JUMATATU
WIKI YA 14 YA MWAKA-B
6/7/2015
Somo:
Mwa 28:10-22
Zab:
90
Injili:
Mt 9:18-26
Nukuu:
“Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa
Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao
wako,” Mwa 28:13
“Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa
magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika
uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa,” Mwa 28:14
“Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta
tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo
niliyokuambia,” Mwa 28:15
“Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa,
wala mimi sikujua,” Mwa 28:16
“Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia
niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani
nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu,” Mwa 28:20-21
“Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na
katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi,” Mwa 28:22
“Alipokuwa akiwaambia
hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi
amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi,” Mt 9:18
“Na tazama, mwanamke
aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa
nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake,” Mt 9:20
“Yesu akageuka,
akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule
mwanamke akapona tangu saa ile,” Mt 9:22
“akawaambia, Ondokeni;
kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana,” Mt 9:24
TAFAKARI:
“Mungu huawaridhia walio wake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
usalama wetu wa mwili na roho upo mikononi mwa Mungu aliyetumba kwa sura na
mfano wake. Mungu aliyeupendo na huruma, mara zote hufurahishwa na maisha yale
yanayompendeza kulingana na upendo na huruma anotujalia kila siku. Hivyo leo
tuongozwe na tafakari hii: “Mungu huawaridhia walio wake.” Yakobo anaridhiwa na
Mungu na kutangaziwa mambo makuu. Licha ya kwamba neema na baraka alizozipata
Yakobo kutoka kwa baba yake zilikuwa za udanyanyifu, huruma na msamaha ni kwa
Mungu mwenye mamlaka hiyo pasipo shaka. Naye Mungu anamridhia Yakobo kwa
kusema, “Mimi ni Bwana, Mungu
wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na
uzao wako,” Mwa 28:13. Je, twatambua kuwa nchi yetu ndiyo mahali petu na hatupo
hapo kwa bahati mbaya? Je, twaona uchungu na kuchukua hatua kwa faida ya umma
tunavyoona baadhi yetu wakijineemesha kwa rasilimali za taifa hili? Je, Baba wa
Taifa hili, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere angekuwa mbinafsi na mtaka
vyake na familia yake, leo viongozi tulikuwa nao wangepata hivyo
wanavyovitapanya? Kwa nini tunashindwa kumuishi Baba huyu wa Taifa hili na
alama na kielele cha Imani aliyokuwa nayo Baba Ibrahimu kwa Waisraeli? Je,
hatuoni tena siku hizi?
Mungu anapotujalia
neema na baraka kesha tazama miaka mingi ijayo juu ya kila mmoja wetu. Je,
wakati ujao unamaana yoyote kama leo tunatapanya kila kitu kwa ulafu na ufisadi?
Twaweza kweli kumlaumu Mungu kwa mipango yake mizuri juu yetu na kizazi
kijacho? Yakobo anahaidiwa na Mungu uzuri huo wa nyakati zijazo. “Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe
utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika
wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa,” Mwa 28:14.
Tunapoishi kadiri ya mpango kazi wa Mungu ndivyo tunavyobarikiwa na mataifa
yatuzungukayo ndivyo yatakavyobarikiwa. Je, baada ya miaka 50 ijayo tukiwa wote
ni watumwa katika nchi yetu, baraka hizo zitakuwepo? Je, mataifa yatuzungukaya
nayo yatabarikiwa kwa utumwa wetu?
Wapendwa, tunapata
ulizi wa Mungu kila tuendapo iwapo tu tunaishi kadiri ya mpango kazi wake,
yaani kuishi kadiri ya maagizo yake. Maagizo makuu ya Mungu kwetu ni kuishi
upendo na kila mmoja wetu. Uonyeshapo upendo kwa mwenzako ni kutambua kuwa
upendo aliokupa Mungu kwa kukuumba kwa sura na mfano wake, ni upendo huo huo
uliopo kwa mwenzako, na huyo ndiye Mungu anayeishi kati yetu kila siku, (rejea
Mt 25 yote). “Na tazama, mimi nipo
pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa
maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia,” Mwa 28:15. Je,
tunaulizi imara zaidi ya ulinzi wa Mungu? Ona masikini wanavyolala kwa amani bila
hata kufunga milango yao! Tumaini lao lote lipo kwa Mungu. Umasikini si tu ule
wa kutokuwa na kitu, au upungufu wa kiungo fulani cha mwili, bali umasikini wa
kuwa na nafasi ya Mungu katika maisha na moyo wako.
Tunapotambua ukweli
huu katika maisha yetu, yatupasa kuwa na malengo kuhusu maisha yetu. Malengo
katika maisha ni moja ya kujitambua kwamba haupo hapa duniani kwa bahati mbaya.
Pili haupo hapa duniani kupitisha muda tu. Mungu anakutaka ufanye kitu kwa
ajili yake. Kitu hicho kiwe na mwono wa ukombozi kwa taifa lake. Wewe unakuwa
sasa ndiyo miguu, mikono, masikio, macho, mdomo, na ladha ya Mungu. Hivyo
Yakobo anaweka malengo yake baada ya kutambua sababu ya uwepo wa Mungu katika
maisha yake. “Yakobo akaweka nadhiri
akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa
chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba
yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu,” Mwa 28:20-21. Je, Mungu wako
unayemwamini ni nini katika maisha yako?
Kujibu swali hili:
Mungu ni nini katika Maisha yako, lisibakie katika nadharia. Jambo hilo au jibu
hilo liweke katika vitendo. Mtume Yakobo anasema hivi: “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini
mwake,” Yak 2:17. Yakobo mwana wa Isaka anaweka imani yake katika matendo. “Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa
nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya
kumi,” Mwa 28:22. Je, unamtolea Mungu moja ya kumi ya mapato yako? Twawezaje
kupata baraka kama hatushukuru hata kwa kile kidogo tulichokirimiwa?
Wapendwa wana wa
Mungu, wakati nyakati zilipotimia Mungu aliyekuwa mbali sana katika uelekezaji
na utendaji alikuwa Emmanueli yaani, Mungu pamoja nasi. Ukaribu wa Mungu nasi
kwa kupitia mwanaye mpendwa Yesu Kristo, ni hakikisho la uzima ndani yetu.
Mungu wetu ni hai muda wote. Uwepo wa neno aliyefanyika mwili ni uhai katika
miili yetu hii inayokufa. Na hivyo, “Alipokuwa akiwaambia
hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi
amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi,” Mt 9:18. Uhai
ndani na katika Kristo unaonekana kwa wote wale waliomridhia. Kristo ndiye
kimbilio letu na uhai wetu. “Na tazama, mwanamke
aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma,
akaugusa upindo wa vazi lake,” Mt 9:20. Mwanamke huyu anaona uhai ndani na
katika Kristo. Analishika pindo la vazi la Yesu kwa imani na anapona. Naye Yesu
anamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke
akapona tangu saa ile,” Mt 9:22. Je, unaimani thabiti na Yesu Kristo, Bwana na
mwokozi wa Maisha yako?
Wapendwa
katika Kristo, Bwana wetu Yesu Kristo akiwa njiani kufanya uponyaji, anakutana
na taarifa za kuhuzunisha kwamba uhai ule anaoukimbilia haupo tena. Kwa vile
yeye ni Bwana wa Uhai na amekuja kwa sababu hiyo ya uhai tena tuwe nao wa
kutosha, anasema, “Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu,” Mt 9:24.
Kifo ni usingizi tu. Wote wenye kumridhia Mungu wataamshwa kutoka uzingizi wao
siku ya mwisho. Je, bado umelala? Amka na mfuate Kristo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
MWANA
NDIYE MCHUNGAJI WANGU SITAPUNGUKIWA NA KITU. AMINA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario