sábado, 13 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 5 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 5 YA PASAKA-A

Somo I: Mdo 6:1-7

Zab: 33:1-2, 4-5, 18-19

Somo II: 1Pet 2:4-9

Injili: Yoh 14:1-12

Nukuu:

“Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2

“Ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao,”Mdo 6:6.

Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi,” Yoh 14:1.

Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo,” Yoh 14:3.

“Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima,” 1Pet 2:4.

“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu,” 1Pet 2:9.

TAFAKARI: “Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya Pasaka ya Mwaka “A” wa Kanisa. Jumuiya ya kwanza ya wakristo kadiri ya somo la kwanza leo, wanaingiwa hofu kutokana na jumuiya hiyo kuongezeka, na huduma kutokwenda sawa. “Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2. Hivyo wanaona ipo hatari ya kuacha kulihubiri neno wakabaki kutatua matatizo yanayotokana na manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.

Jumuiya hii kwa kuongozwa na nguvu ya Kimaadili, Unyenyekevu, na Roho Mtakatifu, wanakabiliana na hofu hii kwa kufanya uteuzi wa watu saba “Mashemasi,” kutatua tatizo hilo. Mitume wanatoa agizo na vigezo vya kuwachagua wasaidizi hao na kusema, “basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno,” Mdo 6:3-4.

Baada ya vigenzo na masharti kuzingatiwa, wateule hawa wanawekwa wakfu kwa tendo “ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao,” Mdo 6:6. Tendo hili linamsisitizo wa umoja wa Mitume ambao leo tungesema umoja wa maaskofu, “Collegiality of Bishops.” Umoja huu ni muhimu sana leo katika Kanisa letu. Tunapoona mmoja katika kundi hili akitamka yake kama anavyojisikia, ni wazi taasisi hii muhimu na fundishi inaingiliwa. Tulio wengi tunajiuliza, hilo alinenalo kalitoa wapi, na kwa baraka ya nani? Na kama jambo hilo asemalo linaukweli, Je, ni kwa manufaa ya nani?

Wapendwa wana wa Mungu, ingawa upo uwezekano wa mtu yeyote kuupata wokovu na kuifikia Mbingu kutokana na msukumo wa maisha yake yenye kuongozwa na dhamiri yake njema na hofu ya Mungu hata kama hakuwahi kusikia habari njema za Kristo Yesu, wewe na mimi tuyeunganishwa na Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo, Kristo hubaki kuwa njia, kweli, na uzima katika usahihi wake. Kwa wale ambao bado hawajafikiwa na habari njema ya wokovu ila wanaishi kwa dhamiri zao njema, Kanisa kupitia Mamlaka yake fundishi-Magisterium, linasema hivi juu ya wokovu wao; -Mafundisho ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 847 inafundisha juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale wasiomjua Kristo ndiyo ponya yao.

Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa leo, “Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na Matumaini,” inaelezea ukweli huu kama ifuatavyo; “Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,” (no. 22)

Pamoja na ukweli huo, ikiwa wewe na mimi tumeunganishwa na Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo na kuwa warithi wa ufalme wa mbinguni, yatupasa kuishi ndani na katika Kristo. Hivyo ni wajibu wangu leo na daima kumjua Kristo, kumpenda, kumtumikia–(kupitia wote wale walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27), na mwisho ni Yeye tu atakaye nihesabia haki mbele ya kiti chake cha uzima wa milele mbinguni. Masomo yetu ya leo yamefafanua kwa undani kweli hii.

Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa wewe ni mfuasi wa Kristo na Mungu aliye hai, katika maana ya kuziishi vyema na kwa uaminifu ahadi zako za ubatizo, yakupasa kuelewa ukweli huu juu ya Kristo Yesu. Ukweli ni kwamba, bila Kristo hatuwezi kufanya lo lote, liwe dogo au kubwa. Kama Kristo ni Mzabibu nasi tu matawi yake, twawezaje basi kushamiri na kupata uhai pasipo shina lenyewe? Kitendawili hiki kinateguliwa na Kristo mwenyewe. Naye anasema, Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5.

Ndugu yangu na Mbatizwa mwenzangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kwa weledi wako na yote uliyonayo, Je, waweza kutoboa mbingu bila Kristo Yesu? Na kama vile haitoshi, Yesu anaenda mbali zaidi na kujifananisha yeye na Mlango. Ndugu yangu na Mbatizwa mwenzangu, Kristo tu ndiye Mlango wa kufikia huo upande wa pili, yaani, Mbingu. Naye Yesu anatuambia hivi, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho,” Yoh 10:7, 9. Upekee wa Kristo kama ndiyo Mlango sahihi umebebwa na maneno haya mazito ya Yesu. Naye anasema hivi, “Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia,” Yoh 10:8.

Maana yake ni kwamba, kama hapo-“wakati fulani” iliwezekana wachache kwa ujanja ujanja wao kupita, au waliojitangazia na hata kujiinua kwamba wao ni “milango,” hawakuwa sahihi, na hata leo kama wapo si milango au mlango sahihi. Habari Njema kwa sasa ni kwamba Yeye mwenyewe-Yesu Kristo ndiyo HABARI NJEMA HIYO, na ndiyo MLANGO SAHIHI na wa KWELI.

Mpendwa katika Kristo, hapana shaka yoyote kwamba msukumo wa maisha ya Mtume Paulo ulipata msingi imara katika fundisho hili la Mtume Petro, kwamba “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo-Yesu Kristo,” Mdo 4:12. Ufahamu huu ndio, yaani, ‘Kristo ndiye kila kitu katika maisha yetu,’ ndio unaotupeleka kuyafahamu maneno ya Yesu katika Injili ya leo. Naye Yesu anasema, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Yesu Kristo ni njia kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua Yesu ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukulia kindugu katika misalaba ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu tunakutana naye Kristo katika hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii tunakutana nayo katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi wa neno.

Na Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:56.

Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa kupitia Sakramenti ya kitubio tunapatanishwa tena na Kristo kutoka katika hatia zote. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18. Hakuna sababu ya kufa moyo pale ambapo mambo huenda ndivyo sivyo. Mungu aliye Upendo na Huruma uanza upya nasi pale tunapokuwa tayari kufanya hivyo. Hivyo ndani na katika Kristo hakuna sababu ya kuwa na hofu. Tumwamini Kristo na tuziamini kazi zake na hasa kupitia Masakramenti yake. “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi,” Yoh 14:1.

Ndani na Katika Kristo kunautulivu wa kweli, naye kesha tuandalia makao ya milele. Duniani hapa ndugu yangu tunapita tu. Ulimwenguni hapa ni sehemu ya maandalizi ya huo umilele. Mbinguni ndipo kwenye nafasi ya kila mmoja wetu, na ndiyo makao ya milele. “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali,” Yoh 14:2. Lengo la Kristo ni kumpata kila mmoja wetu. Hili ndilo pia lengo msingi la Kanisa. Lilipo Kanisa katika maana ya Mwili wa Kristo nasi tukiwa viungo hai vyake, Kanisa huwa Sakramenti ya Wokovu kwa sababu Kristo yu hai mahali hapo.Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo,” Yoh 14:3. Ndungu yangu, je, hu kiungo hai cha mwili wa Kristo, yaani Kanisa?

Wapendwa wana wa Mungu, msingi wa haya yote tunayoyaona kutoka jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo yanatokana na msingi wa imani waliyokuwa nayo juu ya Yesu Kristo na yale aliyoyafundisha. Ni ukweli usiotia shaka kwamba jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo waliamini barabara yule wamfuatao na kumshuhudia mbele za watu. Mtume Filipo anapomwuliza Yesu tuonyeshe Baba nayo yatosha kumwamini, Yesu anamjibu na kusema, “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Kristo anafumbua ukweli wa kumwilishwa kwake, si tu kwa Filipo, hata kwetu pia. Kumwilishwa huku kwa Yesu Kristo ni ukweli wa Mungu mwenyewe katika fumbo na umbo hili la kibidamu kama sisi ila utofauti wake ni kwamba hakutenda dhambi kama mwanadamu. Yesu Kristo anakazia ukweli huu na kusema, “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh 14:10b. Ufunuo huu wa Mungu kupitia Yesu Kristo ni wa wazi na wakati mwingine wakujificha. Ila hapana shaka hata kidogo kwa umungu wa Kristo kunakojieleza kwa yale aliyoyafanya yaani kazi zake.

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo analifumbua jambo hili pale tunapokuwa na shaka juu yake kwa kusema, “La! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11b. Imani ya kweli juu ya Kristo ndiyo inayotufanya kuishi na kutenda kama alivyofanya Yesu Kristo. Ukweli huu anausema Kristo mwenyewe, na wale wote waliouishi ukweli huu, Kristo amefanya makuu kupitia kwao kwa mkono wake. “Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Matendo makuu hufanyika kwa mtu huyu aaminiye juu ya Kristo si kwa faida yake binafsi, ila kwa kupitia mtu huyu Mungu anatukuzwe na kuabudiwa milele ndani ya Yesu Kristo mwanaye. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13. Je, ndugu yangu, hupendi kuwa sababu ya utukufu huu wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo?

Wapendwa, jibu la swali hili ndilo kiini cha Imani yetu, na maisha yetu kama Wakristo na Wafuasi wa Kristo leo katika dunia hii tunayoishi: “KUWA SABABU YA UTUKUFU WA MUNGU KUPITIA MWANAYE YESU KRISTO, na si vinginevyo.

Ndugu yangu, unapopata kuona njia kwa macho ya kiroho ni sawa na kuzaliwa upya. Ni kushibishwa nuru ile iangazayo katika kweli halisi. Ni msukumo wa neema ndani yako unaoangaza na kuyaona yale yaliyo juu ya uwezo wako kiakili kama wanadamu. Neema ya Mungu ndani na kwa njia yake Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, utuwezesha na kutuongoza kuyafikia yale Mungu anayotamani sote siku moja kuyafikia. Hivyo ndugu yangu, “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima,” 1Pet 2:4. Jiwe hili ndilo Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai.

Kwa Sakramenti ya Ubatizo miili yetu inakuwa Hekalu la Roho Mtakatifu, na viungo wa Kristo kama Kanisa. Kwa Sakramenti ya Ubatizo tunashirikishwa ukuhani wa kawaida wa Yesu Kristo.Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo,” 1Pet 2:5. Licha ya kuwa makuhani wa kawaida wa Kristo, kwa Sakramenti ya Ubatizo, tu wa milki ya Mungu katika nuru ya ajabu-wana wa Mungu aliye Mtakatifu.Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu,” 1Pet 2:9. Tu wana wa nuru na kwa sababu hiyo ndicho alichokijia Yesu. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46.

Ndugu yangu, bila shaka ulishakutana na mdudu huyu (kwa Kichaga hujulikana kama-“Kirombocho”). Mdudu huyu husukuma kinyesi cha ng’ombe kwa kutumia miguu yake ya nyuma kutwa kuchwa, kila siku. Hufanya kazi hii kwa bidii kubwa sana, na hasa pale anapokisukuma kinyesi hiki kuelekea mlimani.

Jambo la kushangaza mara afikapo kileleni, kwake siyo mwisho wa kazi, safari, wala pumziko. Kinyesi hiki huweza kumponyoka na kuporomoka tena hadi chini kabisa, mwanzoni, pale alipoianza safari, na kazi huanza tena.

Kwa mwono wa kujishughulisha kama sera, mdudu huyu anaitendea haki. Ila kwa upande wa “maisha yenye kuongozwa na malengo,” mdudu huyu yupo nje ya sera.

Bila shaka wewe na mimi tusipo ishi maisha yenye ‘kuongozwa na malengo,’ na Kristo akiwa kielelezo chetu kama ‘Njia, Kweli, na Uzima,’ tutaishia kuwa kama mdudu huyu “Kirombocho.”

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima,” 1Pet 2:4.

Tusali: Ee Yesu, tuongoze kuishi maisha yenye malengo na mwisho tuufikie ule uzima wa milele.

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario