa Mungu, msemo huu wa Kiswahili, “sikio la
kufa halisikii dawa,” utusaidie katika tafakari yetu ya leo. Katika somo letu
la kwanza tunaona namna ambavyo Musa anavyookolewa na kutunzwa kwa namna ya
ajabu hadi kuwa mtu mzima na kuendeleza kazi ile ya ukombozi wa wana wa
Israeli. “Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe.
Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini,” Kut 2:10.
Mtoto huyu aliyeokolewa kutoka majini, Musa, anakuwa kielelezo na mkono wa
Mungu. Hata hivyo Musa anapata upinzani kutoka kwa ndugu zake licha ya utetezi
wake na juhudi zake kuliokoa Taifa lake. “Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea
ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo
wa ndugu zake. Basi akatazama
huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha
ndani ya mchanga,” Kut 2:11-12
Ni jambo gumu
sana kuelewa ubaya wa kitu ndani ya mfumo wa kitu kile. Waisraeli wangetamani
sana kuendelea katika mateso yale kuliko kujaribu upande wa pili wa maisha
wasiyoyajua. Ni hali ya kawaida binadamu kuwa na hofu kwa kile asichokijua,
hasa mambo yale yamtoayo kwenye mang’amuzi yake ya kila siku. Hapa ndipo
tunaposema, “heri nusu shwari kuliko shwari nzima.” Musa anajaribu kuwaonyesha
upande wa pili wa uhalisia wa mambo, lakini ndugu zake wanafanya upinzani juu
ya ukweli ule.
Nasi leo
tunaitaji kutoka kwenye utumwa wa fikra na kuyaona mambo kama yalivyo. Tumejawa
hofu ya tusichokijua na tumekuwa
watumwa kwa hofu hii. Hatuwezi kwenda mbele kama hatupendi kufanya tofauti ya
yale tuliyoyazoea kila siku, na miaka yote. Ujasiri ya Musa unamtia matatani.
Habari za mauaji ya yule Mmisri zilizovujishwa na jamaa yake Musa inakuwa
sababu ya Musa kutoroka na kuinusuru roho yake. “Basi Farao alipopata
habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa
katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima,” Kut 2:15
Mara zote tunapopambana na
kweli, au kujikwamua kwenye shida fulani, mawazo pingamizi hayakosekani. Ugumu
huu wakati mwingine husababishwa na kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa jambo
lile. Huku ndiko tunaposema kwamba sikio la kufa halisikii dawa. Jambo hili
ndilo analolisema Yesu anapoitazama miji ile iliyokithiri kwa uovu. “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa
kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni,
wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu,” Mt 11:21. Ni mara ngapi
tunaambiwa ukweli wa mambo lakini mara zote tunabakia na ushabiki usiokuwa na
tija yoyote? Kwa nini hatupendi kuona ukweli kama ulivyo na badala yake
tunaupindisha? Katika jambo hili, Yesu anatupa angalisho na kusema, “Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya
Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe,” Mt 11:24.
Wapendwa, hawatashuka malaika kutoka mbinguni na kutuambia
mambo haya zaidi ya watu wenye uelewa tunaoishi nao kila siku kutuambia kweli
hiyo. Mungu utumia watu wake
kulisemea lile lililo ovu. Watu wenye maadili mema na mwono chanya, walisemapo
jambo yatupasa kusikia na kulipembua kwa kina. Je, yote yasemwayo kuhusu maisha
yako, hali yako, na Taifa lako hayana ukweli? Je, unaridhika na hali hii?
Umechukua hatua yo yote?
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE YESU
YAFUNGUE MACHO, MIOYO NA AKILI ZETU ILI TUYAONE MAMBO KAMA YALIVYO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario