MTAKATIFU
TOMASO, MTUME
3/7/2015
Somo:
Efe 2:19-22
Zab:
116
Injili:
Yoh 20:24-29
Nukuu:
“Mmejengwa juu ya
msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,”
Efe 2:20
“Katika yeye ninyi
nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho,” Mt 2:22
“Basi wanafunzi wengine wakamwambia,
Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari,
na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika
ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo,” Yoh 20:25
“Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa
kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu,
wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye,” Yoh 20:27
“Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu
na Mungu wangu!” Yoh 20:28
“Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa
umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki,” Yoh 20:29
TAFAKARI:
“Majeraha ya Utukufu ya Yesu, Tomaso aponywa majeraha yake ya ndani.”
Wapendwa wana wa Mungu, kanuni ya Imani ile ndefu
tunakiri maneno haya na ndiyo msingi na mafundisho ya Kanisa: “Nasadiki kwa
Kanisa moja, Takatifu, Katoliki, la Mitume.” Leo kutokana na siku hii maalumu
ambapo Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Tomaso Mtume, ni vyema katika tafakari
yetu tukajikita kwenye hicho kipengele cha Mwisho, Mitume. Imani yetu ujengwa
na kuelekezwa kwa mafundisho yenye kubeba mamlaka zifuatazo: Mamkala ya
Kimungu, Mamlaka ya Kristo, Mamlaka ya Maandiko Matakatifu, Mamlaka ya Kanisa,
Mamlaka ya Mitume (mamkaka fundishi ya Kanisa/magisterium). Mamlaka zote hizo
chanzo chake ni Mamlaka ya Kimungu/Divine Authority. Tunapomtazama leo Tomaso
tunamtazama katika mamlaka ya Mitume, ambayo iliwekwa na Yesu Mwenyewe na
kuachwa katika uongozi wa Mitume, Petro akiwa ndiye kiongozi Mkuu.
Hivyo Kanisa letu, tena
Katoliki limejengwa katika mamlaka hiyo ya Mitume. Mtume Paulo anatukumbusha
jambo hilo kwa kusema, “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo
Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20. Nasi leo katika Kristo Yesu,
kwa sakramenti ya ubatizo , tumejengwa katika msingi huo wa mitume na kuwa
maskani ya Mungu katika Roho. “Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya
Mungu katika Roho,” Mt 2:22. Hivyo hatupaswa kuwa na shaka yo yote juu ya
msingi huu wa Kanisa, na chini ya Mitume wake. Mtume Tomaso anajulikana sana
kama Tomaso mwenye shaka. Tomaso mwenye shaka hakuamini ufufuko wa Yesu, hivyo
anabakia na majeraha yake ya kutokupenda. Tomaso anaitaji uponyaji. Kujua hatua
za uponyaji huu wa Tomaso yatupasa kuanza nyuma kidogo kuanzia ule mstari ya
19b, yaani Yoh 29:19b.
Jambo
hili la kutokupenda kutokana na majeraha na kuumizwa kwetu, linaonekana wazi
katika Injili ya leo ambapo tunaona watu wawili (Yesu Kristo Mfufuka na Mtume
Tomaso) waliojeruhiwa, ambao mwisho wa siku mmoja wao (Yesu Kristo Mfufuka)
anamponya mjeruhiwa mwenzake (Tomaso).
Uponyaji wa kwanza anaoutoa Yesu Kristo
kwa wanafunzi wake ni kuiondoa hofu kwa salamu yake ya upendo, “Akaja Yesu,
akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Yoh 20:19b. Tendo hili la
kuwa na Amani ya kweli ndiyo mwanzo wa kuanza kupenda kuliko kwa kweli na
furaha ya kweli. Wanafunzi wa Yesu wanaonyesha furaha hii, na kuanza kupenda
tena, ingawa Mtume Tomaso hawakuwepo katika kundi. Naye Yesu baada ya salamu ya
upendo iliyojaa matumaini mapya, “akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi
wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana,” Yoh 20:20. Furaha hii inaendana
na maagizo ya kufanya anayoyatoa Kristo kwa wanafunzi wake. Naye Kristo akawavuvia,
akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi,
wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23.
Kristo hapendi furaha ya kweli aliyotupatia tubaki nayo wenyewe. Hivyo furaha
hii twapasa kuisambaza kwa wengine kila mmoja kadiri ya wito wake, vipaji
vyake, dhamana na nafasi yake katika jamii anayoishi. Ndugu yangu ukiona hapo
unapoishi hata mbwa wanakukimbia bila sababu, ujue wewe ni shiiiiida!
Tomaso aliporejea anakokujua mwenyewe kwa
kupoteza imani yake juu ya Kristo, anapoambiwa jambo hili la kuonekana kwa
Kristo, hakuamini hata kidogo. Naye kwa ufahamu wake anatoa vigezo vya kutambua
ukweli aliousikia kutoka kwa wenzake. Naye anatoa vigezo na masharti ambavyo
lazima vizingatiwe. “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia
kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu
wake, mimi sisadiki hata kidogo,” Yoh 20:25. Kwa masharti haya na vigezo hivi
tunaweza kuona ni kwa jinsi gani Tomaso alijeruhiwa na kusononeshwa kwa tukio
la kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo.
Wapendwa, baada ya siku nane, tunaona
tukio la kukutana kwa wajeruhiwa hawa wawili, yaani Yesu Kristo Mfufuka na
Mtume Tomaso. Mjeruhiwa wa kwanza ni Yesu Kristo. Yesu anamkuta Tomaso na
kumwonyesha majeraha yake, na kusema, “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono
yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali
aaminiye,” Yoh 20:27. Tendo hili la Yesu kumwonyesha Tomaso majeraha yake na
kuumizwa kwake kunatoa picha ya majivuno ya Yesu na wakati mwingine kama
kujigamba vile. Jambo hili lina ukweli wake kwa katika mtazamo huu wa majeraha
na makovu aliyokuwa nayo Yesu. Majereha ya Kristo na
maumivu yake hayakuwa majeraha ya kushindwa, bali majeraha ya UPENDO WA KWELI.
Majeraha ya Kristo yalikuwa majeraha ya USHINDI uliotukuka. Hayakuwa majeraha
ya kuuma, bali majeraha ya UTUKUFU. Ni majeraha ya UPENDO. Upendo ambao upo
tayari kujitoa sadaka bila kipimo na kutojibakiza. Kristo anaonyesha ubavu wake
na mikono yake ilivyotobolewa si kwa kujionyesha au kuhukumu, bali kuonyesha
uzito na undani wa upendo wake kwa Mitume na kwetu sote.
Japokuwa
Tomaso hakuwa na majereha kwenye ngozi yake, na hakuwa na kuvuja damu kutoka
mwilini mwake, majeraha yake yalikuwa ndani ya moyo wake. Haya ni maumivu ya
ndani. Moyo wake ulijeruhiwa kwa kusitikishwa na kifo cha Bwana wake.
Alijisikia kudanganywa na Bwana wake Yesu Kristo. Alijisikia kushindwa baada ya
kuyaweka matumaini yote kwa Kristo kwa sababu alifikiri Yesu Kristo ni Masiha,
Mfalme, na kuhoji kwa nini Yesu afe kifo katili kama kile cha msalaba.
Alifikiri Yesu Kristo angeikomboa Israeli kutoka kwenye dola ya Kirumi.
Anajiuliza hivi, kwa nini hata yeye mwenye-Yesu ameshindwa kujinasua kutoka
watesi wake? Mtume Tomasi alisikitishwa na kusijikia kusalitiwa na Yesu. Tomaso
alishawishika kabisa kwamba alifanya uchaguzi usio sahihi kumfuata mseremala wa
Galilaya. Kwa kweli Tomaso alikuwa na maumivu makubwa sana.
Wapendwa wana
wa Mungu, maumivu na majeraha ya Moyo huchukua muda mrefu kupona. Majeraha haya
na maumivu ya Moyo yanachukua kuda mrefu kupona kwa sababu twaweza kuyaficha na
kujifanya hayapo. Twaweza kuongea na kutenda mambo yetu kama vile hakuna jambo
lolote baya au upungufu wowote wetu. Wengi wetu twaweza kukaa katika hali hii
kwa miaka mingi kwa kujivisha taswira nyingine na mwonekano mwingine ambao sio
uhalisia wa kile kilicho ndani mwetu ingawa tunaendelea na mateso na maumivu
hayo. Lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kudumu katika hali hii kwa muda wote na
nyakati zote. Mara tutaanza kujisikia vibaya na kujisikitikia na kufikiri marafiki
zetu wametutenga na wapo mbali bila kutusikiliza maumivu yetu yanayotusonga
moyoni. Mara tunajisikia kwamba hawajali na wanaubaridi kuhusu maumivu yetu, na
hivyo kuwachukia pia.
Hivyo,
katika kukutana kwa wawili hawa, mmoja wao yaani Yesu Kristo ana majeraha ya
UTUKUFU, na mwingine yaani Tomaso ana majereha ya maumivu ya ndani. Yesu Kristo
alikuwa tayari kujiponya kwa nguvu ya majeraha yake. Tomaso alihitaji kuponywa
majeraha yake lakini hapakuwa na mtu wa kumponya. Hapa ndipo wanapokutana
wajeruhiwa hawa wawili. Mjeruhiwa wa kwanza anamponya wa pili. Uponyaji huu
unajionyesha kwa maneno ya Tomaso mwenyewe anapomjibu Kristo baada ya Kristo
kumtaka kuvitia vidole vyake kwenye makovu na majeraha yake, akisema, “Bwana
wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28. Mwisho wa
kukutana huku, kila mmoja anapata majeraha ya UTUKUFU, na kuwa tayari kuponya
wengine wenye maumivu.
Wapo maelfu ya watu
wameumizwa na kujeruhiwa miongoni mwetu. Wengine wanabeba chuki kwa usiri
mkubwa ndani ya mioyo yao kwa kusalitiwa
kulikotokana na kutokuwa na uaminifu kwa wenzi wake wa ndoa. Wengine
wanabeba chuki dhidi ya wanaofisi wenzao kwa kuwaenezea umbea na uongo mitaani.
Wengine pia wanabeba ndani ya mioyo yao chuki na manung’unika kwa milongo ya
miaka iliyopita kwa kukosa sehemu ya kuponyeshwa na kusikilizwa. Wengine
maumivu haya wanayabeba tangu kuzaliwa kwao hadi sasa kutokana na namna ya
kutungwa mimba kwao kuliko kataliwa na kwa bahati mbaya au nzuri akazaliwa.
Wengine wamesalitiwa na wapenzi wao na kuyabeba hayo hadi sasa hata kama wanaishi
yao ya ndoa. Wapo wengi sana waliojeruhiwa na kuumizwa vibaya kwa namna tofauti
tofauti. Jambo hili linaweza kutokea kwa yeyote yule, iwe mlei, mtawa na hata
mtawa na mkleri.
Ndugu yangu, hata kama
tutayaficha majereha na maumivu yetu, kwa binadamu itafika wakati lazima
atayaonyesha tu wazi kwa kutafuta uponyaji. Ni njia mojawapo ya kurudisha
mizania ya ndani katika uumbaji wetu. Ukweli ni kwamba walioumizwa kweli na
kupata majeraha ya ndani hawawezi kuficha na kuvaa kinyago hicho kwa muda
mrefu. Wanaweza kuwadanganya wanaowazunguka kwa wakati tu, ila hawawezi
kujidanganya wenyewe na kuficha ukweli huu. Maumivu ya ndani ni vigumu sana
kuyavumilia.
Watu hawa wanaitaji
uponyaji. Wangepewa nafasi na uchaguzi wote wangependa kugusa majeraha ya
Kristo. Wanapenda kujua kwa uhakika kama kuna mtu anayewapenda vya kutosha kwa
kujeruhiwa kwao na mtu huyo yupo tayari kufa kwa kuwapenda. Tatizo kubwa ni
kwamba hawawezi kumwona tena Kristo. Wanaweza tu kuwaona watu wanaojiita
Wakristo. Wakristo ambao wanajulikana kwa kujinadi kulibeba jina la Kristo na
siyo kumuishi Kristo. Swali ni hili: Je wakristo hawa wapo kweli kama Kristo?
Je, wakristo leo wameumizwa vya kutosha kwa UPENDO kiasi kwamba wanaweza
kuwaponya walioumizwa? Je, ni kweli wakristo leo wamefufuka kutoka kifo cha
kujijali wenyewe, na ubinafsi, kwamba wanaweza kuwa matumaini na kielelezo cha
kuwarudisha waliopotea kwenye kundi kwa kuumizwa kwao?
Ndugu yangu, kuurithi
ufalme wa Mungu, ni kuishi vyema wito wako na vipaji alivyo kupa Mungu. Vipaji
hivyo siyo mali yako bali viwafaidie wengine, na hasa katika kuyaponyesha
majeraha na maumivu waliyokuwa nayo. Hiki ndicho kielelezo cha maisha yetu kama
Wakriso na wafuasi wa Kristo Mfufuka. Jambo hili si katika kuangamizana, bali
katika ufaidiana na kuongozana katika umilele ambao ndiyo makusudi ya Ufalme wa
Mungu.
Wapendwa ulimwengu wa leo
unamwitaji sana Kristo. Kama ulimwengu usipomwona Kristo kwa Wakristo wa leo,
waliojerehiwa watajitoa kwa Mungu, na kubeba mioyo yao inayovuja damu na
vidondo visivyoponyeka kwingine kusipo Mungu. Na wanavyojitoa huku ufikia
mahali na kuinamisha vichwa vyao na kufikiri katika akili zao: “Mungu amekufa!”
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU, KWA MAJERAHA YA
UTUKUFU WAKO NASI TWAPONA MAJEREHA YA MAUMIVU YETU YA NDANI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario