JUMAMOSI
WIKI YA 6 YA PASAKA-B
16/5/2015
Somo: Mdo 18:23-28
Zab: 46
Injili: Yoh 16:23-28
Nukuu:
“Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo,
mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika
maandiko,” Mdo 18:24
“Akaanza
kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia
wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi,” Mdo 18:26
“Kwa
maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa
maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28
Na siku ile mtaomba kwa
jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba
mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi
nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27
TAFAKARI:
“Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni siku nyingine tena na kwa neema ya Mungu twalitafakari neno lake la uzima.
Leo, kwa namna ya pekee tulitafakari neno hili, “Baba mwenyewe awapenda kwa
kuwa ninyi mmenipenda mimi.” Upendo wa Baba kwetu ni matokea ya upendo wetu kwa
mwanaye, Yesu Kristo. Kumpenda Kristo ni kushika na kuishi yake
aliyotufundisha. Hatuyafanyi hayo kwa ajili yetu binafsi, ila kwa ajili ya
wengine. Kristo kautoa uhai wake si kwa ajili yake binafsi, bali kwa ajili yetu
sote, na kutufanya huru kutoka kifungo cha dhambi. Kwa sadaka yake pale
msalabani sote tumerudishiwa urithi wetu na kuwa wana wa Mungu.
Tukiyafanya hayo na
kuishi msingi huu wa Imani, ni kielelezo tosha kwa kumpenda Mungu kwa kuishi
yale aliyotufundisha Kristo. Tendo hili litatupa uhalali wa kuomba na kupata
bila vizingiti vyovyote kwa sababu tumempenda Mwana, ambaye mwana na Baba ni
kitu kimoja. “Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi
nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na
kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27.
Apolo aliyekuwa Myahudi
kweli kweli, anaguswa na upendo huu wa Kristo, na anatoa ushuhuda kwa Wayahudi
wenzake ambao hawakumkubali Kristo. Huku ni kumpenda Kristo bila kuona haya
mbele za watu. Ni kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo. Hata hivyo hatutaweza
kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo kama hatumfahamu Kristo. Apolo anamfahamu
Kristo kwa kuyasoma maandiko Matakatifu na kuyaelewa. Huwezi ukatoa kile usichokuwa
nacho. Kwanza ni lazima ukielewe kitu hicho ndio uwe na mamlaka la kukisema.
Imani hukuzwa kwa hatua. Huwezi kukurupuka tu na kuanza kutoa ushuhuda,
isipokuwa kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu. “Basi
Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika
Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko,” Mdo 18:24. Mkristo inakupasa
kulisoma neno la Mungu. Jiwekee utaratibu angalau kila siku usome neno la
Mungu. Ukishalisoma jiulize swali hili moja tu: Je, neno hili linasema nini juu
ya Maisha yangu?
Kulinena neno na
kuliishi kwa ujasiri, hukuzwa pia na wenzetu walikwisha ijua njia hiyo. Apolo
anasaidiwa na Prisila na Akila. Lengo la ndugu hawa si kumdhoofisha Apolo, bali
kumtaka awe makini zaidi kuhusu neno la Mungu. Ni kumfanya awe hodari zaidi. Ni
kumwongezea maarifa ili afanye vizuri zaidi. Hapa tunajifunza pia unyenyekevu
wa Apolo kukosolewa na kuwa msikivu. Ni mara chache sana wale ambao wanajiona
wanajua na wakati mwingine kwa kuchukua vigezo vya kuwa na kundi kubwa nyuma
yao, kuwa tayari kusikiliza ushauri. Apolo ni tofauti kabisa. “Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata
Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa
usahihi zaidi,” Mdo 18:26. Mafanikio yetu katika maisha yasitutie upofu wa kujifunza
zaidi.
Utayari wa Apolo
kujifunza maarifa zaidi, unamwongezea ustadi wa kila alichokuwa anakijua awali.
Kwa sababu hiyo, “aliwashinda Wayahudi
kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu
ni Kristo,” Mdo 18:28. Ndugu yangu, tusichoke kujifunza mambo mapya na hasa
pale tunaposhauriwa kufanya hivyo na wenzetu kwa sifa na utukufu wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
Ee Bwana Yesu Kristo,
uwe njia na wokovu wangu, usiniache. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario