ALHAMISI
WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo:
Mdo 18:1-8
Zab:
98:1, 2-3ab, 3cd-4
Injili:
Yoh 16:16-20
Nukuu:
“na kwa kuwa kazi yao
ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa
mafundi wa kushona hema,” Mdo 18:3
“Hata Sila na
Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno,
akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo,” Mdo 18:5
“Walipopingamana naye
na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu
ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa,” Mdo
18:6
“Akaondoka huko
akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye
nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi,” Mdo 18:7
“Na Krispo, mkuu wa
sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia,
waliamini, wakabatizwa,” Mdo 18:8
“Bado kitambo kidogo
nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona,” Yoh 16:16
“Yesu alifahamu
ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa
nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi
mtaniona?” Yoh 16:19
“Amin, amin,
nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20
TAFAKARI:
“Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa
watu wa Mataifa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
tunapotafakari neno hili “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi;
tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa,” inatukumbusha wosia wa Bwana wetu
Yesu Kristo kwa wanafunzi wake aliposema, “Na
mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile,
au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu,” Mt 10:14. Hiki ndicho
kilichomtokea Mtume Paulo na wenzake kule Korintho alipokataliwa na kupingwa
waziwazi aliposema ‘Yesu ni Kristo,’ yaani mpakwa mafuta na aliyetengwa au
kutwaliwa kwa kazi maalumu. Na kazi hiyo maalumu ni swala zima la ukombozi wa
mwanadamu, nikiwa mimi na wewe. Mtume Petro katika kweli hii hapindishi mafundisho
sahihi ya kile kimuhusucho Yesu. Naye anawaambia Wayahudi na sisi pia kwamba, “Yeye
(Yesu Kristo) ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa
kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna
wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya
mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:11-12.
Wayahudi hawakupenda kabisa kuupokea na hata kuusikia ukweli huu juu ya Kristo.
Je, leo sisi ni bora kuliko Wayahudi? Ndugu yangu unayesafiri nami katika
tafakari hii, tusipoyashika na kuyaishi aliyotufundisha Kristo, yaani, “Habari
Njema ya Wokovu wetu,” hatutakuwa tofauti na
Wayahudi na wale wote wampingao Kristo.
Wapendwa wana wa
Mungu, uhasili wa Yesu na kile alichokijia kimesemwa vizuri sana na Mwinjili
Yohana. Yesu Kristo ni Mungu na Mwanadamu. Kristo Yesu ni Mungu katika kweli
hii kama asemavyo Mwinjili Yohana, “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,”
Yoh 1:1,3. Yesu Kristo ni mwanadamu pia kutokana na kile alichokijia na kufanikisha,
yaani, kukukomboa wewe na mimi katika utumwa wa dhambi. Hivyo Neno hili ili
kufanikisha tendo hilo, lilimwilishwa. Naye Mwinjili Yohana anatuambia hivi: “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Kujaa huku
kwa ‘kweli na neema’ kunapita watangulizi wake wote katika historia nzima ya
wokovu wetu, licha ya nafasi na ukubwa wa yote waliyoyafanya (watangulizi wake
Yesu) katika historia hii ya wokovu wa mwanadamu.
Hivyo ndugu yangu, ni
kweli kabisa na pasipo shaka yoyote juu ya ukweli huu, kwamba, “kwa kuwa torati
ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,”
Yoh 1:17. Hiki ndicho wasichotaka kusikia Wayahudi wa nyakati zile za Yesu, na
baadhi yao hadi leo. Hiki pia ndicho wasichotaka kusikia wale wote wampingao
Kristo kwa matendo yao hadi leo. Kwa tendo hilo la kumwilishwa, na kutenda kile
alichokijia Yesu Kristo, yaani, kutupatia fursa tena ya kuwa wana wa Mungu na
warithi wa ufalme wa Mungu, kinaonyesha umasikini wa KRISTO kwetu, ambalo tokeo
lake ni UTAJIRI kwetu. Ndugu yangu, katika kweli hii, Mtume Paulo anasema maana
halisi ya tendo lile la KUMWILISHWA KWA NENO; “Maana mmejua neema ya Bwana wetu
Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri,
ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ndugu yangu,
hii ndiyo maana halisi ya Yesu Kristo ‘kutupenda upeo,’ kama atuambiavyo
Mwinjili Yohana katika saa ile ya mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo hapa duniani.
“Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali
akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba,
naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1.
Wapendwa
wana wa Mungu, Kanisa la mwanzo lilisimama imara katika kweli hii niliyokwisha
isema, na hivyo walikuwa tayari kupata karaha zote kwa sababu ya kweli hii. Mimi
na wewe tutakuwa huru, ‘kweli’ itakapotawala katika maisha yetu, Yoh 8:32.
Ukweli wa kitu kama ulivyo kamwe hautegemea namna tujionavyo, bali namna kweli
ile ilivyo na ipasavyo kuwa. Tatizo langu na wewe ni kwamba kwa asili yetu
twapenda kusikia mazuri na yale tuyapendayo tu, na yanayohusu maisha yetu.
Kweli ni mizania ya kile ulicho na kile kilicho katika umilele wake. Je, mimi
ni nani kupindisha kweli kama ilivyo? Naweza kufanya hivyo kwa wakati tu, bali
historia lazima itaniumbua kwa wakati ufahao. Huu ndio msingi wa maneno ya
Mtume Paulo kwa wale Wayahudi wa Korintho, kwamba, “damu
yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu
wa Mataifa,” Mdo 18:6b. Ndugu yangu, tenda lililo kweli, haki, na jema, na uende
zako. Shukrani ni majaliwa. Shukrani hizi zawezekana kuwepo ungali hali, au
kuwa shuhuda kwa vizazi vijavyo. Ukweli wa hili nilisemalo tunaweza kuuona
katika Injili ya leo. Yesu anawaambia Mitume wake, “Bado kitambo kidogo nanyi
hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona,” Yoh 16:16. Maneno haya
yanawachanganya sana wafuasi wake Yesu Kristo.
Ni kweli kabisa kwamba
ilimpasa Kristo kuondoka ili tuneemeke na matunda ya Roho Mtakatifu kama Mwalimu
wa kutukumbusha yale yote Kristo aliyotufundisha. ‘Na bado kitambo kidogo
tutamwona’ ikiwa ni swala la wakati tu. Jibu la maneno haya mazito ya Yesu lipo
kwenye hili alilolisema mwenyewe, kwamba: “Amin,
amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Hivyo ndugu yangu, mateso yako leo na sasa
yatokanayo na kweli ndani na katika Kristo Yesu, ni swala la wakati tu. Hakuna
uovu wowote unaoweza kudumu katika umilele wake. Umilele na mamlaka yote yapo
kwa Mungu yaani, kwa Yesu Kristo mwenyewe kama Mungu na mwanadamu, “kwa
kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi,
vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi,
au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16.
Je, bado unamashaka juu ya Kristo Yesu? Kuwa na furaha na yote ufanyayo ndani
na katika Yesu Kristo, licha ya changamoto zake. Amina.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yesu alifahamu ya kwamba wanataka
kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo
kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?” Yoh 16:19
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nipe ustahimilivu na nguvu ya kushinda pale ninapokutana na
changamoto za kuishi Ukristo wangu ndani na katika Wewe. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario