sábado, 18 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 15 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 15 YA MWAKA-B
18/7/2015
Somo: Kut 12:37-42
Zab: 135:1, 10-15, 23-24
Injili: 12:14-21
Nukuu:
Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini,” Kut 12:40

Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda,” Mt 12:20

Na jina lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21

TAFAKARI: “Huyu ndiye Yesu.”

Wapendwa wana wa Mungu, haikua rahisi sana kwa wana wa Israeli kuupokea ujumbe ule waliopewa na Mungu kupitia mtumishi wake Musa, ya kwamba iliwapasa kutoka nchini Misri kwenye masufuria ya nyama na matango, na kwenda wasipopajua. Wana wa Israeli walikaa utumwani nchini Misri kwa muda wa kutosha. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini,” Kut 12:40. Kwa mtazamo huu, hata wale waliokuwepo katika mkakati wa kuondoka nchini Misri kuelekea nchi ya ahadi, hawakuona sababu ya kufanya hivyo, kwani walishaanza kuzoea mfumo wa maisha yale ya kitumwa. Hali hii ilimpatia Musa misukosuko mingi juu ya utayari wa wana wa Israeli. Lawama na manung’uniko yalikuwa mengi hasa pale walipopata taabu na dhiki nyingi nyikani.

Ni vigumu sana kuukataa mfumo wa maisha ambao kwayo tumeishi muda mrefu hata kama hauna tija. Wengi wetu huogopa sana kile tusichokijua kwa yale tuyatarajiayo. Ni ndani na katika Kristo tunapata uhakika wa kile tusichokijua na tusichokuwa nacho katika uhasilia wake licha ya shida na dhiki tuzipatazo kadiri ya wito wa kila mmoja wetu. Mungu anasema juu ya Yesu, yaani, uwezo na mamlaka aliyonayo, kwamba, Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda,” Mt 12:20. Huyu ndiye Yesu!

Wapendwa wana wa Mungu, ni kupitia jina lake Yesu Kristo twaponywa na twalitumainia milele yote. Ukweli huu si kwa sisi tu tafuasi wake, yaani wabatizwa, wakristo, bali kwa mataifa yote.Na jina lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21. Kwa hiyo ndugu yangu, popote pale ulipo mfanye Yesu kuwa sababu ya ukweli ndani yako, njia ya maisha yako, na uhai wako.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU KUWA SABABU YA HIKI NILICHO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario