JUMAPILI YA 16 YA MWAKA-B
19/7/2015
Somo I: Yer 23:1-6
Zab: 22:1-6
Somo II: Efe 2:13-18
Injili: Mk 6:30-34
Nukuu:
“Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya
wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala
hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema
Bwana,” Yer 23:2
“Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala
hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema
Bwana,” Yer 23:4
“Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama,
na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 23:6
“Naye akiisha kuuondoa
ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili
afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani,” Efe 2:15
“Akawapatanisha wote
wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule
uadui kwa huo msalaba,” Efe 2:16
“Kwa maana kwa yeye
sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja,” Efe 2:18
“Akawaambia, Njoni
ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa
sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,”
Mk 6:31
TAFAKARI:
“Makusudi ya Mungu: “asipotee hata mmoja wa wale aliowaumba kwa sura na mfano
wake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
maisha yetu leo hapa duniani ni kulisadifu lile alilolianzisha Mungu na kulikusudia.
Kwa maana hiyo, “Makusudi ya Mungu: “asipotee hata mmoja wa wale aliowaumba kwa
sura na mfano wake.” Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa
kwamba maisha unayoishi kadiri ya wito wako, wewe ni kielelezo cha kusudio la
Mungu katika uumbaji wake. Hapo ulipo, uwe mkleri, mtawa au mlei, uliokabidhiwa
asipotee hata mmoja. Ni kosa kubwa sana kufanya hujuma kwa wale ambao Mungu
ametukabidhi. Hivyo Mungu kwa kupitia Nabii Yeremia anasema, “juu ya wachungaji wanaowalisha watu
wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama;
angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana,” Yer 23:2. Mpendwa
katika Kristo, kama wewe ni kiongozi kwa ngazi yoyote ile, elewa kwamba wewe ni
jalala la kila kitu. Hivyo yote uyapokeayo na kuambiwa na watu yachunguze kwa
makini sana, na utoapo neno la mwisho lilenge katika kuwapata wale waliochini
yako na siyo kuwapoteza.
Ndugu yangu, huyu tunayemwabudu na kumtumikia ni Mungu mwenye
haki. Mungu wetu si Mungu wa visasi, bali ni Mungu anayetutaka tuishi katika
haki na upendo. Na Mungu anasema hivi; “Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli
atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 23:6.
Yatupasa kuwa watu wa haki hata kama kwa kutenda haki tunaumizwa.
Wapendwa, Mungu wetu anatutakia mema siku zote, na hivyo kwa
njia ya msalaba kupitia mwana wake mpezi, licha ya kwamba ni kifo cha aibu
kutokea katika historia ya mwanadamu, anaonyesha upendo wake mkuu usio na
kipimo kwetu. “Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya
amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya
nafsi yake; akafanya amani,” Efe 2:15.
Amani hii tuipatayo ni tunda la kifo cha msalaba wa bwana wetu Yesu Kristo,
Ndugu yangu, maisha yako kama mfuasi wa Kristo hayawezi kutenganishwa na
msalaba wa Bwana wetu Yesu. Ni katika msalaba tunapata utukufu. Hivyo, “Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia
ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba,” Efe 2:16. Hakika Mungu anatupenda upeo!
Ndugu yangu, tunapoutambua
ukweli huu, tujue kabisa tupo karibu na Roho wake Mtakatifu ambaye kwa kupita
yeye tunapata maondoleo ya dhambi zetu, na kutufunulia yale yaliiojificha
katika umilele wa Mungu. “Kwa maana kwa yeye sisi
sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja,” Efe 2:18. Je, ni nani
atakayetutenganisha na upende wake Kristo? “Upendo haupungui neno
wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma;
yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu
kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini
ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika,” 1Kor 13:8-10. Upendo wa
Mungu kati yetu hutufanya kile tulicho katika kweli na kile Mungu alichokusudia
katika maisha yetu.
Ndugu
yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, Mungu anatutakia mema kila dakika.
Na katika jambo hili ni vyema kuwa na muda wa kutosha katika kuyatafakari mambo
makuu ya Mungu anayotutendea kila siku ya maisha yetu. Jiwekee utaratibu wa
kuyatafakari makuu haya ya Mungu, hata mara moja kwa mwaka. Mfano wewe na
mwenzi wako wa ndoa, wewe kama mkleri, na hata mtawa, nje ya utaratibu wa
kawaida uwe na muda binafsi wa kuyatafakari hayo. Ikiwezekana hata kwa wiki
moja ukiwa katika sehemu tulivu na ya
sala. Hivi ndiyo Bwana wetu Yesu Kristo awatakavyo wanafunzi wake wafanye. “Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa
na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda,
hata haikuwapo nafasi ya kula,” Mk 6:31. Mara
nyingi tumekuwa kama bomba lenye kumwaga maji na kujisahau lenyewe na kuleta
ukavu pale liliposimikwa.
Ndugu yangu, naomba nikupe
mfano huu: kuna aina nne za watu. Lakini leo nitasema aina moja ya watu
inayoendana na injili na masomo yetu ya leo. Miongoni mwetu, wapo watu ambao
wapo tayari kufanya jambo lolote la huruma kwa yeyote wanayemsikia bila
kujibakiza.
Mtu wa mtindo huu
namfananisha na bomba yetu ya kawaida ambayo ukitaka maji yakupasa kuifungua na
kutoa maji kadiri ya kiwango utakacho. Bombo hilii la maji ni lile tuitumiayao
mabafuni mwetu. Hutoa maji yake kwa mpango mzuri sana. Kitu cha kushangaza ni
kwamba pamoja na umakini wake, juu ya bomba hii huwa pakavu sana. Hata kama
tupo mstari wa mbele kwa kuwahudumia watu kadiri ya upendo na ukarimu wetu,
yatupasa kujikumbuka wenyewe. Hatupaswi kujisahau nafsi zetu. “Ukarimu huanzia
nyumbani.” Iweje nimwone Yesu kwa wengine na kumsahau Yesu kwa wale ninaoishi
nao kila siku? Hivyo, pamoja na huduma tuzitoazo kwa watu wengine zisizokuwa na
shaka yoyote, hatupaswi kujisahau wenyewe.
Tumsifu Yesu Kristo!
MUNGU ANAKUPENDA UPEO, NA
KWA SABABU HIYO HAPENDI UPOTEE. AMINA.