IJUMAA WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo:
Mdo 25:13-21
Zab:
103:1-2, 11-12, 19-20ab
Injili:
Yoh 21:15-19
Nukuu:
“Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote
baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa
na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari
ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba
yu hai,” Mdo 25:18-19
“Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii,
nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya,”
Mdo 25:20
“Akamwambia
mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile
alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe
umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu,” Yoh 21:17
Akasema, Amin, amin,
nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda
utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine
atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh 21:18
TAFAKARI: “Lisha, Chunga, Lisha Kondoo Wangu.”
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na Mtume Petro kumkana
Yesu mara tatu, leo Petro anatambua kosa lake, analikiri kosa lake, na yupo
tayari kufuata maagizo na mfano wa Kristo kama mchungaji mwema. Petro
anaulizwa swali mara matatu, kama kumkumbusha alivyomkana Kristo na Bwana wake
mara tatu. Mtume Petro kuulizwa kwa swali hili mara ya kwanza kunabeba msingi
wa muulizo wa mara nyingine mbili zilizobaki. Yesu anamuuliza Petro, Je! Simoni
wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Neno “hawa” limebeba ujumbe mzito sana
katika maisha ya kiroho.
Kumpenda Kristo kuliko
“hawa” kwa maanisha kumpenda Yesu Kristo kuliko vitu vingine vyote. Kumpenda
Kristo kusiko fananishwa na yale tuyaonayo na hata kuyagusa. Ni kumfanya Kristo
kuwa ndiyo njia ya kweli, uzima wa kweli, na ukweli usiotia shaka katika maisha
yetu ya kila siku. Ni kutokuwa na mashaka kabisa tunapokuwa katika mikono yake.
Ni kumfanya Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako. Swali hili aliloulizwa Petro,
nasi tunaulizwa kila siku tunapoenenda katika njia yake.
Wapendwa wana wa Mungu,
jibu la Petro lilikuwa, “ndiyo Bwana, wewe wajua nakupenda.” Maneno haya
ayasemayo Mtume Petro yanamsingi wake kiimani. Mtume Petro hayatamki tu kwa
kumpendezesha Kristo, licha kwamba alimkana kuwa hamjui. Wakati Yesu
anafundisha kuhusu fumbo la mwili na damu yake kuwa ni chakula cha uzima, wengi
wa wanafunzi wake walimwacha kwa sababu fundisho lile lilikuwa gumu. Mafundisho
haya yalikuwa mzito sana. Hivyo Yesu aliwauliza wale Thenashara,
“Je!
Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Yoh 6:67.
Mitume wote walikuwa kimya kama wamepigwa ganzi vile. Ni Mtume Petro tu kwa
ujasiri wake aliweza kumjibu Kristo, tena kwa kile kilichokuwa kimeujaza moyo
wake na kusema, “Bwana! Twende kwa
nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi
tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu,” Yoh 6:68-69.
Huu ndiyo msingi wa jibu la Petro kwamba, “Ndiyo Bwana, wewe wajua nakupenda.”
Hata hivyo baada ya
kujibu kuwa anampenda Kristo, Mtume Petro anapewa majukumu ya jibu lile
alilolitoa. Mtume Petro anawajibishwa kutumika kama alivyomkiri Kristo na
kusema, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye
hai,” Mt 16:16. Maagizo ya Kristo kwa Petro ni kulisha kondoo zake, kuwalinda,
na kuwalisha. Kazi hapa ni kulisha, kulinda, na kulisha. Hii ndiyo maana ya
Jina lake ‘Petro,’ “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa
mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na
lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:18-19.
Mtume Petro anarudishiwa mamlaka yake aliyopewa na Kristo.
Wapendwa
wana wa Mungu, tendo hili la Kristo analolionyesha kwa Mtume Petro, ni tendo la
upendo wa hali ya juu, na hata sisi hasa pale tunapojenga uhusiano naye tena
baada ya kumwasi. Yesu yupo tayari kutupokea kama tulivyo ili mradi tujirudi na
kufanya toba ya kweli. Kristo hakuvunja ahadi yake aliyokwisho isema juu ya
Petro licha ya udhaifu aliyouonyesha siku ile ya kukamatwa Yesu Kristo. Tendo
hili linatukumbusha pia simulizi lile la mwana mpotevu. Upendo huu wa kibaba
ndiyo upendo wa Mungu kwetu. Mungu anasema na mtu mwovu, “Haya,
njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa
nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa
1:18. Hii ndiyo huruma ya Mungu kwetu. Mtume Petro anarudishiwa mamlaka yake na
kupewa kazi ya kulisha, kulinda, na kulisha daima kondo wake Kristo.
Wajibu huu aliopewa
Petro, nasi tumepewa kwa njia ya ubatizo wetu na kushiriki ukuhani wa Kristo
ulio wa kawaida. Hivyo twawajibika kufanya kazi hii ya kulisha kondoo zake, hasa
kwa matendo yetu mema pale tulipo. Tuwe mfano kwa matendo yetu na kuwa barua za
kusomwa na wegine. “Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu,
inajulikana na kusomwa na watu wote;
mnadhihirishwa
kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali
kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo
ni mioyo ya nyama,” 2Kor 3:2-3. Kuishi katika ukweli huu, kutatugharibu maisha
yetu kama mshumaa uwakavyo nakutoa mwanga ndivyo hivyo unavyokufa. Kwa wajibu
huu wa kuwa barua za kusomwa na wengine kwa matendo yetu mema, Yesu anamwambia
Petro, “Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga
mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na
mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh 21:18. Mtiririko wa ukweli
huu ndiyo unaomkuta Mtume Paulo anavyohukumiwa na kwenda kifungoni huko Roma.
Mwisho wa siku Mtume Petro, na Paulo waliyatoa maisha yao na kufa kifo dini
kumshuhudia Kristo. Ndugu yangu, palipo Msalaba wa Kristo ndipo ulipo Utukufu
wake. Hii ndiyo njia yetu sote kama wafuasi wake kila mmoja kadiri ya wito
wake.
Tumsifu Yesu Kristo
“Lakini utakapokuwa mzee,
utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka,” Yoh
21:18b
Tusali:-Yesu
Mwema, tufanye barua iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye
hai. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario