sábado, 11 de julio de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 14 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 14 YA MWAKA-B
Somo: Mwa 44:18-21, 23b-29; 45:1-5
Zab: 104
Injili: Mt 10:7-15
Nukuu:
“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.” Mwa 45:5

“Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8

“Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo ktika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu,” Mt 10:14

TAFAKARI: “Tusichoke kutenda lililo jema na lenye kumpendeza Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika ulimwengu tunaoishi leo unatutaka kufanya yale tu yanaotufurahisha moyo, na yale tu yanayotupa faida. Nje ya mafao hayo ni vigumu kufanya yale yanayompendeza Mungu. Masomo ya leo yanatufikarisha kuona furaha na umuhimu wa kufanya lililo jema na lenye kumendeza Mungu, hata kama kwa macho yetu na mtazamo wetu itaonekana ovyo. Yusufu analiona hilo na kuwaambia ndugu zake  maneno haya: “Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.” Mwa 45:5. Ni kweli kwamba ndugu zake Yusufu walifanya kitendo kiovu sana kwa kumuuza. Pamoja na maumivu haya, Yusufu haoni sababu ya kutosamehe na kuanza upya katika kumtumikia Mungu.

Katika somo letu la Injili tunaona usia wa Yesu wa kuhimiza maisha ya kutenda mara zote lile lililo jema na lenye kumpendeza Mungu kama tutatenda bila kujibakiza. “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8. Jambo la msingi la kuelewa juu ya ukweli huu ni kwamba tufanyacho ni kwa mkono wa Mungu nasi twafanya tu kama watumishi wanaotimiza wajibu wao msingi.

Ndugu yangu, tuyafanyavyo mambo haya hatufanyi kwa kumpendekeza mtu, bali twayafanya kwa kutimiza wajibu wetu  na hasa kwa kufanya lile linalompendeza Mungu. Hivyo,  “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu,” Mt 10:14. Kukung’uta mavumbi ya miguu ni kutenda lililo jema na kutokutegemea shukrani yoyote. Kama wapo watakao beza tendo hili la wema, adhabu yake ni hapa hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE NEEMA YA KUTENDA LILILO JEMA SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario