JUMANNE WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 11:19-26
Zab: 87:1b-3, 4-5, 6-7
Injili: Yoh 10:22-30
Nukuu:
“Basi
wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano,
wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa
Wayahudi peke yao,” Mdo 11:19
“Mkono
wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21
“Habari
hizo za watu hao zikafika masikioni mwa Kanisa lililokuwako katika Yerusalemu;
wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia,” Mdo 11:22
“Na wanafunzi waliitwa
Wakristo kwanza hapo Antiokia,” Mdo 11:26b
“Basi Wayahudi
walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe
Kristo, utuambie waziwazi,” Yoh 10:24
“Yesu akawajibu,
Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu
ndizo zinazonishuhudia,” Yoh 10:25.
“Lakini ninyi
hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu,” Yoh 10:26
“Kondoo wangu waisikia
sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27.
“Nami nawapa uzima wa
milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono
wangu,” Yoh 10:28
TAFAKARI:
“Matendo mema ndani ya Kristo na katika Kristo, umtambulisha Kristo pale
tulipo; wote tumeitwa kuwa wamisionari.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kutawanyika kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, kulitokana na kuhujumiwa kwa
jumuiya hiyo, na hasa kile kifo cha Shahidi Stefano. Kwa upande mwingine,
kupitia mateso haya, habari njema zinafika kila kona na wengi wanamwamini
Mungu. “Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari
ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile
neno ila kwa Wayahudi peke yao,” Mdo 11:19. Kutawanyika huku kwa jumuiya hizi
za Wakristo tukienda mbali zaidi tunaona ni kutokana na sadaka ile ya pekee
aliyoitoa Yesu pale msalabani. Ni kwa kupitia sadaka hiyo hiyo-kwa kila mmoja
wetu, Kanisa linakua na kuenea popote duniani.
Wapendwa, tunapokuwa na
Kristo katika nia na matendo yetu tunabarikiwa kwa sababu tuyafanyayo ni
mwendelezo wa kazi yake ya kuikomboa dunia. “Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao,
watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21. Hapa tunaona safari ya
uinjilishaji ndiyo inaanza, na Kanisa katika maana ya kila Mbatizwa linakuwa
Kanisa la Kimisionari. “Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa
lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia,” Mdo
11:22. Kazi hizi za kimisionari ndizo zinazolifanya Kanisa likue na kuenea kila
mahali. Kazi hizi pia ndizo zinazo watambulisha wale wazifanyazo. Ni hapa
Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi wa Yesu wanaitwa Wakristo. “Na wanafunzi
waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia,” Mdo 11:26b. Kuitwa kwao huku ni
kutokana na matendo yao kuendana na kile walichokuwa wakikiamini na kukihubiri-Yesu
Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, kufanya toba ya kweli, na kukaribia kwa Ufalme
wa Mungu.
Wapendwa katika Kristo,
mtindo huu wa kimisionari unaitajika sana nyakati zetu. Matendo mema ndani ya
Kristo na katika Kristo, umtambulisha Kristo pale tulipo; na kwa namna hiyo wote
tumeitwa kuwa wamisionari. Umisionari wa kutembea na vipasa sauti kwa sasa
hauna nafasi sana. Tunaitaji umisionari wa matendo mema kwa watu wote. Kristo
alishaanza kulifanya hili pale ambapo Wayahudi walitaka kupata uhakika kama
kweli yeye ndiye Kristo mwenyewe. “Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi
hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo
zinazonishuhudia,” Yoh 10:25. Kazi azifanyazo Yesu ndizo zinazomthibitisha. Ni
kwa namna hiyo hiyo kwamba kazi tuzifanyazo kama Wabatizwa na Kanisa kwa ujumla
wake zitamtambulisha Kristo pale tulipo.
Wapendwa, asiyesadiki
matendo hayo mema ni wazi hamsadiki hata Kristo pia. Je, tuache kutenda mema?
Jibu ni HAPANA. Tusiache kutenda mema kwa vile tu wapo watu ambao hawayaoni
mema tuyatendayo, na wala hawamsadiki Kristo. Yesu anasema, “Lakini ninyi
hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu,” Yoh 10:26. Ni Kristo
mwenyewe anayejua hatma ya wale wasiomsadiki. Kazi yetu ni kusambaza upendo wa
Kristo kila kona. Ni Kristo mwenyewe atakaye wabadilisha mioyo yao wasiomsadiki
kadiri atakavyoona yeye na wakati ufaao. Naye anasema, “Kondoo wangu waisikia
sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27. Kondoo walio mbali na sauti ya Kristo ipo siku
watavutwa karibu kwa matendo yetu mema kama wafuasi wake Kristo. Ni Kristo
mwenyewe atawapa uzima na kuwahifadhi katika mikono yake.Yesu anasema, “Nami
nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu
atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28. Mimi na wewe kama wabatizwa
tutimize vyema ahadi zetu za ubatizo.
Tumsifu Yesu Kristo.
“Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao,
watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana,” Mdo 11:21
Tusali:-Ee
Yesu Kristo na Mchungaji wetu Mwema, tujalie neema ya kutenda matendo mema kila
wakati. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario