viernes, 3 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 13 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 13 YA MWAKA-B
4/7/2015
Somo: Mwa 27:1-5, 15-29
Zab: 134:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mt 9:14-17
Nukuu:
Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa,” Mwa 27:3-4

Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau,” Mwa 27:22

Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe,” Mwa 27:28-29 

Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga,” Mt 9:15

Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16

Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote,” Mt 9:17

TAFAKARI: “Upya ndani na katika Kristo”

Wapendwa wana wa Mungu, kufunga ilikuwa moja ya mambo makuu matatu kadiri ya Imani, mila na desturi za kiyahudu. Kufunga iliendana na kusali, pamoja na kutoa sadaka. Haya mambo matatu yalikuwa ya msingi sana. Kitendo cha wanafunzi wa Yesu kuonekana kutokufunga kiliwashangaza wengi, na hasa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji. Yesu anapoulizwa swali hili: kwa nini wanafunzi wako hawafungi, anajibu na kusema, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga,” Mt 9:15. Uhusiano wetu na Kristo una sura mbili; kuna wakati wa furaha na wakati wa huzuni, itupelekayo kwenye utukufu. Tukiwa na Yesu tu wana wa Bwana harusi na yatupasa kufurahi naye kuliko haki.

Kwa upande wa pili wa uhusianao wetu na Yesu unatukumbusha upo wakati wa kutoa ushuhuda wa kweli juu ya kile tunachoamini kuhusu Yesu. Huu ndio wakati wa kutesema na hata kufa kwa ajili ya Kristo. Huu ndio wakati wa kufanya toba ya kweli kwa ajili ya maaondoleo ya dhambi zetu. Huu ndiyo wakati wa kufanywa upya ndani na katika Kristo. Huu ndio wakati wa kutakaswa na kubeba bendera ya ushindi ya mwanakondoo.

Nyakati hizi mbili za mahusiano yetu na Kristo ndizo zitupazo kiini cha imani yatu. Sisi si wakristo wa Jumapili tu, yaani, pasaka, bali tu wafuasi wa Kristo siku zote na hasa siku ile ya Ijumaa, yaani mateso na kufa kifo dini. Tunakufa kifo dini kwa kuufia ukweli siku zote za maisha yetu. Yatupasa kusimama katika kweli, kufundisha iliyo kweli, kuishi yaliyo kweli, na kushuhudia lililo kweli, hata kama litagharimu uhai wetu. Haya ndiyo maisha ya ufuasi wa Kristo ambao tuliowengi hatutaki kusikia.

Jambo lingine la muhimu kujua ni hili: Yatupasa kuelewa lile lililo la zamani ambalo kwa sasa linakamilishwa na hili jipya, mbalo tangia awali lilikuwa limejifucha ndani ya lile la zamani. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16. Maana yake nini? Ndugu yangu, katika safari ya ukombozi wa mwanadamu, katika hatua ya mwanzo ya safari hiyo, imebebwa katika agano la mwanzo. Agano hili kama lilivyo laelezea historia ya mwanadamu hatua kwa hatua. Kwa lenyewe agano hili kama lilivyo linamaana ila limekosa ukamilisho au hitimisho. Ukamilisho wa Agano la kwanza ni Upya wa Agano jipya, ikiwa ni ufunuo wa wazi wa Mungu kwa tukio la neno kufanyika mwili. Agano hili jipya licha ya kwamba ni ukamilisho wa agano la kale, tangu mwanzo lilikuwa limejificha ndani ya agano la kale. Hivyo Yesu anatutaka kulijua jambo hilo na pia kutenganisha maagano haya mawili katika “umaana wake” na “nafasi zake.” Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote,” Mt 9:17. Hivyo katika jambo hili twapaswa kumfuata Kristo katika ukamilifu wote na kuachana na michanganyo. Ni heri kuwa baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani. Hili vuguvugu kiimani ndilo litakalo pasua hekalu hili la Roho Mtakatifu.

Uhusiano wetu na Mungu leo sio wa kiujanjaujanja kama tuonavyo katika somo la kwanza. Hata kama Mungu huweza kutumia njia za ajabu kufikia lengo la kumkomboa mwanadamu, tuishipo ndani na katika Kristo ukweli ndiyo utakaotuweka huru. Yakobo anapata baraka kutoka kwa Baba yake Isaka kwa ujanja na uongo wakisaidiana na mama yake. Haki ya Esau inahujumiwa. Kuliishi jambo hili leo ni kuishi mtazama wa kizamani ambao bado hujakamilishwa. Yesu ndiye njia, na ukweli, na uzima, (Yoh 14:6).

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU, TUJALIE TUISHI KATIKA KWELI YAKO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario