JUMATATU WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 14:5-17
Zab: 115: 1-2, 3-4,
15-16
Injili: Yoh 14:21-26
Nukuu:
“Na
makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa
Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme,
kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji,” Mdo 14:11-12
“Walakini
mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio
wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema,
Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi;
twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na
kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote
vilivyomo; ambaye zamani
zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe,” Mdo 14:14-16
“Yeye
aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye
atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21
“Mtu
asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu,
ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24
“Lakini
huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26
TAFAKARI:
“Na tuwe kile kilicho kadiri ya makusudio ya Mungu katika uumbaji wake, sisi
kama wanadamu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
siku yetu hii ya leo na tulitafakari neno hili kadiri ya masomo yetu ya leo,
“na tuwe kile kilicho kadiri ya makusudi ya Mungu katika uumbaji wake, sisi
kama wanadamu.” Mungu kutuumba sisi kama tulivyo, yaani wanadamu anasababu
kubwa sana katika historia nzima ya wokovu wetu. Moja ya sababu kubwa ya
kutuumba kama tulivyo wanadamu ni kuwa na uwezekano wa kutushirikisha yale
yaliyo ya kimungu [yake], na kuyafanya kama yalivyo tukiwa wawakilishi wake
halisi. Bila shaka hii ndiyo sababu kubwa ya kutuumba kwa sura na mfano wake.
Pamoja na
kutokukubalika kwa Mtume Paulo na wenzake na Wayahudi kutokana na ujumbe
waliokuwa wakiutoa ikiwa ni mwendelezo wa kazi ya Kristo, wanakimbilia Listra
na Derbe kupata hifadhi. Mtume Paulo na Barnaba wanafanya mambo makuu kwa mkono
wa Mungu, na kuleta tafrani kubwa. Tendo hili la uponyaji wa mtu mwenye udhaifu
wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, linaibua hisia za watu hawa wa
Likaonia na kuwaona Paulo na Barnaba kama miungu ya kuabudiwa. “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo
wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya
wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu,
na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji,” Mdo 14:11-12. Hakika,
tendo hili ni moja ya mambo hatari sana katika utume wetu. Ukiona hali hii
ndani mwa watu inajitokeza na kuacha kumwabudu Mungu na kuanza kukuambudu wewe
kama mchungaji wao, ujue wazi ufanyacho si matakwa ya Mungu bali shetani amechukua
mkondo wake.
Ni ukweli usiopingika
kwamba, tunastahili pongezi kwa yale tuyafanyayo na hata wakati mwingine
kuthaminiwa hasa kwa kuitambua kazi tunayoifanya. Ila mtazamo na mwelekeo huu
wa kuthaminishwa na kutambulika kwa yale tuyafanyayo usichukue kamwa nafasi ya
Kristo na Mungu. Hivyo kwa kutambua kasoro hii, Mtume Paulo na Barnaba wanatoa
angalizo kwa Walikaonia na kusema, “Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi
tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na
kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu
na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye
zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe,” Mdo
14:14-16. Hatari kubwa katika jambo hili ni kwamba, binadamu anapoukataa
ubinadamu wake, anajeuka kuwa mbaya kuliko shetani, kwani shatani alishaukubali
ushetani wake pale alipomwasi Mungu.
Ndugu yangu, kuukubali
ubinadamu wetu ni pamoja na kujitambua na kuzishika amri za Mungu kwani twataka
kuongozwa na Mungu na kuwa watoto wa Mungu. Hivyo Yesu anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye
anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na
kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Nani asiyependa kutambuliwa na Mungu? Embu
fikiri yote uyafanyayo leo kadiri ya wito wako mwisho wa siku yanakosa kibali
mbele ya Mungu. Kumpenda Mungu ni kushika amri zake. Kristo kesha tuambia ni
amri ipi iliyo kubwa kuliko zote. Je, neno UPENDO ni geni kwako? Yesu anasema,
“Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo
langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24. Hata Bwana wetu Yesu Kristo
alipokuwa hapa duniani hakujifanyia mambo yake kadiri atakavyo. Alikuwa makini
sana kutimiza mapenzi ya yule alimpeleka yaani Mungu Baba. Swali la kujiuliza
mara zote ni hili, je, hapa nilipo na kadiri ya maagano yangu kimaisha
ninayafanya mapenzi ya Mungu? Kama jibu ni hapana, Je, nimejiandaaje kujibu
swali hili siku ya mwisho?
Ndugu
yangu, mpango wa Mungu kwetu na hasa swala zima la maisha ya umilele
limeratibishwa vizuri sana. Nafasi uliyokuwa nayo leo na “mawezekano ya
kimaisha,” “life opportunities” hayapo kwa bahati mbaya kwako au upendeleo.
Yote haya yanasababu kubwa kuhusu maisha yako ya sasa na wale wanaokuzunguka,
na hatma yake, yaani, umilele. Hata
hivyo, kwa kutusaidia, Yesu Kristo anatukumbusha jambo muhimu sana ndugu zangu.
Naye anasema, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba
atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia,” Yoh 14:26. Hivi kama tumefundishwa yote na kukumbushwa yote
tunayosababu ya kushindwa mtihani ulio mbele yetu? Ni katika maana hii Yesu
anatuambia mwisho wa kiama jambo hili litatokea kwa hakika. “Ndipo kutakapokuwa
na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii
wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje,” Lk 13:28. Neno hili
“kusaga meno” limesemwa mara sita Injili ya Matayo, mara moja Injili ya Marko
na mara moja Injili ya Luka. Maana yake ni kwamba hakutakuwa na nafasi ya
kujitetea kwani nafasi ya kufanya vema ni leo na sasa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye
anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na
kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21
Tusali:-Ee Yesu, tufanye kile tulicho na tuishi kadiri ya mango wa
Mungu maishani mwetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario