sábado, 18 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 15 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 15 YA MWAKA-B
15/7/2015
Somo: Kut 3:1-6, 9-12
Zab: 102:1-4, 6-7
Injili: Mt 11:25-27
Nukuu:
Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:5

Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa,” Kut 3:9 

Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu,” Kut 3:6

Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?” Kut 3:11

Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako,” Mt 11:25-26

TAFAKARI: “Mungu huyatenda makuu kwa wanyenyekevu wa Moyo.”

Wapendwa wana wa Mungu, tuitazamapo historia ya wokovu wetu, tunagundua kwamba Mungu hufanya kazi na wale wajishushao na wanyenyekevu wa Moyo. Licha ya tabia na mwono huu wa Kimungu, wale wate wanoshirikishwa mpango wa Mungu katika tendo la Kimungu, huwa ni watu wa kawaida sana, na mara nyingine huwa wale waliodharaulika na jamii husika. Mama Bikira Maria ni mmoja wa wale walioshiriki mambo makuu ya Mungu katika unyonge na unyenyekevu wake. Naye Bikira Maria analitambua jambo hili na kusema,  Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48.  Bikira Maria anatambua pia kile kinachotendeka kwake ni upendeleo wa Mungu ndani mwake, na hivyo kinamakusudio makubwa kadiri ilivyompendeza Mungu. Naye anasema, Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Jambo hili linatokea pia kwa Musa ambaye anapokea misioni hiyo kama kiongozi wa wana Waisraeli kuwatoa kutoka utumwani Misri.

Kazi anayopewa Musa inamlazimu kuyaacha yote yale yaambatanayo katika maisha yake ambayo hayampendezi Mungu. Mungu anapompa majukumu haya mazito na muhuhi anampa angalisho na kusema, “Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:5. Wapendwa wana wa Mungu, kuvivua viatu ni kuenenda na kufanya katika hali halisi ya kile ulichotumwa kufanya bila kuwa na hisi fulani kama miwani ya kutazamia uhalisia wa mambo. Mara nyingi tumewahukumu watu na hata kuwatenda ndivyo sivyo kutokana na mang’amuzi yetu yasiyoendana na uhalisia wa jambo. Mara nyingi tumewahukumu watu kutokana na historia zetu mbaya. Na mara nyingine tumeenda mbali zaidi katika kutenda na kuhukumu kulikotokana na simulizi za chuki juu ya wale tunaoishi nao zisizo za kweli. Hivyo kuvivua viatu ni kuzama ndani kabisa katika mila na desturi za watu tuliotumwa kwao ili kujua ukweli wa mambo. Yatupasa kuweka kando nadhania zetu za vitu, na kuuona ukweli kama ulivyo. Hili ndilo jambo la msingi Musa ilimpasa kulijua kabla ya kulitenda lile Mungu alilotaka alitende juu ya watu wake.

Wapendwa, mara zote mjumbe hulifanya lile alilotumwa kulifanya na Bwana wake. Hatupaswi kubadili ujumbe ule kwa kujiinua nafsi zetu. Hivyo Mungu anamtaka Musa alitende lile aliloliona juu ya mateso ya Wana wa Israeli. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa,” Kut 3:9. Agizo na mamlaka haya yanatoka kwa Mungu mwenye Mungu na aliye hai. Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu,” Kut 3:6. Neno hili ni lenye nguvu, na Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu na kile alichokiumba kwa sura na mfano wake. Hata hivyo, kazi aliyopewa Musa haikuwa rahisi. Hivyo Musa anajipima nguvu na ushawishi aliokuwa nao kwa watu wake na mtesi wake, Farao, na kujiona mdogo na dhaifu. Naye akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?” Kut 3:11. Huu ndio unyenyevu wa Musa mbele ya Mungu. Ndugu yangu, yapo mambo mengi katika utume wetu kila mmoja kadiri ya wito wake, kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi kufikia malengo. Hivyo tunahitaji msaada wa Mungu.

Kujishusha huku na kuwa wanyenyekevu mbele ya Mungu mwenye kuyaweza yote, ndiko kunakotutafakarisha maneno na sala hii ya Yesu katika Injili ya leo: Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako,” Mt 11:25-26. Je, twatoa shukrani kwa Mungu hata kwa kile kidogo Mungu alichotuwezesha kukifanya? Je, mafanikio niyapatayo natambua ni mkono wa Mungu, au ni akili zangu na ujanja wangu? Ndugu yangu, ‘moyo usio na shukrani hukausha mema yote.’

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE FADHILA YA UNYENYEKEVU. AMINA.

No hay comentarios:

Publicar un comentario