jumamosi wiki ya 7 ya pasaka-b
23/5/2015
Somo: Mdo 28:16-20,
30-31
Zab: 10
Injili: Yoh 21:20-25
Nukuu:
“Ikawa
baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika
akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno
lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali
nimefungwa, tokea Yerusalemu,” Mdo 28:17
“Basi
kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana
nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli,” Mdo 28:20
“Akakaa
muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga,
akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu,
na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na
mtu,” Mdo 28:30-31
“Yesu
akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate
mimi,” Yoh 21:22
“Kuna
na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata
ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa,” Yoh 21:25
TAFAKARI:
“Na tuenende katika wema na kutenda mema hata pale tunapokatishwa tamaa; mti wa
matunda ndio urushiwao mawe.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo kadiri ya msomo yetu, napenda niwaalike nyote kwa pamoja
tulitafakari neno hili, “Na tuenende katika wema na kutenda mema hata pale
tunapokatishwa tamaa; mti wa matunda ndio urushiwao mawe.” Ni hali ya
kibinadamu na silika yake kulipa kisasi pale anapofanyiwa ndivyo sivyo. Kwa
upande mwingine si jambo la kawaida kwa yule aliyempokea Kristo kuwa Bwana na
mwokozi wa maisha yake kuyafanya hayo yasiyopendeza machoni mwa Mungu.
Tunayofanyiwa leo kinyume cha utashi wetu na yasiyo haki kabisa, Kristo
alishafanyiwa tena kwa kiwango cha juu kabisa, na kisicho fikirika kwa uwezo wetu
kama wanadamu. Tunapopatwa na sintofahamu kama hizi katika maisha tusiache
kusonga mbele kwa kutenda mema. Kristo mara zote awe ndiye kielelezo na sababu
ya kusonga mbele kwa yale mema yanayopiwa mawe.
Mtume Paulo ambaye kwa
fitina nyingi za Wayahudi, mema yake yote aliyoyafanya mbele zao, yanapigwa
mawe. Ni ukweli usiotia shaka kabisa hakuna arushaye mawe kwenye mti usio na
matunda. Mtume Paulo kwa kubambikiziwa kesi zisizona kweli, aliamua kukata
rufaha kwa dola ya Kirume ili haki itendeke. Hapa lazima tuelewa ukweli huu;
Mtume Paulo hafanyi jambo hili kwa kujitetea, bali kuwasaidia watesi wake
watambue makosa yao na kutenda mema. Hata katika hali hii ya mateso na
mahangaiko, Mtume Paulo anazidi kutoa somo kwa watesi wake. “Ikawa
baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika
akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno
lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali
nimefungwa, tokea Yerusalemu,” Mdo 28:17. Ndugu yangu, Je! katika hali hii
unaweza kutoa ushududa wa Furaha kwa watesi wako na ukabaki kuwa tumaini kwa
wale waliochini yako?
Mtume
Paulo anayo furaha ya ndani na matumaini makubwa katika mateso yake hayo.
Tunaliona jambo hili anapoyasema maneno haya kwa matumaini makubwa. “Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama
na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la
Israeli,” Mdo 28:20. Mtume Paulo anamatumaini makubwa katika ukombozi wa Taifa
lake licha ya uhasi wao kwa Kristo. Mara baada ya kufika Roma, Mtume Paulo
hakuona walalamikaji wake, wala kushtakiwa kwa lolote. Hata katika hali hii ya
uonevu, Mtume Paulo hakatishwi tamaa kulihubiri neno la Mungu. Hivyo, “Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba
yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu,
na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na
mtu,” Mdo 28:30-31. Ndugu yangu, kila mmoja wetu kwa nyakati tofauti kesha
umizwa na kwa maumivu hayo yamemjengea jeraha kubwa sana moyoni. Kwa kumtazama
Mtume Paulo, hakuna sababu ya kutembea na kovu hili. Usijiwekee ukuta mbele ya
matumaini yake. Vunja ukuta huo na uwe huru mwili na roho. Yawezekana kwa
kipindi hiki unachojizibia kuona mbele mwanga wa Kristo, watesi wako hawana
habari nawe tena. Watesi wa Mtume Paulo hawana habari naye tena kwani kesha
waacha Jerusalemu. Furaha yao kwa sasa ni kutouona uwepo wa Mtume Paulo ambaye
alikuwa mwiba kwao. Je, wanaweza kutuliza ukumu ya Mungu kwa matendo yao yasiyo
haki?
Yesu
Kristo anatupa ujasiri wa kuishi kwa kumfuata yeye tu, na kutoa mashaka yote
tunayokutana nayo katika maisha. Ni katika Kristo tunabaki na uzima wetu. Yesu
Kristo alizua mtafaruku mkubwa kwa Mitume wake aliposema kati yao mmoja wao
hataonja mauti. Hivyo hisia za Mitume zilimwendea Mtume Yohane kwa sababu Yesu
alimpenda sana. Hakika Yesu hakumaanisha kwamba Mtume Yohane hatoonyo mauti,
bali alimaanisha yeyote atakaye mfuata kwa uaminifu atakuwa na uzima ndani
yake. “Yesu
akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate
mimi,” Yoh 21:22. Ndugu yangu, mfuate Kristo kila siku, na kuwa tayari
kujifunza kutoka kwake kila siku.
Yapo mambo mengi ya
kujifunza kutoka kwa Kristo. Haya tunayoshirikishana kila siku, ni kukusaidia
tu nawe uweze kujijengea tabia ya kuyatafakari makuu ya Kristo ndani ya maisha
yako kila siku. Anza kwa kujihubiria mwenyewe, na ujumbe huo utakaoupata
washirikishe na wengine. Kristo anavyoongea ndani yako, anataka pia upeleke
ujumbe huo kwa wengine, na kutufanya sisi kuwa habari njema ya wokovu kwa wote.
Hivyo basi, “Kuna na mambo mengi
aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu
usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa,” Yoh 21:25. Ndugu yangu anza
kuyatafakari hayo machache kwa kuyatazama maisha yako kwa hayo machache, na
Mungu anakufunulia makubwa zaidi kila siku. Wewe si bahati mbaya leo na sasa.
Tumsifu Yesu Krito!
EE YESU
NIFUNULIE SIRI YA MATESO YANGU, NA NIJAZE FURAHA NINAPOYATAZAMA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario