lunes, 8 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 4 YA PASAKA


JUMATANO WIKI YA 4 YA PASAKA

Somo: Mdo 12:24-13:5a

Zab: 67:2-3, 5, 6, 8

Injili: Yoh 12:44-50

Nukuu:

Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2

Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao,” Mdo 13:3

Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka,” Yoh 12:44-45

Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46

Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu,” Yoh 12:47

Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yoh 12:48

TAFAKARI: “Ndani na katika Kristo Yesu kuna Nuru ya Kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu aliye hai kwa nyakati tofauti katika historia ya wokovu wetu anajitambulisha kama Mungu muumbaji wa nuru. Naye anasema, “ Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa 45:7. Yesu Kristo anatuagiza tuwe Nuru na Chumvi kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake pale alipo. Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:13-14. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tu chumvi ya ulimwengu pale tunapokuwa tayari kushuka katika hali zetu na kuchanganyika na watu kwa lengo la kuwa kikolezo cha kumfanya Kristo ajulikane kwao na siyo sisi kama tulivyo.

Kanisa la Mwanzo na hasa baada ya hujuma zile zilizofanywa na Wayahudi waliompiga Kristo na wafuasi wake, kamwe halikuacha kuwa nuru na chumvi. Kwa kulitambua hilo hawakuacha kuwa kikolezo cha Kristo na kumfanya Kristo ajulikane kwa wengine wasiomjua. Kwa kuwa kikolezo cha Kristo kwa mfano wa Chumvi, na Maadili mema kwa mfano wa Nuru, Roho Mtakatifu aliyaongoza yote waliyofunga na kuomba. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,” Mdo 13:2. Hata pale walipojibiwa maombi yao hawakuacha kuyakabidhi yote mikoni mwa Mungu ili Kristo aendelee kutenda makuu juu yao. Na “ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao,” Mdo 13:3. Huu ni mfano mzuri wa mshikamano katika kweli ile anayotufundisha Kristo katika Kanisa lake kila siku.

Wapendwa katika Kristo, tusipo fanya hili ambalo ndila lengo na shabaha ya chumvi hatutakuwa na maana yoyote hata kama tukibaki katika ubora wetu. Kutotimiza lengo kwa kile ulichokusudiwa ni sawa na kutokuwepo. Hivyo ndivyo Yesu asemavyo kama lengo hilo halitotimizwa, ‘chumvi hivyo hutupwa nje na kukanyagwa na watu.’ Zaidi ya kushuka na kujichanganya na watu na kuwa kikolezo kwao-kumfanya Kristo ajulikane, yatupasa kuwa nuru katika maana ya kuwa na maadili mema. Maadili haya mema kama Wakristo ndiyo hututofautisha na wengine katika ona yetu kama Kristo, fikiri yetu kama Kristo, tenda yetu kama Kristo, na amua yetu kama Kristo. Kwa kuyafanya haya pasipo unafiki, Kristo huinuliwa katika ulimwengu, na nuru yake usambaa kote, nasi kwa tendo hilo huesabiwa haki na Mungu. Hivyo kimaadili yatupasa kuwa juu kama ilivyo kwa mwanga ili usambae eneo kubwa taa yapaswa kuwekwa mahali pa juu. Naye Yesu anasema, Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga,” Lk 8:16; Lk 11:33. Ni kwa maadili yetu mema huwa nuru pale tulipo na kwa mataifa yote.

Matendo yako mema yanayosukumwa na maadili yako mema kama Mkristo na Mfuasi ya Yesu Kristo ni nuru hai pale ulipo. Hivyo Yesu anasisitiza na kusema, Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Ndugu yangu, mtazamo wako katika kuona, kufikiri, kuamua na kufanya hutegemea sana nuru uliyokuwa nayo, yaani, maadili yako ambayo husukuma tenda yako kama mwili, nafsi na roho. Na hiki ndicho ulicho, yaani, Mwili, Nafsi, na Roho-Mtu kamili. Katika kweli hii Yesu anasema, Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!” Mt 6:22-23. Maadili mema husukuma matendo mema ya mtu, na hili ndiyo taa la mwili.

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo katika mwono wa Nuru ndiye HUKUMU yetu katika wema na haki, na hasa pale tunapomwamini. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu,” Yoh 3:18-19. Kwa nini basi twajisikia ahueni tungali katika giza? Bila shaka kutokana na mwelekeo wa dhambi na anguko lake, shetani ujigeuza na kuwa mfano wa nuru katika mtazamo wa giza na kutufanya kugaagaa katika dhambi. Mtume Paulo anasema, Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru,” 2Kor 11:14. Ukweli ni kwamba Yesu Kristo mwenyewe ndiye nuru halisi ya ulimwengu, na ndani na katika yeye hakuna giza bali uzima wa milele. Yesu anatuhakikishia hili na kusema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima,” Yoh 8:12. Ndugu yangu bado tu wajisikia ahueni kuishi katika giza?

Kumwamini Kristo ni kukaa katika nuru na ndicho alichokijia ili wewe na mimi tuwe katika nuru. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46. Kutokumwamini Kristo ni kukaa katika giza kunakosukumwa na matendo maovu, Yoh 3:19. Nuru ambayo kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo ni maadili mema ambayo husukuma matendo yake mema, tunda lake ni haki na kweli. Ni kweli isiyotia shaka kwamba mwenye maadili mema huwa na hofu ya Mungu, hivyo kutenda kwake huwa kwa haki na kweli. Mtume Paulo anaweka wazi kweli kwa wale wamwaminio Kristo na kusema, Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana,” Efe 5:8-10. Palipo na wema wote, haki na kweli, kuna upendo wa kweli na watu huishi kindugu.

Hivyo ndugu yangu, kupendana kindugu ni kukaa katika nuru na kinyume chake ni giza tupu. “Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho,” 1Yoh 2:10-11. Ndugu yangu, kwa nini basi hadi leo hupendi kupatana na ndugu yako? Kama kweli wamwamini Kristo Yesu kuwa nuru halisi ya ulimwengu, mbona basi unashindwa kuwa chumvi na nuru hapo ulipo? Ni jukumu lako kama mfuasi wa Kristo kumfanya Kristo aonekane kwa watu wote hata wale wasio mwamini.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46

Tusali:-Ee Yesu uliye Nuru halisi, tufanye kuwa nuru na chumvi pale tulipo kila mmoja kadiri ya hali na wito wake. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario