IJUMAA
WIKI YA 7 YA PASAKA-B
22/5/2015
Somo:
Mdo 25:13-21
Zab:
102
Injili:
Yoh 21:15-19
Nukuu:
“Na
wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama
nilivyodhani, bali walikuwa na
maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya
mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu
hai,” Mdo 25:18-19
“Nami
nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka
kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya,” Mdo 25:20
“Akamwambia
mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile
alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe
umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu,” Yoh 21:17
“Akasema,
Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na
kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh 21:18
TAFAKARI: “Lisha, Chunga, Lisha Kondoo Wangu.”
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na Mtume Petro kumkana
Yesu mara tatu, leo Petro anatambua kosa lake, analikiri kosa lake, na yupo
tayari kufuata maagizo na mfano wa Kristo kama mchungaji mwema. Petro
anaulizwa swali mara matatu, kama kumkumbusha alivyomkana Kristo na Bwana wake
mara tatu. Mtume Petro kuulizwa kwa swali hiii mara ya kwanza kunabeba msingi
wa muulizo wa mara nyingine mbili zilizobaki. Yesu anamuuliza Petro, Je! Simoni
wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Neno “hawa” limebeba ujumbe mzito sana
katika maisha ya kiroho.
Kumpenda Kristo kuliko
“hawa” kwa maanisha kumpenda Yesu Kristo kuliko vitu vingine vyote. Kumpenda
Kristo kusiko fananishwa na yale tuyaonayo na hata kuyagusa. Ni kumfanya Kristo
kuwa ndiyo njia ya kweli, uzima wa kweli, na ukweli usiotia shaka katika maisha
yetu ya kila siku. Ni kutokuwa na mashaka kabisa tunapokuwa katika mikono yake.
Ni kumfanya Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako. Swali hili aliloulizwa Petro,
nasi tunaulizwa kila siku tunapoenenda
katika njia yake.
Wapendwa wana wa Mungu,
jibu la Petro lilikuwa, “ndiyo Bwana, wewe wajua nakupenda.” Maneno haya
ayasemayo Mtume Petro yanamzingi wake kiimani. Mtume Petro hayatamki tu kwa
kumpendezesha Kristo, licha kwamba alimkana kuwa hamjui. Wakati Yesu
anafundisha kuhusu fumbo la mwili na damu yake kuwa ni chakula cha uzima, wengi
wa wanafunzi wake walimwacha. Mafundisho haya yalikuwa mzito sana. Hivyo Yesu
aliwauliza wale Thenashara, “Je! Ninyi nanyi
mwataka kuondoka?” Yoh 6:67. Mitume wote
walikuwa kimya kama wamemwagiwa maji. Ni Mtume Petro tu kwa ujasiri wake
aliweza kumjibu Kristo, tena kwa kile kilichokuwa kimeujaza moyo wake na
kusema, “Bwana! Twende kwa nani?
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh
6:68-69. Huu ndiyo msingi wa jibu la Petro kwamba, “Ndiyo Bwana, wewe wajua
nakupenda.”
Hata hivyo baada ya
kujibu kuwa anampenda Kristo, Mtume Petro anapewa majukumu ya jibu lile
alilolitoa. Mtume Petro anawajibishwa kutumika kama alivyomkiri Kristo na
kusema, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye
hai,” Mt 16:16. Maagizo ya Kristo kwa Petro ni kulisha kondoo zake, kuwalinda,
na kuwalisha. Kazi hapa ni kulisha, kulinda, na kulisha. Hii ndiyo maana ya
Jina lake ‘Petro,’ “Nami nakuambia, Wewe
ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya
kuzimu haitalishinda. Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:18-19. Mtume Petro anarudishiwa mamlaka yake
aliyopewa na Kristo.
Wapendwa
tendo hili la Kristo analoonyesha kwa Mtume Petro, ni tendo la upendo wa hali
ya juu, na hata sisi hasa pale tunapojenga uhusiano naye tena baada ya kumwasi.
Yesu yupo tayari kutupokea kama tulivyo ili mradi tujirudi na kufanya toba ya
kweli. Kristo hakuvunja ahadi yake aliyokwisho isema juu ya Petro licha ya
udhaifu aliyouonyesha. Tendo hili linatukumbusha pia simulizi lile la mwana
mpotevu. Upendo huu wa kibaba ndiyo upendo wa Mungu kwetu. Mungu anasema na mtu
mwovu, “Haya, njoni,
tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe
kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18.
Hii ndiyo huruma wa Mungu kwetu. Mtume Petro anarudishiwa mamlaka yake na
kupewa kazi ya kulisha, kulinda, na kulisha daima kondo wake Kristo.
Wajubu huu aliopewa
Petro, nasi tumepewa kwa njia ya ubatizo wetu na kushiriki ukuhani wa Kristo
ulio wa kawaida. Hivyo twawajibika kufanya kazi hii ya kulisha kondoo zake,
hasa kwa matendo yetu mema pale tulipo. Tuwe mfano kwa matendo yetu na kuwa
barua za kusomwa na wegine. “Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni
mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa
kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali
kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo
ni mioyo ya nyama,” 2Kor 3:2-3. Kuishi katika ukweli huu, kutatugharibu maisha
yetu kama mshumaa uwakavyo nakutoa mwanga ndivyo hivyo hivyo unavyokufa. Kwa
wajibu huu wa kuwa barua za kusomwa na wengine kwa matendo yetu mema, Yesu
anamwambia Petro, “Amin, amin, nakuambia,
Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini
utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua
usikotaka,” Yoh 21:18. Mtiririko wa ukweli huu ndiyo unaomkuta Mtume Paulo
anavyohukumiwa na kwenda kifungoni huko Roma. Mwisho wa siku Mtume Petro, na
Paulo waliyatoa maisha yao na kufa kifo dini kumshuhudia Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
Ninyi ndinyi barua yetu iliyoandikwa si kwa wino,
bali kwa Roho wa Mungu aliye hai. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario