sábado, 4 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 14 YA MWAKA-B

JUMAPILI WIKI YA 14 YA MWAKA-B
5/7/2015
Somo I: Eze 2:2-5
Zab: 122
Somo II: 2Kor 12:7b-10
Injili: Mk 6:1-6
Nukuu:
Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao; Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao,” Eze 2:4-5

Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi,” 2Kor 12:7

Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu,” 2Kor 12:9 

Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10 

Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?” Mk 6:2

Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4

TAFAKARI: “Simama katika kweli, tenda lililo kweli; Lenge mara zote kwenye ukamilifu ingawa kama binadamu kuna udhaifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama anaadhimisha Dominika ya 14 ya mwaka “B” wa Kanisa. Mama Kanisa leo anatutaka tuelekeze tafakari yetu katika neno hili: “Simama katika kweli, tenda lililo kweli; Lenga mara zote kwenye ukamilifu ingawa kama binadamu kuna udhaifu.” Kweli ndiyo msingi wa yale yote tuyanenayo na kuyasimamia, na mwisho wa siku kweli hiyo ndiyo itakayotuweka huru. Yesu analisema hili kwa msisitizo mkubwa, “ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31b-32. Jamii yetu leo, na hasa Taifa letu linapotea kabisa kwa sababu ya kutokusimama katika kweli. Huwezi kusimama katika kweli kama wewe ni muumini wa ubinafsi. Huwezi kusimama katika kweli kama wewe ni muumini wa ufisadi. Huwezi kusimama katika kweli kama wewe ni muumini mwabudu sifa za viongozi dhalimu waliokupa nafasi hiyo kwa maslahi yao binafsi. Na huwezi kusimama katika kweli kama wewe ni muumini wa uongo.

Nachelea kusema kwamba leo kama Taifa kundi kubwa la viongozi wetu tuliokuwa nao ni waamini wa sifa nilizozitaja hapo juu. Kila kukicha wanaliuza Taifa la wana wa Mungu vipande vipande, na ifikapo jumapili tupo nao Makanisani, na hata Misikitini tukimsifu na kumwabudu Mungu. Huku ni kumchezea Mungu aliye hai, na kuna kila sababu ya kupata adhabu kubwa mbele za Mungu. Ndugu wa Taifa hili la Tanzania, leo hatupo kwenye ardhi hii kwa bahati mbaya. Mungu wakati fulani aliona inafaa Taifa hili liwepo na liishi mahali hapa. Tunapoona viongozi wa ngazi za juu wanaliuza Taifa hili vipande vipande kwa vigezo vya kuingia mikataba ya ovyo kwa manufaa yao na familia zao, yatupasa kama Taifa kupiga magoti na kumlilia Mungu.

Leo kadiri ya Somo letu la kwanza, tunahitaji viongozi kama Nabii Ezekieli aliyesimama na kusema kweli bila kupepesa macho. Mungu anasimamia haki za wanyonge wake kwa kuwatumia watu wenye hofu ya Mungu kama Nabii Ezekieli na kusema: Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao; Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao,” Eze 2:4-5

Ni ukweli usipingika kwamba hakuna mwanadamu aliyekamilika. Kila mmoja wetu, na hata viongozi wetu tulio nao wanamadhaifu yao kama wanadamu. Tatizo kubwa tulilonalo ni pale tunahalalisha udhaifu wetu, na kuwasadikisha wale waliotuweka madarakani kuwa huo ndio mtindo wa maisha. Ni vyema tunapotambua udhaifu wetu iwe dawa ya kujirekebisha na kufanya vizuri zaidi. Hii ndiyo sifa mojawapo ya kiongozi, yaani “kujisahihisha.” Kiongozi asiyejisahihisha ni hatari sana kwa wale anaowaongoza. Kama viongozi, katika shughuli zetu si kila mara mambo yatakwenda vema. Tunaweza kukosea hapa na pale. Basi tuwe tayari kusahihishwa na kujisahihisha. Tujisahihishe kweli. Tunajifunza kutoka makosa yetu na ya wenzetu. Zaidi ya hayo tusiyaache makosa yatokee kwa makusudi. Tujitahidi kuzuia makosa na mapungufu mengine yoyote yasitokee. Tulenge kwenye ukamilifu ingawa kuna udhaifu pia.

Udhaifu wenye mwono wa kujisahihisha na kusimama katika kweli, ndiyo Mtume Paulo anauzungumzia kama “Mwiba.” Mtume Paulo anamwomba Mungu mara tatu amwondolee mwiba huu.  Baada ya kulifahamu tatizo lake, Mtume Paulo anatumia tatizo hilo kujiimarisha zaidi katika kweli. Jibu la tatizo lake ni UNYENYEKEVU katika kutenda. Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi,” 2Kor 12:7. Ndugu yangu, je, unaliona jambo hili ndani yako, na kwa viongozi tulionao sasa? Tusipofanya uamuzi wenye tija na hasa kuanzia kwako na kwangu, baada ya miaka 50 ijayo watu wate wa Taifa hili la Tanzania tutakuwa watumwa katika nchi yetu wenyewe. Neema na baraka alizotujalia Mungu zitakuwa sababu ya mateso yetu yasiyokuwa na kikomo.

Mtume Paulo anaona nguvu kubwa ya kusimama katika kweli, baada ya kutambua udhaifu wake. Ndugu yangu, kichaa si kichaa tena anapotambua yeye ni kichaa. Tatizo kubwa la Watanzania tulio wengi bado hatujajitambua kama Taifa, vipau mbele vyake, sababu zake, na hatima yake. Mtume Paulo anapata nguvu kusimama katika kweli baada ya kujitambua. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10. Wapendwa, nguvu katika udhaifu twaipata tuwapo na hofu ya Mungu. Imani ni nguzo muhimu sana kwa kiongozi aliyepewa dhamana ya uongozi na watu. Imani hii ya hofu ya Mungu hutujaza neema ya kusimama katika kweli na kuitenda kweli. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu,” 2Kor 12:9. Kiongozi asiye na Imani ni hatari kubwa. Kiongozi yambidi kusadiki bila kutikisika kile atakacho wafundisha wengine. Yeye mwenyewe awe na imani imara na kuishi kadiri ya imani hiyo.

Imani aliyokuwa nayo kiongozi ndiyo inayomwezesha kuishi kidini na siyo kuwa mdini. Kuishi kidini ni kuwa na hofu ya Mungu kwa yale yasiyompendeza Mungu, na hivyo kutenda mara zote yanayompendeza Mungu. Haiwezekani kiongozi kujilimbikizia mabilioni ya pesa peke yake, ilihali watu wake anaowaongoza ni masikini wa kutupwa. Kiongozi huyu haishi kidini ila ni mdini. Amejawa ubinafsi uliopindukia. Lengo la dini ni kufikia ukamilifu. Kwa hiyo mafundisho ya dini ni muhimu kabisa kwa ajili ya maendeleo ya kimwili na kiroho. Yampasa kiongozi ayajue mafundisho ya dini, ayashike na kuishi mwenyewe kadiri ya mafundisho hayo. Tabia njema inatokana hasa na mafundisho ya dini. Kiongozi unapoishi ukweli huu, lazima watu watakushangaa hasa wale walio kwenye giza.

Katika Injili tunaona jinsi Yesu anavyosimama katika kweli, kutenda lililo kweli bila kujali mitazamo ya watu wake na yale waliyoyapokea enzi na enzi. Yesu anasimama kama alama ya matumaini mapya na mabadiliko kwa watu wake. Yesu leo ndiye kielelezo kikuu cha kusimama katika kweli, kutenda lililo kweli, na kufia lililo kweli. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?” Mk 6:2. Siri kubwa ya Utendaji wa Yesu ipo katika kile alichokiamini na ndicho alicho. Naye anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Kiongozi asionyesha njia, aliye mwongo, na asiyeleta uhai kwa watu, huyo hapaswi kuongoza watu. Kiongozi wa mtindo huo ni JANGA!

Changamoto kubwa ya kuishi kweli, kutenda kweli, na kuifia kweli, ni kutengwa na wale walio gizani ambao kwa idadi huwa wengi sana. Matendo ya gizani hupendwa sana na wengi kwa sababu huficha soni ya mtu. Yesu analijua hili na anawambia ukweli huo wale waamini wa matendo ya giza kwa kusema, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4. Ni ukweli uliowazi kwamba utasongwa na mambo mengi ila kama kiongozi yakupasa kuona ni wangapi wapo nyuma ya kile unachokipigania kwa manufaa ya umma wa watu. Kwa sheria na mitazamo mibovu ya utawala dhalimu, wanaweza kuizima taa uliyoiwasha, ila ukweli wa mwanga ule kamwe hawataweza kuutokomeza. Ni swala la wakati tu, na kweli itajulikana wazi mchana kweupe. Ni Mungu tu mwenye umilele na kweli yake haina ila wala shaka yoyote. Binadamu kwa ukorofi wake na udhalimu wake anauwezo wa kuangamiza mwili, ila roho hana mamlaka nayo.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, ona uchungu juu ya viongozi wako Kitaifa. Ona uchungu juu ya kizazi chako kijacho. Ona uchungu juu ya utumwa ujao baada ya miaka 50 katika nchi yako. Ona uchungu juu ya baraka na neema alizotujalia Mungu kwamba ipo siku hazitakuwa tena zako. Hivyo mimi na wewe tuwe majasiri wa kusimama katika kweli, kutenda lililo kweli, na kulifia lililo kweli. Tuwape nguvu viongozi wetu wachache waliogundua hila hizi za udhalimu. Tuwe kitulizo chao hasa tunapowakumbuka kila siku kwenye sala zetu. Mungu kamwe hamtupi mja wake. Naye Yesu anatuambia kwa msisitizo mkubwa: Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28. Je, ni nani awezaye kutushinda kama Mungu akiwa upande wetu?

Mzee Richard Kitoweo alijulikana sana mtaani kwake kwa jina la “Mzee wa busara.” Siku moja Mzee huyu wa busara alienda mtembelea rafiki yake kijiji cha jirani nyakati za jioni. Akiwa kwa rafiki yake, mvua kubwa ilinyesha bila kukoma na hivyo kumwiya vigumu kurudi nyumbani kwake.

 Hata hivyo rafiki yake alimpa ukarimu wa kulala kwake kwa makubaliano atalala sebuleni kutokana na udogo wa nyumba na vile vile hana shuka za kujifunika. Hivyo Mzee wa busara alirudi nyumbani kwake akinyeshewa mvua na kuchukua shuka na kurudi kulala kwa rafiki yake. Hoja yake ni kwamba kwa rafiki yake kuna umeme na sebuleni pake kuna sofá nzuri, ili hali nyumbani mwake ameacha nyumba kubwa ikiwa na kitanda kikubwa pia.

Zaidi ya hilo, Mzee wa busara mara kwa mara  hujisifia kuwa na kitambi kikubwa kinachotokana na kula kwa jirani yake, na hata kujisaidia kwa jirani yake. Hupenda pia kuoga bafuni mwa jirani yake. Familia yake kwa miaka yote hiyo utumia mito na vichaka kwa huduma muhimu na za kiafya.

Wapendwa wana wa Mungu, Je, kunasababu yoyote kwa Mzee wa Busara kutumia jina hilo alilopewa na baadhi ya marafiki zake wa kijiji kile cha jirani? Kweli kunatofauti gani ya Mzee huyu wa Busara na viongozi wetu tulionao leo?  Je, familia yetu tunajisikiaje Baba anavyopenda kulala kwa rafiki yake kwa hoja anazozitoa? Je, siku nyumba yetu ikipigwa mnada (inchi) na rasilimali zake kwa bei poa, na kujidhalilisha kwa kijiji jirani (mataifa ya kigeni), unasababu yoyote ya kujitetea kama mwanafamilia (Mtanzania) mbele za watu? TAFAKARI SANA!!!!

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUPE UJASIRI WA KUSIMAMA KATIKA KWELI. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario