sábado, 30 de mayo de 2015

TAFAKARI: SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
31/5/2015
Somo I: Kum 4:32-34, 39-40
Zab: 33:4-6, 9, 18-20, 22
Somo II: Rum 8:14-17
Injili: Mt 28:16-20
Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Nukuu:
Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine,” Kum 4:39
Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele,” Kum 4:40
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu,” Rum 8:14
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:16-17
Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,” Mt 28:18 
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu,” Mt 28:19
TAFAKARI: “Mungu kaufungua upendo wake wa ndani kwetu.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mama Kanisa dominika iliyopita amekamisha umaana wake katika Imani kwa kuvuviwa Kanisa Roho Mtakatifu. Dominika hii tunaielekeza katika tafakari nzito baada ya tukio la Pentekoste katika msingi na kina cha fumbo la Imani, ikiwa ndicho kielelezo sahihi na utambulisho wake popote duniani, kuitangaza Imani hiyo na kuifanya hai. Ni fumbo linalotutaka tuelewe kadiri ya uwezo wetu Mungu ni nani (rejera CCC 738).
Wapendwa, fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini na msingi wa  Imani ya Kikristo na maisha kwa ujumla wake. Ni fumbo la Mungu wenyewe (CCC 234)-ambaye ni mmoja katika nafsi tatu. Kupitia Kristo na Roho Mtakatifu tumekuja kujua kwamba kwa Mungu kuna nafsi tatu; katika umoja wa Kimungu, na utofauti kati ya nafsi hizi ndiyo hufanya uhusiano katika umoja huu Mtakatifu. Agizo la mwisho la Yesu kwa wanafunzi wake, Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,” Mt 28:19. Wanafunzi hawa wanafanywa kuwa hivyo, “mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Ni kwa tendo hili la ubatizo, mbatizwa anafanywa na kushirikishwa ukweli wa Imani hii katika uhasilia wake kwamba, “Mungu ni mmoja, Baba Mwenyezi, Mwanawe wa pekee Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu: UTATU MTAKATIFU” (CCC 233). Kanuni ya Imani katika Utatu Mtakatifu ndiyo inayotufanya sisi kuwa Wakristo. Kwa maana hii, vikundi vya kidini ambavyo hubeba na kumtukuza na kumuheshimu Kristo, na kufikiri wao wenyewe kuwa Wakristo lakini hawakiri Imani ya “Mungu mmoja katika nafsi tatu,” kwa tendo hilo wanakosa uhalali wa kuwa Wakristo katika maana halisi. Mfano: Kundi hili si tu kwa upande wa Waislamu wanaokiri kuna Mungu moja tu bila nafsi hizi tatu, lakini pia ‘Mormons,’ Seventh Day Adventists,’ na ‘Mashahidi wa Jehova.’
Wapendwa, Utatu Mtakatifu ni tendo la Mungu kuufungua upendo wake wa ndani kwetu. Kwa ufunuo huu kwetu wa siri za ndani za Mungu juu ya maisha yake, Mungu anatualika katika upendo wake kiasi kwamba hakuna binadamu yeyote alionao au awezaye kufanya hivyo. Kwa mantiki hii, haijalishi kwa kiasi gani tunajaribu, hatuwezi kufahamu fumbo hili la kujifunua Mungu kwetu kwa namna hii ya ajabu. Kama binadamu twaweza kuongea kuhusu mawazo yetu na hisia zetu kadiri ya mang’amuzi yetu, bali kile tulicho kinabakia kuwa fumbo kwetu. Mungu kwa kinyume chake, yu wazi katika ukamilifu wote kwa yeye mwenyewe. Hata hivyo haikumlazimu kujifunua  hivyo kwetu; tunajifunua wenyewe kwake (kadiri ya uwezo wetu) kwa wachache, na wakati mwingine kwa marafiki wetu wa karibu. Lakini kwa upande wa Mungu sisi si tu viumbe, bali ni marafiki wake wa pekee. Yesu Kristo analifunua jambo hili kwa kusema, “15 Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:15
Wapendwa, nafsi ya kwanza ya Utatu Mtakatifu ni Baba. Hata kwa wazazi wanaojali na kuwajibika, mwanamke ambaye ni zaidi ya kitu kingine chochote ni Mama, na mwanaume kwa yeye kuwa Baba ni zaidi ya kitu kingine chochote wake, hata hivyo haijawa hivyo wakati wote, na haiwezekani kuwa hivyo kila wakati. Ni mara ngapi tumeshuhudia wazazi hawa kuzisaliti ndoa zao na hata familia zao?
Lakini ambacho Kristo amekifunua kuhusu Baba yake, ndiyo uwasilia wa Yeye mwenyewe. Yeye Kristo, “ndiye BABA”-katika mwono wa kuwa kile alicho Baba. Kila anachokifanya Kristo, kila neno analoliongea, kwa kila namna anavyotutazama na kutuchukulia ni kama “Baba.” Ni mara ngapi tunamfikiria Mungu na kusahau ukweli huu! Na ni kwa namna ipi inahathiri maisha yetu tunaposhindwa kuishi katika upendo,-nguvu ya upendo wa Baba ambaye anatupenda zaidi ya namna tunavyojua!
Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu ni  Mwana. Mwana amechukua umbo la kibinadamu na kukaa nasi kutufanya kuwa kama yeye na kuunganika naye kwa kufuata mfano wake, kuwa wana wa Baba (“Filii in Filio”) kwa kila kitu tunachofanya, na kusema, kwa kila namna tunavyomtazama yeye.
Nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu ni Roho Mtakatifu. Upendo kati ya Baba na Mwana ni wa Kimungu. Kwa nguvu na uhimara huo, ni upendo usiotenganishwa. Upendo huo umemwagwa katika mioyo yote kwa kushiriki tendo la kipentekoste kupitia sakaramenti ya Ubatizo. Upendo huo ndiyo unaotuwezesha kuhusiana na Mungu kama Baba, kutambua kwa Kristo ndugu zetu. “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba,” Rum 8:15. Roho Mtakatifu anatupa ushuhuda kwamba sisi ni watoto wa Mungu, na kwa pamoja tu warithi na Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu ni wamilele. Huyu ni Mungu anayetusubiri katika umilele. Je, si wakati wa kumfahamu? Ni kweli hatuwezi kwa kutokea mbali kuelewa fumbo la maisha yake ambayo amekuwa huru kujifunua kwetu. Lakini hatuwezi kusahau kwamba Roho Mtakatifu huishi ndani ya mioyo yetu, na tunapomuhusisha kwenye sala zetu, kuishi Imani yetu katika kweli, tunapata mang’amuzi ya Mungu ambayo huenda zaidi ya huwezo wetu kibinadamu, na kutupa uhakika kwamba twaitaji kumjua yeye uso kwa uso katika umilele.
Wapendwa, Mungu wa uwepo wetu si mwenyewe. Wanaoishi maisha upweke na wajane, wanaojiona kuwa wamesahauliwa, kutengwa, wote hao ni uchaguzi na uangalizi wa pekee wa Mungu. Hawapo wenyewe hata kidogo. Mungu ni tajiri na mwingi wa uhai, hata kabla ya kuziumba mbingu na nchi. Wazee, wasiojiweza/walemavu, wasio na kazi, masikini, wote wanaalikwa na Yeye kutambua kwamba Mungu yupo nao. Unachotakiwa kufanya ni kumtafuta kila siku, na zaidi kama umebatizwa, kwani umewekewa unatajiri wake, uhai wake, na dhamani yake, (utu wa kimungu) uliowekwa na kupigwa chapa ndani yetu. Kwa mantiki hii, sote tuliobatizwa tuna muhuri huu wa Utatu Mtakatifu.
Dada Getrudi ambaye ni Katibu wa Baraza la walei Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu hupenda kula chakula chake cha mchana katika Mgahawa ujulikianao kwa jina la “Utulivu.” Kabla ya kula hupenda kufanya ishara ya Msalaba, ila kwa kujificha, ili asionekana na watu.
Siku moja Paroko wa Parokia hiyo naye katika mizunguko yake alipenda kujipatia chakula cha mchana katika mgahawa huo. Sifa ya mgahawa huu inaendana na jina lake. Hivyo baada ya kuagiza chakula na kuletewa, alimwona jamaa mmoja mwenye ndevu ndefu na kikofia cheupe akimkazia macho meza jirani yake. Mtu huyu alimwogopesha sana kutokana na matukio mbalimbali yenye uhusiano na mtu huyu na hivyo alisita kufanya ishara ya Msalaba. Hivyo ilimlazimu kuifanya ishara hiyo ya msalaba akiwa amegeukia ukutani.
Baba Paroka akiwa katika mahangaiko hayo ya kufanya ishara hilo ya msalaba na baada ya kumalizia, “..na Roho Mtakatifu,” hamadi, akakutana uso kwa uso na Katibu wa Baraza la Walei Parokia akiwa naye akifanya kama alivyokifanya yeye. “Tumsifu Yesu Kristo Baba. Nawa upo hapa? Kulikoni Baba Paroko?” Katibu alisema huku akiwa na hofu. “Huwezi jua usalama wetu upo wapi siku hizi. Ni vizuri kutowakwanza wengine,” Baba Paroko alijitetea kwa kile alichokifanya.
Ndugu yangu, tusisahau maneno haya ya Yesu, “Basi kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu  aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.” Mt 10:32-33. Ni mara ngapi tunalisaliti fumbo hili, na kuukana Utatu huu Mtakatifu?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU KWA UWEPO WAKO NA HASA KUPITIA MASAKRAMENTI YAKO, TUWEZESHE KUISHI FUMBO HILI TAKATIFU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario