IJUMAA WIKI YA 18 YA MWAKA-B
7/8/2015
Somo:
Kumb 4:32-40
Zab:
76:12-16, 21
Injili:
Mt 16:24-28
Nukuu:
“Basi, zishike sheria
zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako
baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako,
milele,” Kum 4:40
“Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote
akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate,” Mt
16:24
“Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu
atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona,” Mt 16:25
“Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata
hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26
TAFAKARI: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike
msalaba wake, anifuate.”
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna aliye kati yetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. Ni kwa
ukweli huu kwamba hakuna kati yetu na aliye hai leo katika ulimwengu huu, yupo
kwa bahati mbaya. Kila mmoja wetu na kwa namna alivyo kadiri ya wito wake ni
kusudi la Mungu. Mungu ana mpango wa pekee na maisha yako hapa duniani. Hivyo
kuishi katika mpango huu wa Mungu yatupasa kufuata matakwa ya Mungu. Jambo hili
si rahisi sana kulipokea na kulikubali kwa sababu kadiri ya ufahamu wetu
kibinadamu, itatupasa kwenda kinyume na matakwa yetu na ufahamu wetu wa mambo
na vitu.
Ni kwa namna hii tunaona kwamba baada ya wana
wa Israeli kukombolewa kutoka utumwana Misri inawapasa kuishi kadiri ya mpango
wa Mungu ili wapate kufanikiwa, na siku zao ziwe nyingi katika inchi ile
aliyowapa wairithi. Kuishi mpango wa Mungu ni pamoja na kuzishika sheria zake. “Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo,
upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi
katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele,” Kum 4:40. Kuishi katika
ukweli huu yatupasa kuwa watii na waaminifu kila siku ya maisha yetu. Kwa
upande mwingine, mafanikio yetu katika maisha ni matokeo ya kuushinda ubinadamu
wetu kila siku kwa neema zake Mungu.
Katika
agano jipya la Mungu na watu wake, chini ya mwanaye mpenzi Yesu Kristo, ili
kuurithi uzima huu wa milele, kila mmoja wetu yampasa kuishi njia hii ya uzima
wa kweli kama Mwanaye Yesu Kristo anavyotuwasa katika injili ya leo: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe,
ajitwike msalaba wake, anifuate,” Mt 16:24. Tunamfuata Yesu kwa sababu ‘Yeye
ndiye njia, kweli na uzima,’ Yoh 14:6. Katika ufuasi wetu kwa Kristo, haya
mambo matatu ni muhumu sana: KUJIKANA NAFSI, KUJITWIKA MSALABA, NA KUMFUATA
YESU. Kujikana nafsi ni tendo la kujisalimisha na kuwa tayari kufanya kadiri ya
mapenzi yake Mungu, na siyo tutakavyo sisi au tuonavyo. Ni tendo la kusalimisha
utashi wako kwa Mungu, na kuwa tayari kutumika kadiri ya mpango wa Mungu.
Unafanya tendo hili na kuwa sehemu ya maisha yako kwa kuyachuchumilia yale ya
umilele ukilinganisha na haya ya leo na sasa tu. Ni kuishi ulimwenguni pasipo
kubebwa na malimwengu.
Kujitwika msalaba ni kukubali kuwa hapana utukufu pasipo msalaba.
Maisha tunayoyaishi kila mmoja kadiri ya wito wake, si maisha rahisi. Kuna
wakati katika maisha hayo itakupasa kutoa sadaka kubwa ili kuufia umilele ule
aliotuandalia Mungu. Hivyo kujitwika msalaba ni kupokea mateso pasipo shaka
yoyote na bila manung’uniko. Mambo hayo yanaweza kuwa magonjwa, ulemavu,
mahangaiko katika maagano yetu, mfano: ndoa, maisha ya wakfu, aka. Ni kuona
utukufu wa Mungu katika mateso na mahangaiko yetu ya kila siku tunapokabiliana
nayo. Msalaba huo katika maisha utusukume kuubeba kila siku na kusafiri nao
hadi golgota alipowambwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kuyapokea mateso yote na
kuyabeba mpaka mwisho bila kumwasi Mungu na mwanaye Yesu Kristo. Tukifanya hivi
pasipo shaka yoyote ndipo tutakapo hesabiwa haki na kuushinda mateso hayo.
Mateso hubadilika kuwa ushindi, na msalaba huwa kielelezo cha ushindi huo. Hapa
ndipo tunapoweza kuiokoa nafsi yetu katika majaribu. “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu
atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona,” Mt 16:25. Je, upo tayari
kuipoteza nafsi yako katika umilele wote?
Kumfuata Yesu ni mwito na matokeo ya kujikana nafsi, na
kujitwika msalaba pasipo shaka. Kumfuata Yesu ni kusafiri naye pasipo shaka
tukijua na kuamini kabisa kuwa ni yeye tu njia ya umelele, ukweli wa umilele,
na uzima wa umilele. Ni kufahamu pasipo shaka na kuamini maneno haya aliyosema
Yesu: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni
nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo;
nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30.
Hivyo kitulizo cha mahangaiko na mateso yetu ni YESU TU. Tunapojikana nafsi na
kujitwika msalaba wetu bila kufuatana na Yesu alioshinda mateso na maumivu ya
msalaba ni bure na kupoteza muda. Katika mahangaiko yote tuyapitiayo kamwe
tusimwache Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU NI KWAKO TU TUNAPOPATA FURAHA YA KWELI. TUJALIE
FURAHA HIYO DAIMA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario