miércoles, 27 de mayo de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 8 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 8 YA MWAKA-B
28/5/2015
Somo: Ybs 42:15-25
Zab: 32:2-3, 4-5, 6-7, 8-9
Injili: Mk 10:46-52
Nukuu:
“Yeye huchunguza vilindi, na moya wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana Aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu,” Ybs 42:18
“Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lolote ambalo limefichwa naye,” Ybs 42:20
“Vyote vinahitilafiana, wala hakufanya chochote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio,” Ybs 42:24-25
Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51
TAFAKARI: Naye ni nani atakayekinai kwa kuutazama utukufu wa Mungu?
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari uzuri wa Mungu kwa vile alivyoviumba. Tunapotazama uzuri huu wa uumbaji wa Mungu, tuanze kwa kutazama maajabu hayo katika uumaji wetu. Hakika tutazamapo uzuri huo tunagundua kwamba, “vyote vinahitilafiana, wala hakufanya chochote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio,” Ybs 42:24-25. Tazama yote aliyokujalia Mungu na ulivyo wa pekee, na anavyokupenda kama ulivyo na anavyotaka uwe kama alivyokuumba ili uwakilishe utukufu wake. Pamoja na upendeleo huo kwako, Mungu anapenda kuuchunguza moyo wako kama unashukrani juu ya upendeleo huo kwako.
Wapendwa, moyo usio na shukrani ukausha mema yote. “Yeye huchunguza vilindi, na moyo wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana Aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu,” Ybs 42:18. Wengi wetu hatuoni sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna anavyotukirimia. Wengi wetu mara tuamkapo kitandani kwa mfano; hatuwezi hata kufanya ishara ya msalaba, kwa kutambua tendo hili la utukufu wa Mungu kwa kutupenda upeo. Mara tufanyapo tendo la Msaba kwa Imani na sauti ya ndani, twatambua na kukiri haya juu ya msalaba: “huu ndio ule mti wa msalaba ambao wokovu wetu umetukikwa juu yake.”
Hata baada ya kulindwa na kuepushwa na majanga mengi katika maisha kwa upendeleo huu wa Mungu, bado hatuoni sababu ya kusema neno asante. Giza lijapo twajirusha kitanbani kama mzingo usio na mwenyewe tukijua tutaamka salama kama tulivyofanya tendo hilo siku ya jana. Je, hatujawahi kusikia ‘alilala salama lakini hakuweza tena kuiona siku ya pili?’ Ndugu yangu, “Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lolote ambalo limefichwa naye,” Ybs 42:20. Mungu wetu ni mvumilivu sana. Ni mvumilivu kwa sababu Yeye ni matumaini kwetu. Matumaini haya ni matokea ya upendo aliokuwa nao kwetu usiokuwa na mfano.
Pamoja na upendeleo huo, Mungu kwa kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, yupo tayari kuyafanya yote ayatakayo Baba yake ili utukukufu wake utawale daima. Tatizo kubwa kwetu sisi tu vipofu na kushindwa kuona utukufu huo wa Mungu kwa vile alivyoviumba ikiwa ni pamoja na wewe wenyewe. Ni mara ngapi tunashindwa kumshukuru Mungu kwa uzuri na mema waliojaliwa rafiki na majirani zetu? Badala yake tumekuwa sababu na vielelezo vikuu kuudhoofisha utukufu huo wa Mungu.
Kama tuna nia ya kubadilika ili tuone vizuri kadiri ya utukufu wa Mungu, yatupasa kufanya hatua ya kwanza sisi wenyewe kama alivyofanya yule mwombaji kipofu kwa kupaza sauti ili asikike na kuponywa na Bwana Yesu. Nasi kutokana na udhaifu huo yanitupasa kusema toka moyoni, ‘Yesu mwana wa Daudi, unirehemu.’ Haya ni majuto ya kweli. Hivyo Yesu anamjibu na kumwambia, “Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51. Kwa tatizo alilokuwa nalo mwombaji huyu kipofu alijibu kadiri ya tatizo lake, yaani anataka kuona. Je, mimi na wewe swali la Yesu linatuhusu? Kama linatuhusu, je unajibu sahihi kutokana na swali la Yesu? Mjibu Yesu tatizo lako na uwe huru kuudhihirisha utukufu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NATAKA KUONA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario