JUMANNE WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo:
Mdo 20:17-27
Zab:
68:10-11, 20-21
Injili:
Yoh 17:1-11a
Nukuu:
“Basi sasa,
angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue
mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa
Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki
vyaningoja,” Mdo 20:22-23
“Lakini siyahesabu
maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma
ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,”
Mdo 20:24
“Kwa maana sikujiepusha
na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu,” Mdo 20:27
“Na uzima wa
milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo,” Yoh
17:3
“Mimi nawaombea hao;
siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio
wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10
“Wala mimi simo tena
ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako,” Yoh 17:11a
TAFAKARI: “Uzima wa milele ndio huu; kumjua
Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu
hapa duniani kaitwa kwa namna mbalimbali na ya pekee kadiri iliyompendeza
Mungu. Kuitwa huku na Mungu kwahitaji mwitikio wetu. Hivyo kila mmoja wetu
anavyoitikia bila kujibakiza ndivyo anavyojazwa uzima huo wa milele ambao ni
tayari katika hatua, na ambao bado katika utumilifu wake. Hapa haijalishi
mwitikio huo umechukua taswira gani. Kwa maana nyingine haijalishi wewe ni
mlei, matawa, au mkleri. Hivyo basi, mwitikio huu lazima ulenge kumjua Mungu wa
pekee wa kweli, na Yesu Kristo.
Ni katika mwitikio huo kimaisha Mtume Paulo hajuutii
kumjua na kumtumikia Mungu aliye hai, na Yesu Kristo. Hivyo Mtume Paulo yupo
tayari kwa yote na lolote litakalotokea kuhusu maisha yake na uhusiano wake na
Mungu. “Basi sasa, angalieni, nashika njia
kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji
hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja,” Mdo 20:22-23. Kwa
maneno haya ya Paulo Mtume tunakumbushwa kusimama imara hasa nyakati zile za
sintofahamu katika maisha yetu kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake.
Mtume Paulo anajua wazi
maamuzi yake aliyoyachukua katika maisha msingi wake ni Kristo mwenyewe, na
hajuutii uamuzi wake huo. Siri yake ni kwamba, tunapojitoa kwake Kristo bila
kujibakiza tunauhakika wa uzima wa milele, na safari yetu kuelekea katika
utumilifu huo wa maisha ya umilele ni safari salama na yauhakika. Hivyo, “siyahesabu
maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma
ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,”
Mdo 20:24. Je, wewe na mimi tunao ujasiri huu na kuyatamka maneno mazito haya
ya uzima katikati ya kiza kinene cha sintofahamu ya maisha kama Mtume Paulo?
Kwetu kama wafuasi hai wa Kristo ni changamoto kubwa!
Wapendwa wana wa Mungu,
tufanyapo maamuzi haya katika maisha licha ya magumu tunayokumbana nayo,
tunajua mbele yetu yupo Jemedari Mkuu Yesu Kristo aliyeyashinda yote, na
asiyeshindwa kwa lolote. Mateso na magumu tunayokutakana nayo katika maisha
Kristo anayajua, na ndiye yeye atakayetutoa kwenye mikwamo hiyo kiimani endapo
tutaweka matumaini yetu yote kwake kama mweza wa vyote. Katika ukweli huu Yesu achoki
kutuombea na kutujaza neema na baraka akisema, “Mimi nawaombea hao; siuombei
ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako
ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10. Je, kwa nini Yesu hauombei
ulimwengu? Ulimwengu huu ni kama tanuru la kufulia chuma. Kupata chuma bora na
imara lazima kipite kwenye moto mkali sana. Nasi katika kuyashinda mateso haya
hapa duniani ndivyo tunavyojiimarisha katika imani na kunyakua taji ile
tuliyoandaliwa. Kwa hiyo ulimwengu kama ulivyo ni sehemu ya kukomaza Imani yetu
na kukua Kiroho na kimwili.
Ndugu yangu, Je, mateso
na maisha yako kwa ujumla yana mwelekeo huo wa uzima wa milele, yaani, kumjua
Mungu wa kweli na Yesu Kristo?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini siyahesabu maisha yangu
kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile
niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,” Mdo
20:24
Tusali:-Ee
Mungu, niwezeshe kusimama imara kiimani ili maisha yangu yalenge kukujua Wewe
Mungu wa kweli na Yesu Kristo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario