sábado, 20 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 6 YA PASAKA-A


JUMAPILI YA 6 YA PASAKA-A

Somo I: Mdo 8:5-8, 14-17

Zab: 66:1-3, 4-5, 6-7, 16, 20

Somo II: 1Pet 3:15-18

Injili: Yoh 14:15-21

Nukuu:

Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa,” Mdo 8:7

“wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu,” Mdo 8:14b-15

kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu,” Mdo 8:16

“Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu,” Mdo 8:17

“Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15

“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele,” Yoh 14:16

“ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu,” Yoh 14:17

“Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu,” Yoh 14:18

“Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai,” Yoh 14:19

“Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu,” Yoh 14:20

“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21

Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu,” 1Pet 3:15

“Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo,” 1Pet 3:16

“Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya,” 1Pet 3:17

“Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,” 1Pet 3:18

TAFAKARI: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya sita ya Pasaka ya mwaka “A” wa Kanisa. Leo Yesu anaweka wazi neno hili: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Upendo ndiyo msukumo hai wa maisha ya jumuiya, na sote kama wakristo. Ingawa waweza kutoa bila kupenda, huwezi kupenda ukaacha kutoa. Hali na mtazamo huu ndiyo sura halisi ya jumuiya ile ya kwanza ya wakristo.

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli pasipo shaka yoyote kwamba kila mmoja wetu kuna kitu ambacho kinaongoza na kuyasukuma maisha yake. Kitu hicho ndiyo dira na sababu ya mtu kufanya afanyavyo na kuishi aishivyo. Msukumo huo ndiyo unaotufanya kama tulivyo. Msukumo huyo ndio unaotupa furaha na matumaini kwa yale tunayoyatarajia. Msukumo huo wa maisha ndio unaotupa moyo wa kuendelea kufanya tunayoyafanya. Na kwa upande mwingine, msukumo huo wa maisha huwa sababu ya huzuni yetu ya kudumu.

Hivyo ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, Mtume Paulo anasema jambo hili kuonyesha kile kinachosukuma maisha yake. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Huu ndiyo msukumo sahihi wa maisha yetu ya ufufuko, maisha mapya na Kristo. Ni maisha ya kuutafuta ufalmwe wa Mungu kwa yale yote tuyafanyayo. Ni kumwona Kristo kwa kila unayekutana naye, ishi naye, na kuwajibika kwako kwao kadiri ya wito wako, nafasi yako, na vipaji na uwezo aliokujalia Mungu. Na jambo hili linawezekana pale tu upendo wa kweli unapotawala mioyoni mwa wanajumuiya.

Wapendwa wana wa Mungu, msukumo huu wa maisha (maisha ya ufufuko yenye kusukumwa na upendo wa kweli) ndiyo sababu ya kifo dini na shahidi cha Stefano. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo inahujumiwa na Sauli na kutawanyika. Mitume wakisukumwa na Kristo aliye sababu ya maisha yao, na Roho Mtakatifu, wanabaki Yerusalemu wakitoa ushuhuda wa Kristo hadi toni la mwisho licha ya machafuko yaliyotokea kwa sababu ya kifo cha Shahidi Stefano. Ni nguvu katika umoja wa Roho huyu Mtakatifu inafanya kazi kama Kristo alivyokwisha wahaidia kabwa ya kupaa kwake, kwamba, “nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele,” Yoh 14:16. Na huyu “ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu,” Yoh 14:17

Ndugu yangu, ni nguvu ya Roho huyu Mtakatifu waliyemwamini wa Kristo wa kwanza na Mitume, na kuongozwa naye kwamba hata “siku ile kukatukia adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao Mitume,” Mdo 8:1. Hata wale waliotawanyika kutokana na hujuma hii, hawakukoma kulitangaza na kulihubiri jina hili lililopita majina yote, Yesu Kristo Mnazareti. “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno,” Mdo 8:4. Miongoni mwa watu hawa ni Filipo.

Filipo analihubiri Jina la Yesu na wengi wanaona mwanga, kweli, na uzima kwa kuponywa na kuwa huru. “Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa,” Mdo 8:7. Haya ndiyo mambo makuu ya Mungu kwa wale wanao mwamini na kumtegemea. Haya ndiyo mambo makuu Mungu huyafanya kwa wale wasiokuwa na shaka naye na uwezo wake. Mungu huyatenda makuu hayo kwa wale wasiokatishwa tamaa na vipingamizi dhidi ya kile wanachoamini.

Wapendwa katika Kristo, ndani na katika Kristo kuna uzima na ufufuo siku ya mwisho. Maisha ya kweli na Kristo, ndiyo njia sahihi ya kuufikia umilele ambao ndiyo makusudi ya uumbaji wetu. Kazi kubwa ya Kristo ni kuhakikisha walio mridhia hawapotei hata mmoja. Ulizi ndani ya Kristo ni salama kuliko linzi nyingine zote unazoweza kufikiria. Ni ulinzi, si tu katika usalama wa miili yetu na mali zetu, ila roho zetu katika hali ya ufufuo na uzima wa milele. Naye Yesu anatuhakikishia jambo hili na kusema, “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,” Yoh 6:37.

Kristo aliyeishinda mauti na yu hai sasa ndiye huyo huyo anayetupa matumaini hai na ya kweli kwa kusema, “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu,” Yoh 14:18. Leo Kristo yupo na anakuja kwetu kila tunaposhiriki sakramenti zake pasipo hatia. Tunatiwa uzima kwa kushiriki Mwili na Damu ya Kristo pasipo na hatia, na kunaponywa majeraha yetu yaliyotokana na dhambi zetu kwa sakramenti ya kitubio.

Wewe na mimi kama wafuasi wake Kristo tu mashahidi na watoa ushuhuda wa kweli kuhusu Kristo Yesu aliye yote katika yote. Na hivyo Yesu anatuambia hivi, “Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai,” Yoh 14:19. Bila Kristo Yesu hatuwezi fanya lolote, liwe kubwa au dogo, Yoh 15:5. Ila tukiwa ndani na katika Kristo, Yeye mwenyewe anatuambia, “Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu,” Yoh 14:20. Na haya yote yatafanyika pale tu tunapopendana na kuishi upendo wa kweli kati yetu bila kubaguana. Na huku ndiko kuzishika amri zake. Naye Yesu anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21

Pamoja na hayo yote swali la kujiuliza ni hili; Ndugu yangu maisha yako umeyawekeza kwa nani? Je, kwenye utajiri wako? Je, kwa marafiki zako? Je, akili na ujanja wako? Je, katika maisha yako ya kijanja kijanja? Je, kwenye kadi zako za benk ya “life security?” Yote hayo utayaacha na kuondoka na Roho yako tu. Je, mbele ya Mungu utajitetea na nini? Njia salama ni kuwekeza kwa Kristo kupitia Benk yake-ni “ROHO YAKO.”

Ndugu yangu na Mkristo mwenzangu, pamoja na changamoto tunazokutana nazo ikiwa ni pamoja na imani yetu kama Wakristo Wakatoliki, Mtume Petro anatupa namna ya kufanya na kuishi, yaani, tuwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu,” 1Pet 3:15. Kwa maana nyingine ni wito wetu leo kutoa ushuhuda wa ukimya pale tulipo, na ushuhuda huo ubebe uhalisia wa maisha yetu kama wafuasi wake Kristo na wenye hofu ya Mungu. Katika kweli hii, Mtume Petro anasema, tuwe “…na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo,” 1Pet 3:16.

Kuongozwa na dhamiri njema ni wito vile vile wa kuona uhalisia wa jambo kama ulivyo, na siyo kama nilivyo. Tatizo kubwa la jamii yetu leo, Watanzania, tumeingiwa na woga pasipo woga, na tokeo lake ni nidhamu ya woga iliyojengeka katika mazingira ya unafiki. Tumekuwa watu wa tabasamu pasipo tabasamu, na wapiga makofi pasipo pongezi. Tumepoteza uthubutu wa kuhoji: ‘kwa nini twafanya kama tunavyofanya,’ na mwisho tumebaki kuwa kile tusicho.

Ndugu yangu, Mtume Petro anakuambia wewe na mimi kwamba, “Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya,” 1Pet 3:17. Kweli hii inatupeleka karibu kabisa na tafakari juu ya msalaba. Ingawa penye msalaba kuna utukufu, hakuna utukufu pasipo msalaba. “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,” 1Pet 3:18. Leo wengi wetu twapenda utukufu, na hata kuitwa watukufu bila msalaba. Historia ni mwalimu mzuri sana. Ni punde tu historia itatuweka mahali pake.

Ndugu yangu nikuache na changamoto hii. Maisha yetu ni changamoto kubwa sana kama ilivyo giza na mwanga. Kumbe tunapohitaji mwanga kuliondoa giza, tujifunze kutoka mshumaa. Mshumaa unaotoa mwanga kulifukuza giza, na kwa tendo hilo haliuachi mshumaa katika umbo lake. Na ndivyo ilivyo kwa wapigania haki na amani katika jamii yetu, na wale wote wanaojitoa bila kujibakiza kwa upendo. Na katika kweli hii Yesu anasema, “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. UKIPENDA UTAFANYA YOTE, Mt. Augustino wa Hippo.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya,” 1Pet 3:17

No hay comentarios:

Publicar un comentario