viernes, 15 de mayo de 2015

TAFAKARI: SHEREHE YA KUPAA BWANA WETU YESU KRISTO MBINGUNI

JUMAPILI YA SABA YA PASAKA
SHEREHE YA KUPAA BWANA-B
Somo I: Mdo 1:1-11
Zab: 47:1-2, 5-6, 7-8,
Somo II: Efe 1:17-23
Injili: Mk 16:15-20
Nukuu:
hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu,” Mdo 1:2-3
Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7
Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8
Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni,” Mdo 1:11
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye,” Efe 1:17
akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Mdo 1:22-23
Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
TAFAKARI: “Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”
Wapendwa wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anafanya Sherehe ya Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo Mbinguni. Kupaa huku mbinguni ni moja ya sharti ya kuletewa Roho Mtakatifu kama mshauri wetu. Kupaa kwa Yesu Mbinguni kunatuwajibisha kila mmoja wetu, yaani mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake kama Sakramenti ya wokovu wetu. Ni Kanisa katika maana hii, akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Mdo 1:22-23
Hivyo leo tutafakari kwa undani wajubu huu tulioachiwa na Kristo na tuufanye kweli tukitambua jambo hili si la kupita tu, bali li hai kila siku ya maisha yetu kama sehemu muhimu ya ufuasi wetu kwa Kristo. Hivyo basi wazo kuu na tafakari yetu leo ni kwamba, “Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”
Ndugu yangu, katika maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo kuna mambo makuu matatu yanajionyesha: La kwanza kabisa, yeye akiwa ndiyo Habari njema ya mwokovu wetu, jambo hili linakuwa ndicho kipaumbele chake cha kwanza na kielelezo cha maisha yake. Kuhubiri habari njema za Ufalme wa mbinguni. "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili," Mk 1:15. Hii ndiyo ajenda mzito na mahususi Yesu aliyowaachia wanafunzi na Kanisa kwa upana wake kabla ya kupaa mbinguni akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Ujumbe huu mahususi wa ufalme wa Mungu, unaambatana na hukumu kwa Yule asiyeamini. Wajibu wetu, yaani kwa kila mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake ni kulihubiri neno la Mungu bila kukoma. Mwijili Mathayo kalihusisha tendo hili la kuhubiri neno na ufalme wa Mungu na Sakramenti ya Ubatizo. Maana yake, siyo tu kulihubiri neno la Mungu, bali na kuwavuta watu kwa Mungu na kuuonja upendo na furaha hiyo. "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi" Mt 28:19-20.
Jambo la pili lilikuwa kuwachagua wanafunzi wake ikiwa ndiyo mwendelezo wa "Habari njema" kizazi na hata kizani hadi mwisho wa nyakati. Yesu katika hili anatoa ahadi kwa wanafunzi wake, "Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu," Yoh 14:18.
Na jambo la tatu lilikuwa ni kulitakasa hekalu. Hekali libakie kuwa ni nyumba ya sala. Tunaona mtafaruku wa Yesu hekaluni na wale wavunja fedha. Na hasa pale alipojibu na kusema," livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha," Yoh 2:19. Kwa naama ya ndani zaidi, "Hekalu" ilimaanisha mwili wake mwenyewe na pia ni mwili wa kila mbatizwa. "Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake,"  Yoh 2:21. Mtume Paulo anatuambia miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu. "Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?" 1Kor 3:16.
Ni kwa mtazamo huu Mtume Paulo anasema 'ole wake asipoihubiri njili,' na ni pale pia Yesu anawakumbusha umati waliomjia kuwa yampasa kwenda sehemu nyingine pia kwa ajili ya Habari njema za ufalme wa Mungu. "Akawaambia, "twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa HIYO NALITOKEA," Mk 1:38. Ndugu yangu ni kwa maana hiyo na sababu hiyo "YESU KUTOKEA" kwetu-kuhubiri Habari njema za ufalme wa Mungu na wokovu wetu. Tusipolifanya jambo hili kuwa ajenda muhimu kwa kila mmoja kama mbatizwa, na kwa Kanisa kama chombo cha kutuwezesha kuelekea na kuufikia uzima na utakatifu wetu, basi maisha yetu yatakuwa kama upepo tu hapa duniani. Ndugu yangu, jambo la kujiuliza; nini umuhimu wa utume wako? Pili, nini hasa gharama za kutimiza utume wako? Tuanze na hilo la kwanza. Kuna mambo sita muhimu kuhusu umuhimu wa utume wako.
1. Utume wako ni mwendelezo wa utume wa Yesu hapa duniani.
Wapendwa, kama wafuasi wake, tunapaswa kuendeleza kile alichoanzisha Yesu. Yesu hatuiti tu kuja kwake, lakini kwenda kwa ajili yake. Utume wako ni wa muhimu sana kiasi kwamba Yesu anauzungumzia mara tano, katika njia tofauti tano;
-"Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari," Mt 28:19-20.
Hili ndilo Agizo la Yesu;
-"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe," Mk 16:15
-"na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu," Lk 24:47
-"Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi," Yoh 20:21
-"Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu;  nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi," Mate 1:8
Ndugu yangu, maagizo hayo matano, ni kama Yesu anatuambia hivi, "hakika nataka ninyi mwelewe jambo hili!" Agizo kuu la Yesu (Mt 28:19-20), amepewa kila mfuasi wa Yesu, siyo la wachungaji "makleri" na wamishenari peke yao. Hili ni agizo kutoka kwa Yesu, na si la hiari. Haya maneno ya Yesu siyo "pendekezo kuu." Ndugu, kama wewe ni sehemu ya jamii ya Mungu, utume wako ni wa lazima. Kuupuza itakuwa kutotii.
Ndugu, yawezekana ulikuwa hujui kwamba Mungu anakuwajibisha kwa watu wasiomwamini wanaokuzunguka. "Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mikononi mwako," Eze 3:18. Ndugu, sina lengo la kukuogofya, ila ndiyo ukweli wa Mungu. Wewe ni Mkristo pekee ambaye baadhi ya watu watakufahamu, na utume wako ni kuwaambia Habari za Yesu.
2. Utume wako ni upendeleo wa ajabu.
Ndugu yangu, ingawa ni wajibu mkubwa, pia ni heshima kubwa kutumiwa na Mungu. Mtume Paulo anasema, "Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho," 2Kor 5:18. Kwa maana hiyo, utume wako unahusisha upendeleo wa aina mbili: kumtumikia Mungu na kumwakilisha. Tunakuwa na ubia na Mungu katika kujenga ufalme wake. Eneo hili tunahitaji sana hekima ya Mungu na mwongozo wa Roho wake Mtakatifu. Yote yanawezekana tunapojisalimisha kwake, ndani na katika Yeye. Hivyo, Yesu anatuahidia jambo hili anaposema, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye,” Efe 1:17. Hakuna woga wala hofu tuyafanyapo Mapenzi ya Mungu kwani yote hayo si kwa nguvu zetu wenyewe, bali kwa mkono wa Mungu kwa sababu yote ni kwa ajili ya ufalme wake aliyotuandalia.
3. Kuwaambia wengine wanavyoweza kupata uzima wa milele ndiyo jambo kubwa unaloweza kuwatendea
Ndugu yangu, kama jirani yako angeugua KANSA au UKIMWI na ukawa unafahamu tiba, lingekuwa kosa kubwa kutomfahamisha habari hizo za kuokoa maisha. Ni kosa pia kuficha njia ya msamaha, lengo, amani, na uzima wa milele. Tuna habari kuu kuliko zote duniani, na kushirikisha wengine ndiyo wema mkubwa kuliko wote unaoweza kumfanyia mtu.
Ndugu yangu, tatizo moja tulilonalo Wakristo wa muda mfupi ni kwamba tunasahau jinsi tulivyokuwa hatuna matumaini tulipoishi bila Yesu. Lazima tukumbuke kwamba haijalishi watu wanaonekana kutosheka na kufanikiwa kiasi gani, bila Yesu hawana matumaini na wamepotea na pia wanaelekea katika kutengwa na Mungu milele. "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo," Mate 4:12. Ndugu yangu, kila mtu anamhitaji Yesu.
4. Utume wako una umuhimu wa milele.
Ndugu yangu, ufanyacho sasa kitakuwa na matokeo makubwa kwa hatima ya milele ya watu wengine, hivyo utume wako ni wa muhimu kuliko kazi nyingine yoyote, mafanikio yoyote, au lengo lolote utakalolifikia katika maisha yako hapa duniani. Matokeo ya utume wako yatadumu milele; matokea ya kazi yako hayawezi.
Ndugu yangu, hakuna tena narudia, hakuna Chochote unachofanya kitalingana na kuwasaidia watu wafanye uhusiano wa milele na Mungu. Ndiyo maana lazima tuwe na juhudi kubwa katika utume wetu. Yesu anasema, "imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi," Ndugu, ukweli ni kwamba saa inakwenda na maisha yako ya utume yanapita. Anza utume wako wa kuwafikia wengine sasa! Tutakuwa na muda wa milele wa kufurahi na wale wote tuliowaleta kwa Yesu, lakini tuna muda mfupi tu wa maisha yetu ili kuwafikia. Yesu anatuambia leo kwamba katika jambo hili la kujitoa muhanga kwa ajili yake, litaambatana na ishara nyingi, na kuufichua umungu wake. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
Ndugu, jambo hili halimaanishi uache kazi yako ili uwe mwinjilisti wa kudumu. Mungu anakutaka uwashirikishe watu wengine karibu yako Habari njema. Kama mwanafunzi, mama, mwalimu wa shule, mfanya biashara, au meneja, au chochote unachofanya, unatakiwa daima kutafuta watu Mungu anaowaweka mbele yako upate kuwashirikisha injili. Si lazima kutumia vipaza sauti, bali kwa maisha yako ya kumpendeza Mungu huongea zaidi. Ni kutoa ushuhuda wa ukimya "silence witness" na kuwa barua za kusomwa na wengine. "Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama," 2Kor 3:2-3
5. Utume wako hukupatia umuhimu wa maisha yako.
William James alisema, "Matumizi bora ya maisha ni kuyatumia kwa kufanya kitu kitakachodumu kuliko maisha yako." Ndugu yangu, ukweli ni kwamba, ni ufalme wa Mungu tu ndio utadumu milele. Achana na "viprojekti" vya zima moto! Wakoleze watu Imani. Unacheka!
Kwa sababu hiyo, tunatakiwa kuishi maisha yanayoongozwa na malengo-maisha ya kuabudu, kuwa na ushirika, kukua kiroho, huduma, na utume wetu duniani. Matokeo ya shughuli hizi yatadumu milele. Mipango yetu ya kichungaji ilenge kwenye malengo hayo. "Viprojekti" vyovyote visivyo lenga mambo hayo ni sawa na kupiga mashutu kwa bidii kubwa na ustadi mkubwa pasipokuwa na goli.
Ndugu yangu, kama utashindwa kutimiza utume uliopewa na Mungu hapa duniani, utakuwa umepoteza maisha Mungu aliyokupa. Mtume Paulo anasema, "Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya neema ya Mungu," Mate 20:24
Ndugu yangu, kuna watu katika sayari hii ambao ni wewe tu unayeweza kuwafikia kwa sababu ya mahali unapoishi na jinsi Mungu anavyokufinyanga. "Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako," Zab 119:73
Ndugu yangu, iwapo mtu mwingine atakuwa mbinguni kwa sababu yako, maisha yako yatakuwa yamefanya tofauti ya milele. Anza kuangaza katika maeneo ya utume wako binafsi na usali, "Mungu, nani umemweka katika maisha yangu ili nimweleze Yesu?
6. Ratiba ya Mungu ya kuhitimisha historia inashikamana na ukamilishaji wa agizo tulilopewa.
Siku hizi kuna hamu kubwa ya kujua kuhusu kurudi kwa Yesu mara ya pili na mwisho wa ulimwengu. Swali:
-Je, itakuwa lini?
Ndugu yangu, kabla Yesu hajapaa mbinguni wanafunzi walimuuliza swali hili hili na jibu lake lilikuwa wazi. Yesu anasema, "si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi," Mate 1:7-8. Wanafunzi wanapotaka kuongea juu ya unabii, Yesu kwa haraka aligeukia uinjilishaji akiwataka wakazanie utume wao ulimwenguni. Anasema jambo hilo akimaanisha,"mambo ya kina kuhusu kurudi kwangu hayawahusu. Jambo la muhimu kwenu ni utume niliowapa. Kazanieni hilo!
Ndugu yangu, kusikia juu ya muda halisi wa kurudi kwa Yesu Kristo ni upuuzi, kwa sababu anasema, "walakini wa Habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila Baba peke yake," Mt 24:36. Kwa nini wewe unajaribu kuibashiri? Tunachokijua kwa hakika ni kwamba: Yesu hatarudi mpaka kila mmoja Mungu anayemtaka asikie habari njema awe amesikia. Unashangaa! Yesu anasema, "tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja," Mt 24:14. Umeipata hiyo?
Ndugu yangu, kama unataka Yesu arudi haraka tia bidii kutimiza utume wako, siyo kubashiri unabii. Ni rahisi kutiwa wasiwasi, kwa sababu shetani angependa wewe ufanye kitu chochote kuliko kushirikisha watu wengine imani yako. Atakuruhusu ufanye aina zote za mambo mema ili mradi hakuna mtu yeyote utakayempeleka mbinguni. Lakini mara utakapokuwa na bidii katika utume wako, tegemea Ibilisi kukutupia kila aina ya mambo yatakayokuachisha kazi hiyo. Ndugu yangu, inapotokea hivyo, kumbuka maneno ya Yesu, "mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu," Lk 9:62
Je, zipi gharama za kutimiza utume wako?
Ndugu yangu, kutimiza utume wako vyema itakulazimu uache ajenda zako na ukubali mjadala wa Mungu kwa ajili ya maisha yako. Huwezi tu kung'ang'ania mambo mengine yote ambayo ungependa kufanya katika maisha yako. Lazima tuseme kama Yesu, "Ee, Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke, "Lk 22:42.
Hapa unampatia Mungu haki zako, matazamio yako, ndoto zako, mipango yako, na matakwa yako. Acha kuomba sala za kibinafsi kama vile, "Mungu bariki ninachotaka kukifanya." Badala yake sali hivi, "Mungu nisaidie nifanye kile unachokibariki." Unamkabidhi Mungu karatasi tupu yenye jina lako chini na unamwambia ajaze kwa kina sehemu iliyobaki. "bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki." Rum 6:13b
Kama utajitoa kutimiza utume wako katika maisha bila kujali gharama, utapata baraka za Mungu kwa njia ambazo watu wachache huzipata. Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kufanya kwa ajili ya mtu ambaye amejitoa kutumikia ufalme wa Mungu. Yesu anasema, "Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa," Mt 6:33. Tutimize wajibu huu muhimu. Hapa ndipo kwenye KANISA HAI NA LINALOSAFIRI KATIKA NJIA ILIYO SALAMA. Kwa wale tuliobado na ndoto ya kujua Yesu Kristo atarudi lini, tumeambiwa leo; Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni,” Mdo 1:11. Mara baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, wale wanawake walijidamka kwenda Kaburini malaika aliwaambia ujumbe huu, “enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7. Ujumbe mahususi kuhusu Galilaya ni kwamba tutakutana naye katika maisha yetu ya kawaida kila mmoja kadiri ya wito na maagano yake na Mungu. Kwa maana nyingine tunakutana na Kristo mfufuka kwenye utume wetu. Hapo ndipo Galilaya yako. Leo Yesu anavyopaa kwenda Mbinguni anawakumbusha Wagalilaya na sisi pia. Hivyo atakaporudi siku ya mwisho ni vyema akukute vyema kwenye utume wako.
Mzee Masumbuko alijaliwa kuwa na familia kubwa yenye watoto nane, na hivyo kufanya wote kwa ujumla kuwa kumi. Kazi ya Mzee Masumbuko ili ulinzi wa kampuni moja ya wanyama pori. Mara zote alipewa zamu ya usiku, hivyo kumfanya kuanzia safari kuelekea lindoni mida ya saa tisa alasiri.
Maisha kwa ujumla kifamilia hayakuwa rahisi. Kipatano chake na ukubwa wa familia yake havikuendana kabisa. Jambo hili lilikuwa sababu kuwa ya manung’uniko yake na hata kumlaumu Mungu kwa kutokuwa na usawa. Ila kilichompa faraja mara zote ni tabia njema za watoto wake, na upendo wa watoto wake na mke wake, na juhudi walizokuwa nazo katika masomo. Msingi mkubwa katika familia hii ulikuwa sala. Walimtegemea Mungu kwa kila kitu, na hawakufanya chochote kabla ya kukikabidhi mikoni mwa Mungu.
Siku mmoja akiwa anaelekea kazini akiwa anamenya limao ili ale kwani mchana ulipita mkavu bila kitu, alitazama majumba barabarani huku akivuta harufu nzuri ya vyakula kutoka kwenye majumba hayo, alijawa huzuni na kuanza kumlalamikia Mungu. “Ee Mungu, tazama leo mimi na watoto wangu hatujala, nami naenda huko lindoni sijui kitakachotokea usiku wa leo. Ee Mungu ona, majumba haya na harufu hizi za vyakula, leo familia yangu ni kilio tu,” alijisemea barabarani kama mwendawazimu hivi.
Akiwa anakula lile limao, alitazama nyuma na kuona kuna mtu anaokota yale maganda na kuyala. Tendo hilo lilimfanya asisikie tena harufu za vile vyakula kutoka majumba yale yaliyokuwepo kando ya barabara. Akajiuliza, “Je, kama huyu anakula haya maganda niliyoyatupa, si inanipasa kumshukuru Mungu katika jambo hili? Mimi nakula limao hili na ninakibarua, je, huyu sidhani hata kama kibarua anacho. Ee Mungu unirehemu na niwe na moyo wa shukrani hata kwa hiki kidogo ninachokipata.”
Ni mara ngapi mimi na wewe tunakuwa kama Mzee huyu Masumbuko?
Tumsifu Yesu Kristo!


EE MUNGU, TUTUMIE VYEMA KAMA VYOMBO VYAKO KUENEZA INJILI YAKO NA HASA KWA MAISHA YETU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario