JUMATATU WIKI YA 8 MWAKA “B”
25/5/2015
Somo: Ybs 17:20-28
Zab: 31
Injili: Mk 10:17-27
Nukuu:
“Kwake makosa yao hayakufichika, na dhambi zao zote zipo
mbele zake,” Ysb 17:20-21
“Hata hivyo huwajalia wale watubuo kurudi, na wao
wanaopotewa na saburi huwafariji,” Ybs 17:24
“Basi umrudie Bwana na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za
uso wake na kupunguza kimwazo,” Ybs 17:25
“Yesu
akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu,”
Mk 10:18
“Yesu
akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda,
ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni;
kisha njoo unifuate,” Mk 10:21
“Walakini
yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na
mali nyingi,” Mk 10:22
“Ni
rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika
ufalme wa Mungu,” Mk 10:25
“Yesu
akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo;
maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27
TAFAKARI: “Maisha mapya ndani na katika
Kristo baada ya anguko ni kuanza upya kwa kukiri na kutubu thambi zako.”
Wapendwa wana wa Mungu, hakuna anayetaka kuishi katika
mateso, hata yule aliyefikia hatua ya kuyatoa maisha yake kutoka na kadhia
zitokakanazo na sintofahaumu katika maisha. Mfano, anayejinyonga kwa sababu ya
matatizo fulani, huwa na imani kwa tendo hilo atakuwa ameepukana na tatizo hilo
kwa wakati ule na kuwa sehemu salama zaidi. Yawezekana analifanya jambo hili
akiikimbia aibu na karaha atakazozipata endapo ataendelea kudumu katika tatizo
hilo. Kwa uwelewa huu kimaisha, leo kwa pamoja embu tutafakari neno hili;
“Maisha mapya ndani na katika Kristo baada ya anguko ni kuanza upya kwa kukiri
na kutubu thambi zako.” Neno kuanza upya kwa binadamu yeyote yule ni gumu sana
kutokana na yale yaliyokwisha ujenga ubinadamu wetu. Kuachana na yale ambayo
ndiyo mfumo mzima wa maisha tuliyoyazoea si jambo rahisi.
Wapendwa wana wa Mungu, katika maisha ya binadamu yeyote
yule hakuna mtihani kubwa kama wa kufanya maamuzi, na tena maamuzi sahihi ya
maisha yake. Bila shaka kama tunataka kuwa kitu kingine tena kizuri, hatunabudi
kufanya mtihani huu mgumu katika maisha. Hivyo, kuishi katika Kristo na ndani
ya Kristo, yatupasa kufanya maamuzi haya, na hasa juu ya toba ya kweli. Makosa
uyafanyayo ubaki kuwa siri ndani yako, ila kwa Mungu hakuna liwezwalo kufichwa
wala kusahaulika kama halijafanyiwa toba ya kweli. Hivyo, “Kwake makosa yao
hayakufichika, na dhambi zao zote zipo mbele zake,” Ysb 17:20-21. Pamoja na
uhalisia huu wa Mungu juu ya mwono wa dhambi zetu, Mungu hajawa hakimu wa jino
kwa jino. Mungu mara zote amekuwa subirá kwetu, ili hali tu tupate muda wa
kujirudi na kufuata mpanga mzima wa maisha ya umilele. Ndiyo maana waovu katika
uovu wao uendelea kuishi tena kwa kujinasibu kuliko watu wema wakati mwingine.
Je, mwenzangu, unaitaji “offer” gani zaidi ya hii?
Ni kwa subira hii ya Mungu hapendi tuangamie milele. Sababu
kubwa ya kufanya haya yote ni kwamba kila mmoja wetu amebeba chapa yake katika
uumbaji wetu. Ndugu yangu umeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ndani yako
umebeba chapa ya Mungu. “Hivyo huwajalia wale watubuo kurudi, na wao
wanaopotewa na saburi huwafariji,” Ybs 17:24. Hapa ndipo kwenye UPENDO na
HURUMA ya Mungu.
Katika hali hii, twapaswa kufanya jambo moja tu mbele ya
Mungu ili tuendelee kuwa marafiki zake. Jambo hili ni kuomba radhi kwa kujuta
dhambi zetu na kuanza maisha mapya naye. “Basi umrudie Bwana na kuacha dhambi;
omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kimwazo,” Ybs 17:25. Dhambi zetu
mbele ya Mungu ni vikwazo katika mlolongo wa neema anazopenda kutukirimia bila
mipaka. Kuisha katika hali ya dhambi ni kujifungia kerezeni mwenyewe ili hali
unajua hakutakuwa na huduma za aina yoyote.
Wapendwa, Injili ya leo inatualika kutambua uwepo wa Mungu
na nafasi yake katika maisha yetu, kuhusiana na swala zima la ukamilifu wetu. Ukamilifu
wa binadamu unaompelekea kuwa na mastahili mbele ya Mungu ni kuisha kusiko na
hatia. Kwanza kabisa yatupasa kujua Mungu ni nani katika maisha yetu. Yesu
anatoa angalisho mapema kabisa kwa kusema, “Kwa
nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu,” Mk 10:18. Wema
katika maana halisi ya neno hilo u na Mungu. Kama wema u na Mungu, yote
tuyafanyayo hayawezi lingana na wema wa Mungu.
Ndugu zangu katika
Kristo, yapo mambo mengi yanayotutia matumaini na heri hapa duniani. Ila kwa
mambo hayo hatuwezi kufananisha na uzuri na wema wa Mungu. Tukirejea falsafa ya
Plato, twaweza kusema kwamba, yote tuliyonayo yanaakisi tu wema na uzuri halisi
alionao Mungu peke yake. Ni katika hali hii, Yesu anampa changamoto kijana yule
aliyejiona mkamilifu na hasa amri za Mungu. Jambo hili kwake halikuwa matatizo
kabisa kwani amri hizi alizishika vizuri tangu utoto wake. Hivyo Yesu
anamwambia baada ya kumkazia macho na kumpenda, “Umepungukiwa
na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na
hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21.
Ndugu yangu, yawezekana
hauna mali katika maana ya vitu vya kuonekana na kushikika, ila umejaliwa mali
za kiroho kama; akili nzuri, uwezo wa kusikiliza na kutatua matatizo yaani
busara na hekima, na hata maisha ya ukaribu na watu. Haya pia Yesu anatuambia
tuenende kukayauze na kuwapa maskini. Kuyauza haya hasa katika maana ya utajiri
wa Kiroho, ni kutoshikamanana nayo na kujifananisha nayo kama kielelezo cha utu
wetu mbele za watu na kujitofautisha mbele za wengine na haya yanayoonekana
pekee mbele za watu. Kuwapa maskini kunamaanisha kwamba haya yote tumepewa ili
tuyatoe kwa wahitaji. Kila mmoja wetu hapa duniani ni mwitaji. Hivyo kila mmoja
wetu ni masikini katika hali ya kuhitaji kile asichokua nacho. Hivyo kuishi
kwetu hapa duniani kama wana wa Mungu na wenye hofu ya Mungu, ni kuishi katika
kufaidiana kuliko kwa kweli, yaani niwe kwaajili ya mwingine.
Wapendwa wana wa Mungu,
kuyaona maisha katika mtazamo huu ni sawa na kujikana mwenyewe. Hivyo hatuoni
ajabu kwa kijana yule kuondoka mbele ya Yesu baada ya kupewa maana ya pili ya
sababu ya maisha yake hapa duniani. Kwa maana hiyo, “yeye
akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali
nyingi,” Mk 10:22. Kwa maana nyingine kijana huyu alikuwa na vipaji vingi, au
uwezekano mwingi kimaisha. Jambo hili linamtia hofu ya kuishi kwa sababu
aliishi kwa ajili yake tu. Kuishi kwetu hapa duniani si kwaa ajili yako tu.
Ubinadamu wetu, kama ulivyo katika kitabu cha mwanzo juu ya uumbaji, tumepewa
mamlaka ya uumbaji shirikishi na Mungu. Hivyo tupo hapa duniani kwa ajili ya
wengine pia waone na kutambua uso wa Mungu. Ukweli huu juu ya uumbaji wetu na
sababu zake, tusipoutilia maanani hatutaona wajibu wa kuwa matajiri. Hii ndiyo
sababu ya Yesu kusema hivi juu ya matajiri wasiojua wajibu huo katika dhana
nzima ya kufaidiana, “Ni rahisi ngamia
kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,”
Mk 10:25. Ndugu yangu, chunguza utajiri wako.
Jambo hili si rahisi kulifanya
kwa sababu sote kama binadamu tunayo silika ya umimi. Ila Mtu kuwa huru na
kuishi katika umilele yampasa kuushinda umimi wake. Kinachohitajika hapa ni
utashi wa kweli wa kufanya yaliyo mema na yenye mtazamo wa kimungu kila siku.
Tukiwa katika mwelekeo huu kimaisha, hakuna cha kutushinda. Hivyo Yesu anasema
katika hali hii ya kibinadamu; “Kwa
wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,”
Mk 10:27. Ndugu yangu, kwa Mungu yote yanawezekana. Chukua hatua.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU MWEMA NIONGOZE
KATIKA KWELI YAKO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario