ALHAMISI
WIKI YA 7 YA PASAKA-B
21/5/2015
Somo:
Mdo 22:30, 23:6-11
Zab
15
Injili:
Yoh 17:20-26
Nukuu:
“Ndipo
Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi
kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?” Mdo 23:3
“Paulo
akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa,
Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako,” Mdo 23:5
“Ndugu zangu, mimi ni
Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa
wafu,” Mdo 23:6b
“Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani
yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki
ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21
“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote
nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla
ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24
“Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo;
ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh
17:26
TAFAKARI: “Furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya
Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari neno hili,
“furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya
Kristo.” Kuishi katika dhamira safi ni kuishi maisha yasiyo na hatia, yaani
maisha yanayompendeza Mungu. Ni kuishi bila dhambi, ingawa
twaweza kudondoka tena na tena. Kuishi katika dhamiri safi kunatufanya kuwa
tayari kwa jambo lolote wakati wote wote. Mt. Aloyce wa Zonzaga ni mfano wa mtu
aliyeishi katika dhamiri safi muda wote. Wakati fulani alipokuwa anacheza
mchezo fulani, mlezi wake alimjia na kumwuliza hivi, “endapo umebakia muda
mfupi tu na iwe mwisho wa dunia hii ungefanyaje? “Nitaendelea kucheza mchezo
huu,” Mt. Aloyce alimjibu mlezi wake bila wasiwasi. Jibu la Mt. Aloyce wa Gonzaga
linaonyesha jinsi gani alivyokuwa tayari katika yote.
Mtume Paulo dhamiri safi aliyokuwa nayo haogopi
kuyapokea mateso yote kwa ajili ya Kristo. Paulo anapigwa na kudhalilishwa bila
kulijua kosa lake. Wapo pia wengi kati yetu bila kujua makosa yao wanajikuta
wakikabiliwa na mateso hata wengine wanapoteza maisha yao.
Kristo anatuombea umoja
na amani, akijua ulimwenguni humu tutapatwa na matatizo mengi. “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo
ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate
kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21. Sala hii ya Bwana wetu
Yesu Kristo inaonyesha dhamiri safi aliyokuwa nayo. Dhamiri hii safi ndiyo
inayomsukuma pasipo shaka kujonge mateso, na kifo kile cha msalaba.
Tunapoyapokea mateso
kwa dhamiri safi tunauhakika wa kuwa pale alipo yeye, Yesu Kristo baada ya
maisha haya ya hapa duniani. Uhakika huu anatupa Yesu anaposali, “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po
pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda
kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24
Wapendwa wana wa Mungu,
yatupasa kuisha ndani ya pendo la Mungu nyakati zote na majira yote. Kuuishi
upendo huu wa Mungu ni kutambua pia jina lake ambola Mwana amefanya bidii zote
kutufundisha. Hivyo Yesu anasema, “Nami
naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda
mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26. Ndugu yangu, kuishi
upendo wa Mungu na kutenda yaliyomema huijenga na kuikuza dhamiri safi ndani
mwetu.
Tumsifu Yesu Kristo!
UNIUMBIE MOYO SAFI
UIFANYE UPYA ROHO ILIYOTULIA NDANI MWENGU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario