martes, 7 de julio de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 14 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 14 YA MWAKA-B
Somo: Mwa 32:22-32
Zab:16
Injili: t 9:32-38
Nukuu:
“Akamwambia, jina lako hutaitwa tena Yokobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda,” Mwa 32:28

“Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka,” Mwa 32:30

“Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache,” Mt 9:37

“Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake,F” Mt 9:38

TAFAKARI: “Kuwa mara zote kile ulicho.”

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya mapungufu yetu kama wanadamu, tunaalikwa kila siku ya maisha yetu kuwa kile tulicho. Huwezi kusonga mbele kwa maendeleo yoyote bila kujua kiundani kile ulicho. Siri ya mafanikio ya kila mmoja wetu ipo ndani yetu. Mungu analithibitisha jambo hilo kwa Yakobo kwa kupata kibali mbele ya Mungu, “Akamwambia, jina lako hutaitwa tena Yokobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda,” Mwa 32:28. Kushinda na kupata kibali mbele ya Mungu ni kukubaliwa na Mungu. Tunapokubaliwa na Mungu ni kwamba tupo sehemu salama ya maisha yetu. Je, jambo hilo tunaliwekaje mbele ya macho ya Mungu?

Yakobo kama mwenye kupata mastahili mbele ya Mungu, yupo tayari kufanya lolote kwa upendeleo huo. Yakobo kwa unyenyekevu yote anapaita mahali pale, “Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka,” Mwa 32:30. Kuokoka katika maisha ni kutambua kasoro ulizokuwa nazo huko nyuma na kuwa tayari kuanza na kuendelea na Kristo mwenye siri yote ya maisha ya sasa na yajayo.

Wapendwa, kila siku tunaitwa kutenda na kuishi yale yanayompendeza Mungu. Tatizo kubwa katika ukweli huu ni kwamba hatupo tayari kuyafanya hayo. Wazo lolote lenye kutuhitaji kufanya kile kilicho cha pekee katika maisha yetu kinaitaji kujitoa kusipo na kipimo. Pamoja na ukweli kwamba waitwayo ni wengi, ila wanaokubali wito huu ni wachache. Ni wachache katika maana ya kwamba nguvu na akili zetu tuziwekazo katika utume huu hazima majibu ya haraka na mepesi. Ndipo  Yesu alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache,” Mt 9:37. Sote tumeitwa kuwa watendaji wa kazi ya Mungu bia kujibakiza. Hatuwezi kuona makusudia ya Mungu juu ya maisha yetu yanapotea bure.

Hivyo kila siku tunaalikwa kujitoa kwa ajili ya wito Mtakatifu. Kujitoa huku ni kuwa na dhamira chanya ya kuiombea miito mitakatifu. Tusipolifanya jambo hili kwa ukweli na umakini wake, yote hupotea kama moshi. “Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake,F” Mt 9:38. Kama wewe ni Padre unayefanya utume wako katika parokia, ni vyema ukayatazama kwa ukaribu makundi haya: Kuwa na wakati ujayo mwema, unapaswa kuwa karibu sana na vijana. Kuyapata mang’amuzi ya wakati uliopita yakupasa kuwa karibu sana na wazee. Kujua mahangaiko ya familia ya kila siku, wewe kama mchungaji na padre yakupasa kuwa karibu sana na wazazi. Kujua furaha ya kweli, wewe kama mchungaji mwema yakupasa kujua furaha ya kweli iliyopo kwa watoto.

Tumsifu Yesu Kristo!

EE YESU TAZAMA UKWELI NDANI YA MOYO WANGU, NIPO TAYARI KUJIREKEBISHA NA KUWA WAKO DAIMA. AMINA.


No hay comentarios:

Publicar un comentario