JUMATATU
WIKI YA 14 YA MWAKA-B
13/7/2015
Somo:
Kut 1:8-14, 22
Zab:
123:1-8
Injili:
Mt 10:34-11:1
Nukuu:
“Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto
mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi
hai,” Kut 1:22
“Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja
kuleta amani, bali upanga,” Mt 10:34
“Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala
apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili,” Mt 10:37
“Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza;
naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona,” Mt 10:38-39
“Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya
nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya
mwenye haki,” Mt 10:41
TAFAKARI:
“Yatupasa kujipambanua juu ya ufuasi wetu na Yesu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
mpango wa Mungu haufitiniki kwa hila za mwanadamu. Katika somo la kwanza
tunaona ongezeko la Waisraeli utumwani
Misri linakuwa tishio kwa utawala wa Misri. Hofu hii inapelekea mauaji
ya kimfumo kwa Waisraeli. “Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume
atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai,” Kut
1:22. Pamoja na mauaji hayo ya kimfumo, mpango wa Mungu kwa watu wake hakuna
binadamu awezaye kuubadilisha. Mateso yatakuwepo kwa wakati tu, na kupitia
mateso hayo tunaimarishwa na kufanywa imara katika Imani ile tunayoiishi na
kuishuhudia.
Kuiishi
Imani ni changamoto kubwa sana. Yesu anaiona changamoto hii na anatupa
angalisho. “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja
kuleta amani, bali upanga,” Mt 10:34. Kuiishi Imani yetu ni kufanya vita dhidi
ya utawala wa giza. Mapambano haya lazima yazue sintofahamu nyingi; kifamilia,
kiukoo, na hata kijamii. Hivyo, “Apendaye baba au mama kuliko mimi,
hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili,” Mt 10:37.
Ufuasi wetu katika Kristo, ni ufuasi wa kujikana nafsi kila siku. Mahangaiko
yetu ya kila siku yasiwe ukuta wa kuiishi imani yetu. Ni katika mateso pia
tunakutana na Kristo kwani kwa njia hiyo ya mateso Kristo kaushinda msalaba kwa
kujipatia utukufu. “Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza;
naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona,” Mt 10:38-39. Hakuna
utukufu pasipo msalaba.
Wapendwa wana wa Mungu, tuishi na kila mmoja wetu kwa upendo
na amani. Tupokeane na kutabikiana kwa upendo. Tupokeane kwa upendo katika
kweli. “Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata
thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata
thawabu ya mwenye haki,” Mt 10:41. Tuyaone mazuri kwa wenzetu, na mazuri hayo
yawe kielelezo cha kuuona uzuri wa Mungu kwa yule aliyeumbwa na sura na mfano
wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUPE UJASIRI WA KUTOSHA TUNAPOKUSHUHUDIA KILA SIKU
KWA MAISHA YETU.
No hay comentarios:
Publicar un comentario