JUMATANO WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo:
Mdo 17:15, 22-18:1
Zab:
148:1-2, 11-12, 13, 14
Injili:
Yoh 16:12-15
Nukuu:
“Kwa sababu nilipokuwa
nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu
iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini
habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.” Mdo 17:23
“Mungu aliyeufanya
ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi,
hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala
hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa
maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote,” Mdo 17:24-25
“Basi, kwa kuwa sisi tu
wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au
jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu,” Mdo 17:29
“Kwa maana ameweka siku
atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa
watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu,” Mdo 17:31
“Basi waliposikia
habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema,
Tutakusikiliza tena katika habari hiyo,” Mdo 17:32
“Lakini yeye
atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13
“Yeye atanitukuza mimi,
kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari,” Yoh 16:14
TAFAKARI:
“Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua,”
Mdo 17:23b
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tuone kwa undani kuhusu kuabudu. Inawezekana kabisa kuabudu kwetu
hakuendani kabisa na maana halisi ya tendo hilo. Mtume Paulo katika harakati
zake za uinjilishaji anafika Athene. Mji huu ulijulikana sana kwa ukuaji wa falsafa,
na watu walitumia muda wao kutafuta ukweli kwa fikra nyakinifu. Hivyo kiufahau
walikuwa katika hali ya pekee kabisa. Mtume Paulo alipofika mahali hapa,
aliwakuta watu hawa wana hofu ya Mungu asiyejulikana. Kwa kuliona jambo hilo,
Paulo anawashukuru, na kutoa sababu ya kuwashukuru. “Kwa sababu nilipokuwa
nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu
iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini
habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. ” Mdo 17:23
Mungu huyu anayemwamini
Mtume Paulo na kumhubiri ni “Mungu
aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu
na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana
kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi
na vitu vyote,” Mdo 17:24-25. Kwa ufupi Mungu huyu anayemwamini na kumhuribi
Paulo, ahitaji kuumbwa nasi wanadamu. Hatuhitaji kumfinyanga kwa mikono yetu.
Mungu huyu haitaji kufananishwa na jambo lolote, kwani yote tuyajuayo na
kuyafikiri ndiye aliyeyafanya. Kumfananisha Mungu na kile alichokifanya, ni
kumshushia heshima yake na kumweka katika mizania ya ubinadamu wetu. Hivyo, “kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi
kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa
kwa ustadi na akili za wanadamu,” Mdo 17:29. Kumfinyanga Mungu kwa namna yeyote
ile ni kutokujua tufanyacho na kupoteza muda. Huu ndio ujumbe anaoutoa Mtume
Paulo kwa hawa watu wa Athene.
Wapendwa wana wa Mungu,
ibada ya kweli yenye kuleta furaha kwa Mungu hutokea unapojitoa kikamilifu kwa
Mungu. Kiini cha kuabudu ni kujisalimisha. Kujitoa kwa Mungu ndiyo kuabudu
hasa. Tendo hili la kujisalimisha binafsi linaitwa kwa majina mengi: Kujiweka
wakfu, Kumfanya Yesu Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, Kujitoa
kwa Roho Mtakatifu. Jambo muhimu hapa ni kwamba ulitende, siyo linaitwaje.
Mungu anapenda maisha yako-yote. Asilimia tisini na tano haitoshi. Kuna vizuizi
vitatu ambavyo huzuia kujisalimisha kwetu kikamilifu kwa Mungu: Hatuelewi kiasi
gani Mungu anatupenda, Tunataka kutawala maisha yetu wenyewe, na Tunashindwa
kuelewa maana ya kujisalimisha.
Kujisalimisha
kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa
binadamu hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo
uliyo nayo. Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au
kuteseka ili kubadilisha yanayohitajika kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita
watu waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa
uoga au mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu
wawe kama mitambo (robots) ili kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu
wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha huutia nguvu. C. S Lewis
alisema, “kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi
wenyewe-kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu
wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa…. Ni pale ninapomgeukia
Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu
halisi.”
Kujisalimisha
kunadhihirika vyema katika kutii. Unasema ‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote
anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu
Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata
samaki, Simioni alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena”
“Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na hatujakamata samaki yeyote.
Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini.” Lk.5:5. Watu waliojisalimisha
hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.
Kila
mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama sio kwa Mungu,
utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa, chuki, hofu, au
kwa kiburi chako au tama mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa kumwabudu Mungu-na kama
utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine (sanamu) ili uvipe maisha yako.
Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako, lakini huko huru na matokeo ya
uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama hutajisalimisha kwa Kristo,
utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si njia bora ya kuishi; ni njia pekee
ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza
kwenye kukukatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita
kujisalimisha “huduma yenu yenye maana,” Rum. 12:1. Tafsiri nyingine inasema,
njia yenye maana zaidi ya kumtumikia,” Rum 12:1. Kusalimisha maisha yako si
hisia za kipumbavu lakini ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya
kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Paulo alisema, “Ni lengo letu kwamba
tumpendeze yeye”.2Kor 5:9 Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema
ndiyo kwa Mungu.
Wakati
mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua kwamba kizuizi kikubwa kwa
Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni wewe mwenyewe-matakwa yako
binafsi, kiburi cha hali ya juu, na matarajio yako. Huwezi kutimiza lengo la
Mungu kwa maisha yako huku ukikazania
malengo yako binafsi.
Kama
Mungu ataenda kufanya kazi ya kina ndani yako, itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote
Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo yako ya sasa, matarajio yako ya
mbele, hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia, maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo.
Mweke Yesu katika kiti cha dereva wa maisha yako na uondoe mikono yako toka
kwenye usukani. Usiogope; hakuna chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza
dira. Chini ya uongozi wa Kristo unaweza kudumu chochote. Utakuwa kama Paulo, “Niko
tayari kwa lolote na kuwa sawa na chochote kwa njia ya yeye anayetia nguvu
ndani yangu, yaani, ninajitosheleza katika utoshelvu wa Kristo,” Flp 4:13
Kwa kutotambua ukweli
huu hakutuondolea hukumu ya mwisho. Ufahamu tuliopewa wa kujua mema na mabaya,
ndipo kulipokuwa na hukumu yako. Pamoja na ukweli huu, Mungu amekwisha tupatia
hakimu wetu, yaani Mwanaye Yesu Kristo ambaye katuambia yote yanayohusu ufalme
wake. Yesu Kristo ni sawa na Sheria iliyokwishwa tungwa na kupitishwa kwa
kupigiwa sahihi na Rais. Mungu ndiye aliyethibitisha jambo hili pale mlimani
alipojeuka sura kwa kusema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,” Lk
9:35. Hivyo, Yesu Kristo ndiye hakimu wetu wa haki. “Kwa
maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule
aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika
wafu,” Mdo 17:31. Jambo hili la ufufuko linakuwa tatizo kwa watu hawa wa Athene
na hivyo hawapo tayari kumsikiliza Paulo. “Basi waliposikia habari za ufufuo wa
wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika
habari hiyo,” Mdo 17:32.
Hata pamoja na
kutoeleweka huku wa Mtume Paulo, haikuwa sababu ya yeye kukata tamaa. Katika
utume wetu mara nyingi tunakutana na hali kama hii. Kristo anatukumbusha jambo
la muhimu sana. Hatupaswi kujisikia wapweke, ila tunaye Roho Mtakatifu ambaye
anatufunulia hayo yote yaliyojificha na kutuongoza katika kweli yote. “Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13. Uwepo wa Roho Mtakatifu humtukuza Mwana na
kuyanena yote ambaye mwana anataka kuyanena na kuyafanya. “Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika
yaliyo yangu na kuwapasha habari,” Yoh 16:14. Tunaye msaidizi wa kweli
atakayetufunulia yaliyo ya kweli. Hakuna sababu ya kuwa na hofu tunapokutana na
sintofahamu katika utume wetu, na hata katika maisha kama kweli tunamwamini
Mwana wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa
atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari,” Yoh 16:14
Tusali:-Naam
najisalimisha kwako Ee Yesu Mwema. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario