JUMATANO
WIKI YA 7 YA PASAKA-B
20/5/2015
Somo: Mdo 20:28-38
Zab: 67
Injili: Yoh 17:11b-19
Nukuu:
“Jitunzeni
nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa
waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu
yake mwenyewe,” Mdo 20:28
“Basi,
sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza
kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa,” Mdo 20:32
“Sikutamani
fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi
wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale
waliokuwa pamoja nami,” Mdo 20:33-34
“Katika
mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia
wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni
heri kutoa kuliko kupokea,” Mdo 20:35
“Baba
mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi
tulivyo,” Yoh 17:11b
“Mimi
nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu,
kama mimi nisivyo wa ulimwengu,” Yoh 17:14
“Mimi
siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu,” Yoh 17:15
“Na
kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh
17:19
TAFAKARI:
“Kujitoa kuliko kweli katika utume wetu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tulitafakari neno hili, “kujitoa kuliko kwa kweli katika utume wetu.” Mara
nyingi tumesikia na hata kusoma sehemu mbalimbali kwamba, uongozi katika Kanisa
ni utumishi. Bila shaka msingi huu unatoka kwa Kristo mwenyewe aliyejitoa bila
kujibakiza. Kama kweli tu wafuasi wake hatunabudi kufuata nyayo zake
kisawasawa. Kwa maana hiyo Kiongozi ni kutumika kwa ajili ya wale waliokupa dhamana
uwaongoze, au uliopewa dhamana hiyo na Mamlaka husuka kuongoza. Naye Yesu
anaseme, “mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa
wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Namna hii ya
kujitoa haitazami maslahi binafsi. Utumishi wa aina hii siyo ajira.
Ni kwa mtazamo huu
tunamwona Mtume Paulo akiwa Mileto anawaaga wazee wa Efeso kwa kutambua kazi
yake na wito wake kwao. Huku ndiko kujitoa bila kujibakiza katika utume. Mtume
Paulo anatoa usia wake na kusema, “jitunzeni
nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa
waangalizi ndani yake, mpate kulilisha Kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu
yake mwenyewe,” Mdo 20:28. Kadiri ya uzoefu, mara nyingi tunapoondoka sehemu
zile tulizotumika vyema, mwovu shetani huzinyemelea na kuziharibu. Hivyo ni
vyema kuaga vyema na kutoa msisitizo maeneo yale ambayo yapaswa kuyalindwa kama
mboni ya jicho. Tumenunuliwa kwa damu ya Yesu, hivyo tuilinde Imani yetu
vizuri.
Wapendwa pamoja na
kutoa angalisho hili, ili tuendelee kuzichota neema kwa kazi yetu iliyotukuka
kiutume, tusisahau kuunganika katika sala. Tusiache kukesha katika sala na
kuyakabidhi yote mikoni mwa Mungu. Mtume Paulo anatambu umuhimu wa sala na
kuyaweka yote mikono mwa Mungu. Yote tuyafanyayo yataendelea na kudumu
tukiyaweka mikoni mwa Mungu. Hivyo, “Basi,
sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza
kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa,” Mdo 20:32. Kuyaweka
yote mikoni mwa Mungu ni kutambua nafasi yetu kama binadamu, na nafasi ya Mungu
ambaye ndiye mwezeshaji wa yote. Mtume Paulo anatambua jambo hili anaposema,
“Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila
mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza
ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye,” 1Kor
3:5-7. Ufahamu huu ni muhimu sana katika utume wetu.
Wapendwa wana wa Mungu,
kuna hatari kubwa pale tunapojifananisha na matunda ya kazi zile tunazofanya na
kutotambua tumeyafanya hayo yote kwa kuwezeshwa na Mungu. Hakuna sababu yoyote
ya kujifananisha na kile ulichokifanya. Ukiona watu wanakusifia kuliko kweli,
basi elewa umetumika vyema na Mungu. Hivyo sifa na shukrani zirudisha kwa
Mungu. Kwa kufanya hivi, ni kutambua ubinadamu wako, na uwepo wa Mungu kwa kile
ulichokifanya. Hapa ndipo tunapoomba tena kwa tendo hili la kushukuru. Mtume
Paulo anafahamu ukweli huu anapotoa mapato na matumizi ya mahitaji yake ya kila
siku mbele ya wale aliowatumikia kwa kusema, “Sikutamani
fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi
wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale
waliokuwa pamoja nami,” Mdo 20:33-34. Katika utume wetu, yatupasa kutokuwa
mizigo kwa watu. Jaribu kila siku kuwa mbunifu wa mambo yenye kujenga maisha ya
watu na Imani dhabiti juu ya Mungu wanayemwamini. Huku ndiko kulenga juu alipo
Kristo. “Basi mkiwa mmefufukiwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo
aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Kama hayo tuyafanyayo na
kuyatafuta katika utume wetu hayalengi pale Kristo alipo basi tunapoteza Muda
bure.
Wapendwa katika Kristo,
yote tuyafanyayo yawalenge hasa wanyonge na wasiokuwa na fursa katika jamii
tunayoishi. Huyu ndiye Kristo anayeteseka katikati yetu muda wote. Mtume Paulo
anasema, “katika mambo yote nimewaonyesha
ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka
maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea,”
Mdo 20:35. Huu ndiyo umoja na mshikamano anaotutaka Kristo tuuishi na kila
mmoja wetu bila kujali historia yake, familia yake, nafasi yake katika jamii,
ukoo wake, kabila lake, na hata utaifa wake. Umoja huu na mshikamano katika
Imani ndiyo aliotuombea Kristo kabla ya kifo, mateso, na kufufuka kwake. “Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde
hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo,” Yoh 17:11b. Umoja huu anaotuombea
Kristo ni umoja wa Utatu Mtakatifu na usiogawanyika, yaani: Baba, Mwana, na
Roho Mtakatifu.
Tendo hili na hali hii
tunapoiishi ndiyo furaha ya Mungu, na chukizo kwa yule Mwovu Shetani. Hivyo kwa
namna nyingine yatupasa kuwa imara sana katika Imani. Ulimwengu utatuchukia kwa
umoja wetu. Ulimwengu utatuchukia kwa sababu uraia wetu si wa hapa duniani,
bali mbinguni. Hivyo Kristo analijua jambo hili na anatuombea katika sala hii
maalum, “Mimi nimewapa neno lako; na
ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa
ulimwengu,” Yoh 17:14. Tumeumbwa ili tuishi milele. Mateso tutakayokutana nayo
katika ulimwengu huu ni njia mojawapo ya utakaso wetu tukiuchuchumilia
utakatifu huku tukiishi kwa uaminifu wote licha ya mahangaiko na majaribu.
Hivyo Kristo hatuombei sisi kuondolewa katika ulimwengu huu, bali tuuishinde na
kujinyakulia taji la uzima wa milele. Tunaweza jambo hili tukiwa ndani na
katika Yesu Kristo kwa sababu Kristo kesho tuombea kwa Baba yake atulinde na
yule mwovu. “Mimi siombi kwamba uwatoe
katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu,” Yoh 17:15. Hakuna sababu ya
kujiona kutengwa na Mungu wakati wa shida na dhiki kubwa.
Wapendwa wana wa Mungu,
vita hii dhidi ya mwovu shetani tutaishinda tu tukiwa na Kristo kwa sababu
amejiweka wakfu kwa ajili yetu. Kristo amejitenga na kufanya kazi hiyo tu ya
kutukomboa kwa upendo wake wote. “Na kwa
ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh
17:19. Nasi tutatakaswa katika kweli. Utakataso huu katika kweli ni kuwa
waaminifu katika ufuasi wetu kila siku tunapojitoa na kutumika kwa mpango wake
Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo.
EE YESU KWA MFANO WA
MAISHA YAKO, TUWEZESHE NASI TUJITOE BILA KUJIBAKIZA KATIKA UTUME WETU KILA
MMOJA KADIRI YA WITO WAKE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario