IJUMAA
YA WIKI YA 8 YA MWAKA-B
29/5/2015
Somo:
Ybs 44:1,9-12
Zab:
149: 1-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili:
Mk 11:11-26
Nukuu:
“Wema wao utawadumia
wazao wao, na urithi wao una wana wa wana. Wazao wao wanashikamana na agano, na
watoto wao kwa ajili yao,” Ybs 44:11-12
“Hata
asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa,” Mk 11:12
14 Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako,” Mk
11.14a
“Akafundisha,
akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa
yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Mk 11:17
“Yesu
akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu,” Mk 11:22
“Kwa
sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea,
nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24
“Lakini
kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa
yenu,” Mk 11:26
TAFAKARI:
“Mwaminini Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa kubatizwa kwetu na leo kuitwa Wakristo bila kuishi Imani hiyo hakusadifu
chochote. Hata hivyo, imani ya mtu si tu kwa kile anachokiamini kwa nadharia
fulani, bali ni kuwa na imani, na imani hiyo ijionyeshe katika maisha mazima
yako ya kila siku. Kwa maana hiyo, leo tutafakari neno hili; “mwaminini Mungu.”
Maneno haya anayatamka Yesu kwa wanafunzi wake baada ya Petro kumkumbusha
kukauka kwa ule mti aliyoulaani kwa kukosa kuzaa matunda kwa wakati wake.
Maneno haya ya Yesu
yanatufundisha kwamba, maisha yetu tunayoyaishi yanapoendana na Imani yetu,
neema na baraka zitakuwepo na Mungu atajidhihirisha mara zote kwa yale
tunayoyaamini. Hivyo tunapoamini kuliko kwa dhati, tutastajabia mengi katika
maisha. Mfumo wa maisha ulio kielelezo cha imani thabiti, ndiyo njia pekee ya
kurizishana kizazi hata kizazi. Pamoja na utajiri ambao tunaweza kuwaachia
watoto zetu na hata wale tunaoishi nao ni pamoja na Imani iliyo thabiti. Kwa
imani hii kizazi kitaendele kumcha Mungu na kuneemeka kwa baraka zake. Hivyo,
“Wema wao utawadumia wazao wao, na urithi wao una wana wa wana. Wazao wao
wanashikamana na agano, na watoto wao kwa ajili yao,” Ybs 44:11-12. Huu ndio
urithi utakao tuwezesha kuuona uso wa Mungu.
Wapendwa, Bwana wetu
Yesu Kristo kama Mungu na Mwanadamu; aliona njaa kama mwanadamu, hivyo ilimpasa
kula. Kama Mungu alijua ni sahihi kabisa kwa kipindi kila na majira yale ya
Mwaka, Mtini ule ulipaswa kuwa na matunda. Badala yake hakupata tunda hata
moja. Hivyo anaulaani mtini ule kwa kusema, “Tangu leo hata milele mtu asile
matunda kwako,” Mk 11.14a. Kulaaniwa kwa mtini huu kunatupa angalisho kwa
maisha yetu ya Kiroho. Je, tunatumia fursa tulizokuwa nazo vizuri kukua kiroho?
Wapendwa tendo hili la
kulaaniwa kwa mtini huu kwa kutokuzaa matunda wa wakati wake, kunanikumbusha
aina fulani ya mawe yajulikanayo kama “songoro,” kwa kichangga. Mawe haya hupatikana
mitoni na kwa uhasilia wake huteleza kutokana na kukaa kwenye maji kwa muda
mrefu. Kitu cha kushangaza kwa mawe haya pamoja na kukaa muda mrefu kwenye maji
kwa maisha yote ya mto huo, ulipasuapo jiwe hili ndani yake ni kavu sana.
Hakuna dalili ya unyevunyevu wa maji. Hii ndiyo laana ambayo tunapata kwa
kutotumia fursa tuliyonayo na mazingira tuliyonayo kukua kiroho.
Ni katika mtindo huo
huo miili yetu kama hekalu la Roho Mtakatifu, tunaona Yesu akiwatawanya
waliokuwa wanalinajisi Hekalu la Mungu kama sehemu ya kumsifu, kumwabudu na
kuomba wanapolifanya pango la wanyang’anyi kama sehemu ya biashara. “Je!
Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi
mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Mk 11:17. Hatuwezi kumsifu, kumwabudu
Mungu na kusali kwa utulivu kama hatuna utulivu ndani yetu. Kumbe kukaa na
kumsikiliza Mungu ni kuwa na utulivu ndani yetu. Na siyo tujitawanya kimawazo.
Zaidi ya hayo, tunasali
kwa sababu tunaimani kwa kile tunachokiomba. Kama tunasali kwa sababu ni
utaratibu wa familia, jumuiya na kikundi chetu cha sala, sala hiyo haina uhai.
Huku ni kupotea kiimani na muda pia. Ndani na katika Kristo tunasali kwa sababu
tunaamini tumekwisha pata kile tunachokiomba kwa sababu Kristo ni yote katika
yote. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote
myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24.
Tufanyapo tendo hili kiimani, yatupasa kuwa katika hali ya usafi kimwili na
kiroho. Yatupasa kujitakasa kabla ya kutakaswa na kutiwa nguvu na neema kwa
yale tuyaombayo. Hivyo hatuwezi kujongea mbele ya Mungu tukiwa na hatia.
Yatupasa kujipatanisha na nafsi zetu, wenzetu, na Mungu. “Lakini
kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa
yenu,” Mk 11:26.
Wengi wetu, twajipendekeza
kwa Mungu, kwa kutimiza ratiba yote kila siku tukisema tuna mpa Mungu haki yake
huku upande wa pili hatuishi vyema na ndugu zetu, na jirani zetu. Kusamehe kwa
Mkristo ni AMRI. “Utusamehe makosa yetu kama tunavyo wasamehe walio tukosea.” Maneno haya katika sala ya Baba yetu,
yatukumbushe wajibu wetu wa kusamehe.
Tumsifu Yesu Kristo!
NA TUSAMEHANE KILA
WAKATI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario