JUMATATU WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo:
Mdo 16:11-15
Zab:
149: 1b-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Yoh 15:26-16:4
Nukuu:
“Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi
ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake
ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo,” Mdo 16:14
“Hata
alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona
kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha,” Mdo
16:15
“Lakini
ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye
kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26
“Watawatenga na
masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea
Mungu ibada,” Yoh 16:2.
“Lakini nimewaambia
hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia
hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi,” Yoh 16:4
TAFAKARI:
“Uwepo wako kama Mkristo hai ni kutangaza vita dhidi ya uovu na shetani.”
Wapendwa wana wa Mungu,
jana yaani Dominika ya sita ya Pasaka tumeanza wiki ya sita ya Pasaka, na baada
ya Dominika ya Kupaa kwake Bwana wetu Yesu Kristo, tutasherekea Sikukuu ya
Pentekoste. Ni tukio kubwa sana Kikanisa tunapompokea Roho Mtakatifu
tuliyeahidiwa na Bwana wetu Yesu Kristo. Pamoja na Karama zake na Mapawa yake
katika Kanisa, Roho Mtakatifu hufanya kazi kubwa sana ya kutufanya kitu kimoja
ndani na katika Kristo. Sifa mojawapo kubwa ya Roho Mtakatifu ni kutufanya
wamoja, ikiwa ndiyo sala kuu ya Yesu Kristo kabla ya mateso na kifo chake,
aliposali, “Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe
katika kweli. Wala si hao tu
ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo
ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate
kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami
utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja,”
Yoh 17:19-22. Bila umoja huu, na mwongozo wa Roho Mtakatifu, maisha yetu kama
Wakristo yapo hatarini kabisa. Hivyo, leo natulitafakari neno hili, “Uwepo wetu
kama Wakristo hai ni kutangaza vita dhidi ya uovu na shetani.” Vita hivi
vinaushindi pale tu tunapoishi na Kristo na kuongozwa na Roho Mtakatifu ambaye
anatufunulia yote tusiyoyajua bado na kutufundisha njia sahihi ya kufuata.
Roho huyu Mtakatifu
tunapewa pale tunapoyapokea Sakramenti yake Matakatifu, naye hutujaza neema na
kutufanya kuwa wapya. Haya yote hufanyika kwetu si kwa juhudi zetu, wala kazi
zetu, bali kwa mastahili yake Mungu mwenyewe. Hivyo, “si kwa sababu ya matendo
ya haki tuliyotenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa
pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia
ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate
kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.” Tit 3:5-7.
Ni roho huyu kwa namna
ya pekee huwaongoza walioridhiwa naye kuisha maisha yanayompendeza Mungu kama
ilivyotokea kwa mwanamke yule, Lidia wa Filipi. Na mambo yalikuwa hivi, “Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi
ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake
ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo,” Mdo 16:14. Mtume
Paulo alitumika vizuri kwa jumuiya hii iliyoko Filipi, na hivyo anaacha kitu
cha kuigwa. Ukweli ni kwamba, tunapoisha hapa duniani mwisho wa siku ya maisha
yetu moja ya mambo haya mawili lazima litokee; kuwa MUHENGA au LIHOKA! Muhenga
ni mtu yule anayeacha kitu cha kuigwa na wengine baada ya maisha yake, kama
mchango katika jamii hiyo aliyoisha na kutoa maisha yake kama ushuhuda wa
kiroho ma kimaadili. Lihoka ni mtu yule ambaye hakuacha chochote kama somo la
kuigwa, na watu kujifunza kiroho na kimaadili. Hivyo mtu huyu anakuwa roho
mbaya/ovu kwa jamii ile aliyoiacha, “bad spirit!” Kwa ushuhuda huu wa Mtume
Paulo uko Filipi, anabakia kuwa Muhenga. Ndugu yangu, jambo hili linasema nini
kuhusu utume wako na wito wako hapo ulipo?
Wapendwa,
nimeanza kwa kusema moja ya kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ni kutufanya wamoja.
Hivyo Roho huyu hakumpendelea tu Lidia kufanya kama alivyofanya baada ya
kumpokea kupitia Sakramenti ya ubatizo, ila nyumba yake yote walijazwa neema ya
Mungu, na kuishi katika hofu hiyo ya Mungu, na kuleta taswiri nzima ya uwepo wa
Roho Mtakatifu. Hivyo, “Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake,
akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani
mwangu mkakae. Akatushurutisha,” Mdo 16:15. Shurutisho hili wanalopata Mtume
Paulo na mwenzake Barnaba, ni shurutisho la upendo uliotukuka. Yeyote
anayeongozwa na Roho wa Bwana hakwishi kuwa na upendo wa kujitoa kwa wengine.
Roho huyu huwa sehemu ya kwanza katika kuanzisha joto hilo la upendo kwa
jirani, Roho huyu humwezesha mtu husika kujitoa bila kujibakiza, na mwisho Roho
huyu humfanya mtu huyo kuwa na huruma.
Hakika
kwa matendo haya ya Roho Mtakatifu kwa Mkristo ni sababu tosha ya kuwa na vita
vya kudumu dhidi ya uovu, na hasa yule mwovu shetani. Katika hili Yesu
anatuambia, “Watawatenga na
masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea
Mungu ibada,” Yoh 16:2. Matendo hayo mema yafanywayo kwa nguvu ya Roho
Mtakatifu kwetu, ni Ibada tosha ya Mungu, kwani Mungu ni MWEMA. Hivyo mwovu
shetani katika uovu wake, hatafurahiwa na jambo hili. Hata katika hali hii Yesu
anatutumia Msaidizi wa kutufanya kubaki katika upendo na wema huu wa Kimungu. “Lakini
ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli
atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26. Roho huyu licha ya
kutushuhudia kweli ya Kristo katika maisha yetu, anatufunulia yale yaliyo nje
ya uwezo wetu wa Kibinadamu. Hivyo tendo hili linamfanya Mungu wetu kuitwa
Mungu, na Waajabu muda wote kwa wale wenye hofu juu yake.
Wapendwa wana wa Mungu,
Yesu anatuambia haya yote ili itakapofika saa ile, yaani wakati ule wa kujaribiwa
kwetu, na wakati ule wa kuutoa ushuhuda wetu mbele ya watu juu ya Kristo, tujue
kwamba hatupo wenyewe, bali yupo nasi na haachi kutupigania. Hivyo, “nimewaambia
hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.
Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi,” Yoh 16:4.
Hali hii inatukumbusha msimamo wetu kiimani hasa pale tunapokumbana na
sintofahamu kwenye maisha yetu. Mkristo aliyeiva katika imani hii, mara zote
Mganga yake Mkuu ni Kristo. Ndugu yangu, mara ngapi umemsaliti mganga huyu Mkuu
Yesu Kristo na kwenda kwa akina “nsonganzingwe”? Embu tazama kifua chako, kiuno
chako, shingo yako, paja lako la uso na sehemu nyingine ujuazo zilivyo chanjwa
na kukufanya kama umevaa mkanda wa Rambo! Usicheke! “Jesus is the master key.” Mrushusu naye
atatenda. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini
ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli
atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26
Tusali:-Ee Yesu, usinitoe katika kweli hii; wewe tu baki kwangu kuwa Njia, Kweli
na Uzima. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario