lunes, 25 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-B
26/5/2015
Somo: Ybs 35:1-15
Zab: 49
Injili: Mk 10:28-31                                      
Nukuu:
“Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” Ybs 35: 7-9
“Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” Ybs 35:10
Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30
TAFAKARI: “Faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari neno hili; “faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu.” Kwa ulimwengu huu tunaoishi leo wenye mtazamo wa kupata tu FAIDA na kuishi katika hali ya USHINDANI, kwa haraka haraka huwezi ona faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Tupo kwenye ulimwengu usioguswa na hofu ya Mungu, na hivyo waliowengi siyo tu kwamba hawaamini uwepo wa Mungu, bali pia hawataki kusikia habari zake.
Ndugu yangu kuna faida kubwa sana kutumika vyema kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kuzipata na kuzifikia faida hizi kwa urahisi yakupasa kuzishika amri zake kisawasawa. Kuzishika amri hizi si kwa ajiali ya kuwakonga watu nyoyo zao, bali kuona ni sehemu ya umilele wako, na amri za Mungu kuzishika kwa ufahamu, kutakuongoza katika njia iliyo kweli.
Jambo la pili, ni kuweka amri hizo katika matendo. Na kwa namna ya pekee, Bwana wetu Yesu Kristo amezifupisha amri zote kwa kuziweka katika mihimili miwili, yaani Mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, akili zake zote, na nguvu zako zote. Na muhimili wa pili Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hivyo ukimpenda Mungu kwa kile chote ulicho utafanya haya kadiri ya somo letu la leo; “Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” Ybs 35: 7-9. Jambo hili litakupa wajibu wako mbele ya Mungu. Na utawajibika kumrudishia Mungu kilicho chake. Mara nyingi tunamrudishia Mungu mabaki ya kazi za mikono yetu. Elewa vitu vyote ni mali yake MUNGU.
Mhimuli wa pili wa amri za Mungu ni kumpenda jirani yako kama unavyojipenda wewe MWENYEWE. Hapa utatambua wajibu wako kwa jirani na hasa wahitaji. Utatambua ubinadamu wako na umuhimu wa binadamu mwingine, hasa wale wasiokuwa na fursa katika jamii kutokana na mambo mbalimbali. Hivyo, “Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” Ybs 35:10. Wajibu huu ni muhimu sana kuishi katika hofu ya Mungu. Masikini tunao wengi sana. Kabla ya kuanza kuwatafuta masikini mitaani, masikini hawa tunao kwenye familia zetu, jumuiya zetu za kitawa, jumiya zetu ndogondogo, vigangoni mwetu, na hata parokiani mwetu. Masikini katika hali ya uuitaji wapo wengi sana. Wengine wengependa tu wasikilizwe hiyo ndiyo kiu yao. Wengine wengependa wakusikie tu, hiyo ndiyo kiu yao. Na wengine wangeitaji ufahamu wako katika kuchambua mambo kwa haki na busara.
Wapendwa wana wa Mungu, katika kuyafanya mambo hayo kulingana na miimili hii miwili, hatupotezi chochote zaidi ya kufaidika kwa kutumika vyema. Hakuna anayepoteza muda wake kwa kufanya yale yanayohusu ufalme wa Mungu. Ni furaha kubwa sana mbele za Mungu akiona umewapeleka wengi kwake. Hivyo Yesu anatuambia tunapoyaacha yale ambayo yangetujengea umaarufu hapa dunia usiodumu, kwa namna hiyo hiyo tunajaliwa mengi katika ufalme weke. Hivyo, Yesu anakasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Je, bado unamashaka kwa utume unaoutoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu? Kwa nini hauna furaha katika utume wake? Kwa nini utume wako unawadumaza watu badala ya kuwakuza na kufurahia ufalme wa Mungu? Kwa nini unakuwa sababa ya watu kumchukia Mungu na kuasi njia zake?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE TUTUMIKE VYEMA KWA AJILI YA UFALME WAKO. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario