ALHAMISI WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo:
Mdo 22:30, 23:6-11
Zab
16:1-2a, 5, 7-8, 9-10, 11
Injili:
Yoh 17:20-26
Nukuu:
“Ndipo Paulo
akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi
kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?” Mdo 23:3
“Paulo akasema,
Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee
mabaya mkuu wa watu wako,” Mdo 23:5
“Ndugu zangu, mimi ni
Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa
wafu,” Mdo 23:6b
“Wote wawe na umoja;
kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu;
ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21
“Baba, hao ulionipa
nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu
ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24
“Nami naliwajulisha
jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani
yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26
TAFAKARI:
“Furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya
Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ipo “furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya
Kristo.” Kuishi katika dhamira safi ni kuishi maisha yasiyo na hatia, yaani
maisha yanayompendeza Mungu. Ni kuishi bila dhambi, ingawa twaweza kudondoka
tena na tena katika dhambi. Tuapodondoka katika dhambi tuijongee neema na
huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho. Ndugu yangu, neema na huruma ya
Mungu kupitia Sakramenti hii ya Upatanisho ni kubwa kuliko dhambi zetu. Kuishi
katika dhamiri safi kunatufanya kuwa tayari kwa jambo lolote wakati wowote. Mt.
Aloyce wa Zonzaga ni mfano wa mtu aliyeishi katika dhamiri safi muda wote.
Wakati fulani alipokuwa anacheza mchezo fulani, mlezi wake alimjia na kumwuliza
hivi, “endapo umebakia muda mfupi tu na iwe mwisho wa dunia hii ungefanyaje?
“Nitaendelea kucheza mchezo huu,” Mt. Aloyce alimjibu mlezi wake bila wasiwasi.
Jibu la Mt. Aloyce wa Gonzaga linaonyesha jinsi gani alivyokuwa tayari katika
yote.
Mtume Paulo kwa dhamiri
safi aliyokuwa nayo haogopi kuyapokea mateso yote kwa ajili ya Kristo. Paulo
anapigwa na kudhalilishwa bila kulijua kosa lake. Wapo pia wengi kati yetu bila
kujua makosa yao wanajikuta wakikabiliwa na mateso hata wengine wanapoteza
maisha yao.
Kristo anatuombea umoja
na amani, akijua ulimwenguni humu tutapatwa na matatizo mengi. “Wote wawe na
umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani
yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21.
Sala hii ya Bwana wetu Yesu Kristo inaonyesha dhamiri safi aliyokuwa nayo.
Dhamiri hii safi ndiyo inayomsukuma pasipo shaka kujongea mateso, na kifo kile
cha msalaba.
Tunapoyapokea mateso
kwa dhamiri safi tunauhakika wa kuwa pale alipo yeye, yaani, Yesu Kristo baada
ya maisha haya ya hapa duniani. Uhakika huu anatupa Yesu anaposali, “Baba, hao
ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu
wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh
17:24
Wapendwa wana wa Mungu,
yatupasa kuisha ndani ya pendo la Mungu nyakati zote na majira yote. Kuuishi
upendo huu wa Mungu ni kutambua pia jina lake ambalo Mwana amefanya bidii zote
kutufundisha. Hivyo Yesu anasema, “Nami naliwajulisha jina lako, tena
nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe
ndani yao,” Yoh 17:26. Ndugu yangu, kuishi upendo wa Mungu na kutenda
yaliyomema huijenga na kuikuza dhamiri safi ndani mwetu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Baba, hao ulionipa
nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu
ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24
Tusali:-Ee
Mungu Mwenyezi, uniumbie moyo safi uifanye upya roho iliyotulia ndani mwangu.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario