viernes, 29 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-B
30/5/2015
Somo: Ybs 51:17-27
Zab: 18:8,9,10,11
Injili: Mk 11:27-33
Nukuu:
“Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyumba yangu ya mafundisho.” Ybs 51:23
Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha,” Ybs 51:17
wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?” Mk 11:28
Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mk 11:30a  
TAFAKARI: “Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyuma yangu ya mafundisho.” Ybs 51:23
Wapendwa wana wa Mungu, umasikini mkubwa kwa binadamu wa nyakati zote ni kule kutokujua kwake.  Kwa maana hiyo, ujinga wa mtu ni mateso yake, na ndiyo umasikini wake. Mjinga ni yule asiyefahamu. Mtu huyu ili kuondokana na karaha hii ya kutokufahamu, yampasa kujifunza. Hata hivyo hakuna binadamu yeyote katika ulimwengu huu anayejua kila kitu. Kwa mizania halisi, hakuna binadamu mwenye kujua moja ya kumi ya kila kitu hapa duniani. Kwa maana hii, kila mmoja wetu ni mjinga wa kitu fulani na kiasi fulani. Je, tufanye nini ili tuishi kwa amani na ufahamu wa kutosha?
Wapendwa wana wa Mungu, jambo la kwanza na la msingi kabisa ni kuyajua mazingira yako. Mazingira kwa maana halisi ya ufahamu, ni kuanzia hapo ulipo na hayo yanayokuzunguka. Je, unaufahamu wa kutosha kuhusu hapo ulipo na mazingira yanayokuzunguka. Usipolijua jambo hili, basi huo ndio umasikini wako mkubwa. Hali hii haijalishi rasilimali na fursa ulizokuwa nazo, wala utajiri uliokuwa nao, iwe ni wako au wakurithi. Waswahili katika hili wanasema, “mali bila daftari, huisha bila habari.” Basi kama ni utajiri wa kurithi utatoweka mara. Ni mara ngapi tunasimuliwa kwamba “familia hii wakati fulani walikuwa matajiri sana, leo ni masikini wa kutupwa.”
Ni katika mtazamo na mwono huu kibinadamu, kijamii, na kimazingira, nawaalika tutafakari neno hili; “Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyumba ya mafundisho.” Ybs 51:23. Baada ya kuona maana ya wajinga, sasa tuitazame nyumba ya mafundisho. Elimu aisemayo Mungu kupitia kwa mtumishi wake Yoshua Bin Sira, siyo elimu ya darasani katika tusomavyo leo. Nyumba ya mafundisho ni vile vyote vinavyokuzunguka wewe. Hali ya hewa na mazingira unayoyaishi ni nyumba ya mafundisho. Hali hii ya hewa itakufanya ujenge nyumba ya mtindo upi, uvae nguo za mtindo upi, na hata ulime na kula vyakula vya mtindo upi. Kitu cha kushangaza hata kwa hili ambalo lipo chini ya uwezo wetu hatuwezi kulifanya. Matokeo yake tumebakia kudokolea macho mambo ya wengine na kuyaiga kama kasuku. Vizuri vyote leo ni vile vinavyotoka nje. Lakini hapa wachina wamethibitisha si kweli. Leo matibabu mazuri ni kutoka nje. Hata viongozi wetu wametusadikisha hivyo, kwani hata mafua tu wanaenda nje kutibiwa.
 Watu unaoishi nao ni nyumba ya mafundisho. Je, upo tayari kujifunza kutoka kwa wenzako? Ukweli ni kwamba “anayekimbia mwenyewe mara nyingi hufikiri kwamba yeye ni mkimbiaji bora kuliko wengine.” Yapo mambo mengi tunayojifunza kwa wenzetu na hata kujisahihisha pale tuliposhindwa kufanya vizuri. Maendeleo kwa ujumla wake ni tendo la kujifunza na ushindani. Ila kiroho, ushindani huu huwa tunauchukulia kwa maana hii; “uwe na wifu wa maendeleo.” Kama mwenzako kajenga nyumba na kaezeka bati, basi wewe fikiri juu zaidi. Jenga nyumba yako ezeka vigae. Ushindani huu hata kwa mambo ya kiroho pia twajifunza kwa wenzetu. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuwaheshimu watakatifu. Ila wapo pia kati yetu wanaoishi maisha ya utakatifu kiasi kwamba twataka kujua siri ya mafanikio yao na hofu hiyo ya Mungu walio kuwa nayo. Ila cha kushangaza, badala ya kujifunza mazuri kutoka kwa wenzetu kama changamoto ya sisi kukua kiroho, tunakuwa sababu ya kuwaangamiza kabisa hata wasionekane katika macho yetu. Neema na baraka Mungu azifanyazo kupitia wengine, hatuwezi kamwe kuzifuta machoni mwa Mungu kwa hila zetu za kibinadamu. Roho huyu Mtakatifu afanyaye kazi kupitia wenzetu na kuwatakasa, hatuwezi kumzuia kufanya kazi hiyo kwa kujenga kuza za: wivu, visasi, kukomoana, vipingamizi na hata chuki.
Wapendwa wana wa Mungu, hatuishi kujifunza maovu kutoka kwa wenzetu ili tumwelekee Mungu. Wapo watu wengi miongoni mwetu ni wezi, hasa wa mali za umma wamekuwa mfano wa kuoigwa na kupigiwa debe. Leo vijana wengi wanavutiwa na watu waovu, na wanapenda kuwa kama wao. Vijana wengi leo wanatumika kama njia na ngazi za watu waovu kufikia tamaa zao iwe kisiasa, kijamii, kiuchumi na hata kidini. Ndugu yangu kwa nini watumika vibaya? Hapa ndipo tunapozungumzia “UPUMBAVU.” Upumbavu wa mtu ni saratani ya mtu. Saratani hii umtafuna taratibu, na mwisho wa siku hujikuta hana namna nyingine ya kuishi zaidi ya dada MAUTI. Taifa letu na jamii yetu leo ya Watanzania tunatafunwa na saratani hii-“UPUMBAVU.” Je, mpumbavu ni mtu gani?
Wapendwa, mpumbavu ni yule anayejaribu kukusadikisha usalama wake mchana kweupe akiwa analikata tawi alilokali akiwa juu ya mti mrefu. Kwa maana nyingine, ni mtu anayejifanya anajua kumbe hajui kabisa. Ninapata shida sana, na hata nashindwa kuamini inakuwaje mtu na ufahamu wake kwamba imethibitishwa mtu mfulani amejikoka mabomu {wizi, rushwa, ufisadi, nk}, bado unaenda kumkumbatia na kutaka awe msimamizi wa nyumba yako na shamba lako? Hapa kweli kuna nyumba ya mafundisho? Jambo la kushangaza zaidi hata baadhi ya viongozi wa kidini hawaoni hatari hii baada ya kupata mgao huu wa wizi.
Ndugu yangu, nyumba ya mafundisho ni uwezo wa mtu kuzisoma alama za nyakati. Kuzisoma alama za nyakati ni kufanya tathimini ya namna ulivyoishi jana, unavyoishi leo, na kutokana na mang’amuzi hayo, upate dira ya kuishi kesho. Tulio wengi mtihani huu ni mgumu sana. Ona tunavyojikanganya! Jana ulilaumu hali fulani ya masiha, leo hali ile imejirudia, na kesho unayapigia debe maisha yale ambayo jana uliyalaumu, leo yanakutesa, na kesho unataka yaendelee. Ni kuku tu mwenye ujasiri wa kuishi maisha hayo. Ukitaka kujua ujasiri wa kuku mrushie nyanya utaona uwezo wake wa kufikiri. Kuku anapoiona nyanya huanza kuidonoa ikijiviringisha upande wa pili, kuku yule yule husahau kama ulishaitoboa upande mmoja, hivyo huanza tena kuitoboa upande mwingine. Mungu hajatuumba tuwe kama kuku. Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake. Kwa nini basi tunapenda kuwa kuku? Kwa nini tunamshushia Mungu hadhi yake?
Wapendwa wana wa Mungu, tunapoyakubali mazingira ya kikuku kuku tunapoteza nira na utukufu wa Mungu. Hatuwezi kusema maneno haya; “Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha,” Ybs 51:17. Tunapopoteza nira hii na utukufu huu wa Mungu ndani yetu, hatuwezi kamwe kupata yale tunayomwomba Mungu. Huku ni kuishi bila Mungu, na mateso yake ni kuishi jangwani hadi tutakapotambua tulipoipoteza nira na utukufu ule Mungu aliotupa kwa tendo la uumbaji wetu.
Katika njili ya leo Yesu Kristo anakutana na Wapumbavu wengine. Pamoja na mambo yote aliyoyafanya Yesu ikiwa ni pamoja na miujiza yake, na mafundisho yake yaliyojaa hekima na nguvu ya kimaadili, bado hawajui ni kwa mamlaka gani anayafanya mambo hayo. Wayahudi, na hasa nyakati za Yesu, walikwisha ichakachua Torati kiasi kwamba walichokuwa wanakiishi na kukifuata ilikuwa ni tafsiri ya Torati na masimulizi mbalimbali ya marabi-TALMUD. Hivyo kwa kuitupa Torati kapuni walikosa historia nzima wa wokovu wa mwanadamu, na kilele chake katika fumbo zima la Kristo mwana wa Mungu, akiwa ndiye ufunuo wa wazi kabisa wa Mungu. Hivyo wabishi na “wapumbavu hawa,” wanahoji mamlaka ya Yesu kwa kumwambia, “Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?” Mk 11:28. Yesu hakuwapa jibu la moja kwa moja kuhusu swali lao hili kwani mazingira yalisadifu kabisa kuelewa walicho uliza.
Yesu Kristo hana muda wa kujibizana na wapumbavu. Yesu Kristo anao muda wa kuwafundisha wajinga/wasiofahamu, ili wafahamu siri ya Mungu. Mastahili ya mpumbavu katika maana hii, ni laana na wala si baraka. Wayahudi waliposhindwa kujibu swali alilouliza Yesu, Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mk 11:30a, kwa kujua mtego wake kwamba, “tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi,” na kusema hatujui, naye Yesu hakutoa jibu kwani jibu walikuwa nalo. Huu ndiyo mtazamo wa mtu mpumbavu. Hujiaminisha kujua hata kama hajui.
Wapendwa wana wa Mungu, wenye ufahamu wa kweli, na hofu ya Mungu, tuliombee sana Taifa letu. Taifa letu sasa linaongowa na mihehuko ya wapumbavu ambao wengi sana. Ni sawa na kuwapa vichaa rungu. Je, hapo unategemea nini? Kwa nini jamii yetu leo inawashabikia wezi na mafisadi? Kwa nini wengi wetu leo wamekuwa wapumbavu? Hakika mwendelezo wa upumbavu huu ni mwitikio wa laana ya Mungu. Tusipojikwamua katika mtego huu wa upumbavu, tusishangae mateso makubwa huko tuendapo. Wayahudi walipotaka kuwa na Mfalme kama mataifa mengine ya jirani zao, Mungu aliwapa licha ya kwamba halikuwa chaguo lake. Wakamchagua Sauli. Mfalme Sauli aliwanyoosha vizuri wana wa Israeli hadi pale Mungu alipowachagulia Mfalme Daudi. Je, nasi ndiko tunapoelekea?

Tumsifu yesu Kristo!


EE YESU LITAZAME TAIFA LAKO NA WATU WAKO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario