JUMATATU WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 11:1-18
Zab: 42:2-3; 43:3, 4
Injili: Yoh 10:11-18
Nukuu:
“Basi mitume na ndugu waliokuwako katika
Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu,”
Mdo 11:1
“Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka
mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi,” Mdo 11:9
“Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu
akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo,” Mdo 11:15
“Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao
karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani
niweze kumpinga Mungu?” Mdo 11:17
“Mimi
ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,”
Yoh 10:11
“Mtu wa mshahara, wala si mchungaji,
ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na
kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya,” Yoh 10:12
“Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio
wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama
vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya
kondoo,” Yoh 10:14-15
“Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi
hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha
kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja,” Yoh 10:16
“Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi
nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena,”
Yoh 10:18a
TAFAKARI:
“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji
mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Jumuiya ya kwanza ya Wakristo inaanza kukua na kuenea maeneo tofauti tofauti
nje ya Yerusalemu. Uwezo na Nguvu hizi unatoka na kazi ya Roho Mtakatifu
Mwenyewe ambaye jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo wamemridhia. Jumuiya ile ya
Yerusalemu inapigwa mshangao kuona hata watu wa mataifa wamelipokea nano la
Mungu. “Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya
kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu,” Mdo 11:1. Ukweli ni
kwamba, kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuunganisha sote kuwa kitu kimoja mbele ya
Mungu. Namna ya maisha yetu, mwelekeo wa kijiografia, na ukabila, havina nafasi
katika Kanisa la Mungu. Sote kwa Sakramenti ya ubatizo tunafanywa wana wa
Mungu, na warithi wa Ufalme wa Mungu. Ukweli huu unafunuliwa kwa njia ya maono
kupitia Mtume Petro. “Sauti ikanijibu mara
ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi,” Mdo
11:9. Vilivyoumbwa na Mungu na kutakaswa naye si najisi. Nasi mbele za Mungu,
kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake, sote tunamastahili sawa.
Kwa mastahili haya
mbele za Mungu, hatuwezi kumwekea ukuta Roho Mtakatifu kuzitenda kazi zake.
Ukweli huu unamtokea Mtume Petro, na kusema, “Ikawa nilipoanza kunena, Roho
Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo,” Mdo 11:15. Hakuna
mwenye hati miliki ya Roho Mtakatifu, bali tunapewa haki hiyo kadiri Mungu
apendavyo kugawa karama zake, na kadiri pia ya Roho Mtakatifu huyu apendavyo. “Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile
ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga
Mungu?” Mdo 11:17
Pamoja
na nguvu hizi za Roho Mtakatifu, hatuwezi kutenganisha mahusiano haya na nafsi
nyingine katika umoja hasa ule wa kitendaji. Tunamwitaji Kristo ambaye ndiye
Mlango wa kwenda mbinguni. Kristo akiwa nafsi ya pili ya Mungu, katika utendaji
ndiye aliye mwokozi kwa kile kilichoanguka. Nafsi hii inapokuwa katika utendaji
haimaanishi kwamba kwa wakati huo nafsi nyingine hazifanyi kazi, yaani Mungu
Baba na Roho Mtakatifu. Ni vile vile Roho Mtakatifu katika utendaji,
uvitakatifuza vyote vilivyokombolewa na Kristo, na kwa namna hiyo hiyo nafsi
nyingine, yaani Mungu Baba, na Mungu Mwana hufanya kazi pamoja. Na ndiyo maana
Yesu anasema maneno haya, “Amin, amin,
nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea
penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.
Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo,” Yoh 10:1-2.
Furaha yetu ni kwamba
tunaye mchungaji mwema anayetuthamini na kutujua si tu kwa majina yetu, bali
hata mahitaji yetu. “Mimi ndimi mchungaji
mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:11.
Ameutoa uhai wake kwetu na anautoa kila mara tunapoisikia sauti yake. Kristo
hatotuacha kamwe wala kujitenga nasi yatakatopotokea majangwa kwetu tukiwa na
imani naye na katika njia pamoja naye. “Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye
kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia;
na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya,” Yoh 10:12. Yesu Kristo kwetu si mtu
wa mshahara wala mwajiriwa fulani ambaye huliwa kwa kazi yake.
Kristo kwetu ni yote na
katika yote. Anatupenda kama tulivyo na amekubali na yupo nasi muda wote ili
tufahamu upendo wake kwetu. “Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu
nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama
vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya
kondoo,” Yoh 10:14-15. Taswira ya upendo huu wa Kristo kwetu ndiyo kielelezo
cha uchungaji wake kwetu. Uchangaji huu wa Kristo haubagui wale wasiopenda
ulishaji wake. Huduma anayotoa Kristo habagui hata wale wanaompinga. Hivyo yupo
kwa ajili ya wote kwa wakati wote. Kujitenga na Kristo ni kukataa upendo wake
anaotupa bure wakati wote. Kristo analitambua jambo hilo na anasema, “Na kondoo
wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti
yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja,” Yoh 10:16.
Ni mara ngapi tunawatenga wale ambao wanapingana na mawazo yetu hata ikiwa kwa
nia nzuri?
Wapendwa, haya yote
Kristo anafanya si kwa kulazimishwa na yeyote au na nguvu yoyote ile, bali
anayafanya kwa upendo wake Mkubwa. Haoni shaka wala shida kufa kwa ajili yako. “Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa
mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena,” Yoh
10:18a. Upendo huu wa Kristo kwetu ni wapekee sana.
“Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi
nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena,”
Yoh 10:18a
Tusali:
Ee Yesu Mchungaji Mwema, tufanye wachungaji wema kila mmoja wetu kadiri ya
nafasi na wito wake.
No hay comentarios:
Publicar un comentario