JUMATANO
WIKI YA 8 YA MWAKA-B
27/5/2015
Somo:
Ybs 36;1-2a, 5-6, 13-19
Zab:
78
Injili:
Mk 10:32-45
Nukuu:
Ee Bwana, uisikilize
sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako. Na wote wakaao duniani
watajua ya kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele,” Ybs 36:16-17
“Yesu
akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au
kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?” Mk 36:38
“Yesu akawaambia,
Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya
kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao
watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40
“Yesu
akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa
huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42
“Lakini
haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi
wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10:43-44
“Kwa
maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake
iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45
TAFAKARI:
“Hamjui mnaloliomba”
Wapendwa wana wa Mungu,
sala na maisha ya sala ni vitu viwili tofauti, ila hatuwezi kuvitenganisha
tunapozama katika mahusiano na Mungu yaliyo ya karibu na ya kweli. Kwa ufupi,
sala ni mwitikio wa ndani ya mtu ulio wa kweli na usio na shaka yoyote kwa
Mungu aliye yote katika yote. Mwitikio huu ni tokeo la kiufahamu unaoweka wazi
ubinadamu wetu na mipaka yake, na Umungu katika ukamilifu wake. Hivyo, mwitikio
huu hujidhihirisha katika namna mbalimbali kadiri ya mguso wa ndani wa mtu juu
ya mahusiano haya ya kipekee baina yake na Mungu. Mguso huu wa ndani
hujionyesha nje ya mtu kama: Maombi, kusifu, kushukuru, kuambudu/kujisalimisha
na ukimya wa kujizamisha ndani ya mafumbo na maajabu wa Mungu.
Hivyo basi, tukiwa na
uelewa huu tutafahamu kile/lile tunachokiomba, tunachokisifu, tunaloshukuru,
tunachokiabudu, na kule tunapozama katika mafumbo na maajabu ya Mungu. Leo
tuelekeze tafakari yetu katika maneno haya ya Yesu, “hamjui mnaloliomba.”
Maneno haya Yesu anayatamka kwa Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, ambao
walimwomba Yesu wakae mmoja mkono wake wa kushoto na mwingine mkono wake wa
kuli. Sala kama maombi, haitoshi tu kuweka mbele matamanio yetu binafsi, bali
maombi yetu yawezeshwe kadiri ya mapenzi ya Mungu aliye yote katika yote.
Yakobo na Yohana wanatanguliza matamanio yao na ubinafsi wao. Hawakuweza hata
kuwakumbuka Mitume wenzao waliobaki, yaani wale kumi. Haya ni maombi yasiyo na
ukomavu kiimani. Ni mara baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Yakobo anatambua maana ya maombi, na kusema, “Hata mwaomba, wala hampati kwa
sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu” Yak 4:3. Huyu sana ni
Yakobo Mtume aliyekomaa kiimani. Kwa sasa anajua kile aombacho.
Wapendwa wana wa Mungu,
Yesu ndiye anayetufundisha uhusiano wa maombi yetu na matakwa ya Mungu katika
sala yake kule Bustanini Getsemani. “Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako,
uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke,” Lk
22:41-42. Tuliombalo licha ya kwamba latupendeza na tunalihitaji, yatupasa
kujisalimisha kwake yeye aliye yote katika yote, naye atupe kadiri ya hitaji
letu na mapenzi yake. Huku ndiko Yesu alikomaanisha, “kunywea
kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi” Mk 36:38.
Hivyo
Mungu aliye Baba yetu Mwema na anayetujua sisi watoto wake atatupa
kadiri ya upendo wake. Hivyo, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona;
bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye
atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu,
ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je!
Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:7-11.
Hii ndiyo maana halisi ya kile tuombacho na matakwa ya Mungu kwa yale
tuyaombayo. Kuhesabiwa haki kwa yale tuyaombayo baada ya kupitia taratibu zote;
ni juu ya Mungu mwenyewe kutupa kadiri ya hitaji letu na mapenzi yake. Hivyo,
“Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao
mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si
langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40. Mungu pekee
ndiye anayetuhesabia haki.
Wapendwa, kwa kujua
ukweli wa jambo hili juu ya namna ya kuomba, twaweza kuyatamka maneno haya
kutoka kitabu cha Yoshua Bin Sira, “Ee Bwana, uisikilize sala yao wakuombao,
sawasawa na kibali chako kwa watu wako. Na wote wakaao duniani watajua ya
kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele,” Ybs 36:16-17. Bila kuyafahamu
mahusiano yetu na Mungu, na hali yetu ya ubinadamu, sala kama nilivyoelezea
hapo juu ubakia katika hali ya ukavu.
Udadisi wa Yohana na
Yakobo kutaka sehemu ya pekee kwa Yesu Kristo, kunazua mzozo miongoni mwa
Mitume kwa kauli yao hiyo. Ni kama leo tunaposikia baadhi ya Viongozi wakitangaza
nia zao za kutaka kugombea urahisi kabla ya wakati. Yesu analiona hili na
kulikemea moja kwa moja kabla halijawa tatizo. Kristo hapa anaonyesha ukomavu
katika uongozi na anawataka nao Mitume waige mfano huo. “Yesu
akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa
huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42. Kwa upande wa Mitume hawapaswi kufanya hivyo na
wala kuwa hivyo. Mitume wameshafunuliwa siri ya umilele, hivyo waishi katika
mwono huo wa umilele. Nasi pia kwa ubatizo wetu tumeshafunuliwa siri hiyo ya
umilele, na hivyo yatupasa kuishi kadiri ya mwelekeo huo wa umilele. Naye Yesu
anatuambia, “Lakini haitakuwa hivyo
kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka
kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10:43-44. Maisha ya Mkristo ni
kutumika vyema kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
kielelezo cha kutumika vyema ni Kristo
mwenyewe aliyekuwa mfano hai kwetu na bado ndiye mfano hali kati yetu hasa pale
tunapoona ndugu zetu katika jumuiya na familia wanavyojitoa bila kujibakiza na
kuwa mfano wa Kristo aliye hai. Katika ukweli huu Yesu anatukumbusha kupitia
maisha yake mwenyewe, akisema, “kwa maana
Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe
fidia ya wengi,” Mk 10:45. Basi, nitumike
vyema katika familia yangu kadiri ya nafasi yangu, nitumike vyema katika
jumuiya yangu ya kitawa kadiri ya nafasi yangu, na nitumike vyema katika jamii
ninayoishi kadiri ya nafasi yangu.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU TUFUNDISHE NAMNA YA KUOMBA.
AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario