viernes, 15 de mayo de 2015

Tafakari: Ijumaa wiki ya 6 ya Pasaka-B


IJUMAA WIKI YA 6 YA PASAKA-B
15/5/2015
Somo: Mdo 18:9-18
Zab: 46
Injili: Yoh 16:20-23a
Nukuu:
Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13
bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15
Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20
Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22
TAFAKARI: “Furaha katika Mateso”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari neno hili kadiri ya masomo yetu ya leo, “Furaha katika Mateso.” Licha ya kuwa na mitazamo tofauti kuhusu mateso kadiri ya Imani zetu, uhalisia wa mateso ni mang’amuzi ambayo kila mmoja wetu anaweza kuuelezea. Wapo ambao wameenda mbali zaidi na kusema kwamba kitendo cha mtoto mdogo kulia baada ya kuzaliwa tu, ni ujumbe kwetu kwamba dunia hii tunayoishi hatuwezi kuitenganisha na mahangaiko na mateso yetu.
Mateso ni hali na ni sehemu ya maisha ya binadamu yeyote bila kujali imani yake. Ila "mateso" huwa na maana tu katika sababu na tafsiri yake.
Swali:
-Nini sababu ya mateso yangu?
-Nini sababu ya uwepo wetu?
-je, kuna maana yeyote ya mimi kuwepo?
-kama ipo malengo yake nini hasa kwa hali hii niliyonayo sasa?
Wapendwa yapo majibu rahisi hasa pale tu tunapojua chanzo chake.
Mfano;
1. kuna magonjwa ambayo tunayapata tukijua chanza chake ni nini, tiba yake, na matokeo yake hujulikana. Hapa mwathirika ni kufuata ushauri wa daktari yote huueleweka.
2. Yapo pia mateso kutokana na magonjwa fulani twajua tu chanzo chake, ila tiba na kupona kwake bado ni kitendawili kikubwa.
3. Yapo pia mateso ambayo uelekea kuwa na magonjwa ambayo hatujui chanzo chake, tiba yake, na mwisho hatujui kupona kwake. Hapa binadamu hupita katika uvuli mzito wa umauti. Hapa pia yawezekana kukawa na Mateso tu ambayo si ugonjwa ila ni hali ya "sintofahamu." Unakuta unateseka ila huna maelezo yanajitosheleza.
Aina hii ya tatu ina ugumu sana kwa binadamu kuipokea. Tunajisikia kutengwa hata kutokuona umaana wa Mungu kwetu kama (upendo wake, uwezo wake na hata umuhimu wake)
Bila tafsiri yenye kujumuisha, "sababu, lengo, na uwepo wa Yesu katika historia nzima ya wokovu wetu," ni vigumu kuona maana, lengo, na FURAHA katika mateso yetu kwa ujumla
na zaidi kwa kipengele cha tatu.
Ni ndani ya Yesu Kristo, na katika Yesu Kristo twaweza elewa "fumbo" la TESO na siyo "jibu" lake. Ufahamu huu ukiwepo basi ni mwanzo wa FURAHA katika TESO lolote lile.
Jambo la kufahamu:
Teso au mateso si jambo au hali ya kudumu milele likiwa ndani ya Yesu Kristo na katika Yesu Kristo. Rejea;
-Mt 4:24, -Mt 16:21
-Mk 8:31, -Lk 9:22,
-Lk 16:28, -Lk 17:25,
-Lk 24:26,
 -Rom 8:18
2 Kor 1:6,  2 Kor 1:7
-Wafp 3:10, -Wakol 1:24
2 Tim 1:12, 2 Tim 3:11
1 Pet 4:13, 1 Pet 5:9
Ufu 1:9
Kwa kushiriki ubinadamu wetu na katika safari ya wokovu wetu, Yesu Kristo kaondoa umilele wa Teso/mateso yetu na kulipa/kuyapa maana. Akiwa ndiye Njia, ukweli, na uzima (Yoh 14:6), Yesu anachagua njia ya mateso kutupatia wokovu wetu. Hapa ndipo mateso au teso huwa na maana ndani ya Yesu Kristo na kwa ajili ya Yesu Kristo.Twashiriki pia mateso na wengine katika Kristo tukitambua ukweli huo wa fumbo la teso kwa njia ya sala na majitoleo yetu tukiwa katika muunganiko na Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, Mtume Paulo anaburuzwa na Wayahudi mbele ya Mahakama ya Kirumi kushtakiwa kwa kosa la kuwavuta watu ili wamwabudu Mungu. Je, kunakosa lolote kumwabudu Mungu? Kumwabudu Mungu kama tendo la kujisalimisha kwake ndiyo njia pekee ya kujenga mahusiano yetu na Mungu ya karibu. Ndio njia pekee ya kuzijua siri na ufahamu wa Kimungu. Kwa Mtume Paulo mambo yalikuwa kama hivi: “Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13. Kwa vile Mtume Paulo alisimama katika kweli na haki, Galio anawashangaa Wayahudi kwa madai yao juu ya Paulo, naye anasema, bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15. Tukio hili ni mateso katika furaha. Ni furaha kwa sababu tunajua tunateseka katika kweli, ila hatujui kwa nini tunateswa, na watesi wetu wameingiwa upofu wa kujui kweli. Mtume Paulo analitambua jambo hili kwa undani kabisa na hivyo anasema, “kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18
Kuyaona mateso katika mtazamo huu wa Mtume Paulo ni kukomaa katika Imani, na kujua kusudi la malengo yako hapa duniani. Malengo yetu hapa duniani ni ya muda mfupi, ukilinganisha na umilele baada ya maisha haya. Yesu Kristo anatufumbulia jambo hili katika injili ya leo kwa kusema, Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Wito wa Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu mateso ni kwamba yatupasa kutazama mbele zaidi yaani kile kitakacho kuwa baada ya mateso hayo. Kwa hiyo ni lazima kuona na kutambua kiini cha mateso yetu, na mahusiano yake ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, furaha halisi na isiyo na kikomo ni furaha ya kuteseka pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye. Kuteseka pamoja na Kristo ni kuyatazama mateso yote ndani na katika Kristo, na kumshirikisha mateso hayo ambayo kwayo yeshapewa maana na Kristo. Maana ya mateso katika Kristo ni USHINDI. Kristo kayashinda mateso na kwake tu, mateso huwa maana. Hivyo, Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Furaha hii baada ya ushindi huu wa mateso ndani na katika Kristo, ni furaha ya kweli na isiyo na kikomo.
Ndugu yangu tusisahau maneno haya mazito ya Bwana wetu Yesu Kristo; “Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26. Kuyakimbia mateso ndani na katika Kristo ni kuukimbia utukufu wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!

BWANA WETU YESU KRISTO TUPE UWEZO WA KUYAPOKEA YOTE KATIKA WEWE NA NDANI YA WEWE ILI TUPATE MAANA NA FURAHA KATIKA MATESO YETU NA YA WENZETU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario