JUMAMOSI WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 16:1-10
Zab: 100:1b-2, 3, 5
Injili: Yoh 15:18-21
Nukuu:
“Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na
mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini;
lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1
“Paulo akamtaka huyo afuatane naye,
akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana
wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani,” Mdo 16:3
“Basi walipokuwa wakipita kati ya
miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko
Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo 16:4
“Makanisa yakatiwa nguvu katika ile
Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5
“Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa
umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18
“Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda
walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua
katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19
“Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu,
kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21
TAFAKARI: “Iwapo
ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia
ninyi,” Yoh 15:18
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo kwa namna ya
pekee tutafakari changamoto za uinjilishaji za Kanisa la mwanzo na changamoto
tunazokumbana nazo leo katika utume wetu kama wabatizwa na wahudumu katika
Kanisa. Bila shaka wiki nzima hii tumekuwa tukitafakari changamoto hizi na
hatua waliyochukuwa Mitume kukabiliana nazo, hasa kwa kuitisha Mtaguso ule wa
Yerusalemu.
Matokea ya Mtaguso huu ulikuwa: “Wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu,
na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29.
Hata hivyo Kanisa bado linakumbana na changamoto za mila na desturi za
Kiyahudi. Hivyo ili Timotheo afuatane na Mtume Paulo, inampasa kutahiriwa. “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo
palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi
aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1. Je kwa tendo hili Paulo atakuwa ameenda kinyume
na maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu?
Ndugu yangu
tunayesafiri wote katika tafakari hii, ni vyema tuelewe jambo hili. Licha ya
kwamba Kanisa ni la kiulimwengu, na hili limethibitishwa katika mitaguso
mbalimbali, maamuzi ya mitaguso hiyo hayaondoi upekee wa changamoto ya Kanisa
mahalia, mfano Kanisa la Tanzania. Hapa ndipo tunapozungumzia busara za
kichungaji kuenenda na mazingira husika bila kuwakwaza watu. Hivyo, tukio hili la
kutahiriwa kwa Timotheo linaendana na mazingira maalumu bila kuwakwaza watu,
ili kuweza kupenyeza ujumbe ule waliokuwa wameubeba au kusudiwa, na hapa ikiwa
ni maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu.
Mtume Paulo anatupa
sababu ya kufanya hivyo ikiwa ndiyo busara ya kichungaji. “Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa
ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye
ni Myunani,” Mdo 16:3. Je, Paulo alilifanya jambo hili kutowakwaza Wayahudi?
Bila shaka Paulo analifanya jambo hili kwa malengo hayo, kama anavyosema
Kristo, “Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo
hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia
lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa
wadogo hawa,” Lk 17:1-2. Ni vizuri kutowakwaza wale tunaotaka waufahamu ukweli
wa Mungu. Kwa upande wa kichunguaji, ni rahisi sana kumhubiri Kristo kwa kwale
wasiomjua bado, kuliko kuwarudisha wale waliokatishwa tamaa hasa pale
tunapowakwaza.
Kwa
mambo yale ambayo hayaendi kinyume na imani yetu, yanapotokea bila kujua au
kujiandaa, ni vyema tukayapa muda ili tuyaelewe na kutumia mbinu ya kuwaelimisha
wale wayafanyayo, hasa tukilenga katika kutaka kujua ‘kwa nini wanafanya kama
wanavyofanya.’ Hivyo kwa kulitambua jambo hilo, inakuwa rahisi kufikisha ujumbe
ule uliokusudiwa. “Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile
amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo
16:4. Mambo haya huwa tunakutana nayo mara nyingi hasa pale tunapoanza utume
mpya katika mazingira mageni kinyume na mila na desturi zetu tulizokulia na kuzizoea.
Jambo la msingi ni kushikilia mafundisho sahihi ya Kanisa (katika kuyafundisha
kwa lugha nyepesi na mifano hai ili yaeleweke kwa waamini) na yenye mwelekeo wa
wokovu, na maisha ya umilele.
Ni
dhahiri kwa Kanisa la mwanzo mengi yalifundishwa na yenye kuleta umoja kindugu
na Kikanisa kwa ujula wake, ila haya manne yapo wazi, ususani tendo la
kutahiriwa kuonekana kama kigezo cha kuchangamana pamoja; Kwanza, mafundisho
yalisisitiza kuzishika amri za Mungu. “Kutahiriwa si kitu, na
kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu,” 1Kor 7:19.
Pili, kuishi maisha ya
Ufufuko ndani na Katika Kristo Yesu, na hapa yakilenga haswa mila na desturi
zetu zilizopotofu na zisizo na mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Msalaba
wa Kristo ndiyo kielelezo cha huo Utukufu wenyewe. “ Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa,
bali kiumbe kipya,” Gal 6:14-15. Hapa tunakumbushwa pia hakuna Utukufu pasipo
Msalaba kwa ye yote yule aliye mfusi mwaminifu wa Yesu Kristo.
Tatu, mafundisho ya
Kanisa la mwanzo yalijikita kwenye kweli ya kuwa yote katika yote na Kristo
Yesu. Kujitoa bila kujibakiza katika hali ya kusahau tofauti zetu zisizo na
mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Hivyo “hapo hapana Myunani wala
Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala
mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3.11.
Nne, yote yapo kama
yalivyo kwa neema ya Mungu. Hakuna kati yetu mwenye kujihesabia haki mwenyewe.
Zipo sehemu nyingi katika Maandiko Matakatifu, na hasa Agano Jipya
zinazoonyesha kweli hii. Hivyo ndugu yangu, “kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda
wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si
kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa
kwenu ninyi,” 2Kor 1.12
Hivyo
wapendwa wana wa Mungu, wewe na mimi yatupasa kujua kweli hii, kwamba, utamaduni
wa mahali fulani ni sehemu ya Maisha yao, na hivyo ni Utakatifu wao. Kwa maana
hiyo, tuwapo katika mazingira hayo ni kufanya kama alivyoambiwa Musa na Mungu,
“Bwana
alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile
kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu
vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut
3:4-5. Yatupasa kuvivua viatu vyetu, ili kujua utakatifu wa mahali pale. Yatupana
kuwa tayari kuona upya na watu wa mahali pale ili kujua ukweli halisi ya maisha
yao. Uinjilishaji wetu na umisionari kwa ujumla wake unapokosa dhana hii ya
kuona upya yale tunayokutana nayo, ukiambatana na upole wa kujifunza, mwisho wa
siku tunaishia kutokuwaelewa watu husika na kuwa na sintofahamu kubwa. Mtihani
huu Mtume Paulo anaufaulu vizuri, na matokea yake ni kwamba, “Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao
ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5. Ukiona kila
unayekutana naye anakukimbia ujue kunatatizo kubwa katika mahusiano yako na
wale unaokutana nao. Kabla ya kumtafuta mchawi, zama kwanza ndani yako na
jipekue vizuri namna yako ya kufanya mambo, na namna ya kufikisha kwao kile
ulichotarajia-ujumbe.
Wakati mwingine
yawezekana kabisa ukakumbana na pingamizi kubwa kutokana na mazoea yao ambayo
yamekuwa sehemu ya tabia yao. Unapotenda jambo jema kwa watu na mapokeo yake
yakawa mabaya, wala usikate tamaa. Tumia njia njingine ili ujumbe ule ule
uwafike vyema. Na zaidi ya hayo Yesu anatuimarisha kwa kutupa moyo na kusema, “Iwapo
ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia
ninyi,” Yoh 15:18. Kama ulimwengu huo ulishamchukia yule kwa wakati huu
unayemtumikia, hakika huyo huyo ndiye atakaye kupa njia na namna ya kufanya
pale ukutanapo na mkwamo. Yesu anasema hivi kuhusu hali hii mara inapotoka: “Na
watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini
lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho
Mtakatifu,” Mk 13:11. Kwa vile ujumbe uusemao na kuusimamia si wetu binafsi,
kwa wakati huo Roho Mtakatifu atatusaidia kuyasema yale yatupasaya kuyasema kwa
sifa na utukufu wa Mungu.
Ukweli ni kwamba yeyote
anayekuwa ndani na katika Kristo, ujitenga na mwelekeo na mtazama wa yale
tunayoyaishi na kukutana nayo kila siku. Mtu huyu huyaona mambo yote katika
mtazamo mwingine. Unapokuwa na maisha yenye malengo, na hasa maisha katika
ufuasi wa Kristo, utayaona yote katika umilele. Kukiona kitu katika umilele
wake, ukweli huu hupingana na dhana ya leo na sasa. Tupo katika ulimwengu wa
‘ponda mali kifo chaja.’ Hivyo Yesu Kristo anatuambia kuhusu ukweli huu,
kwamba, “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini
kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa
sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19. Hufanyapo kila kitu na kupigiwa
makofu, jaribu kuchunguza makofi hayo. Wakati mwingine makofi hayo huashiria
kejeri.
Mwisho tuwe tayari
kutendwa vibaya kama Kristo alivyotendwa kwa sababu watesi hawa hawamjua yule
aliyempeleka Kristo. “Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa
kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21. Tusisahau pia matatizo na magumu
katika utume wetu, yanatufanya kukua na kukomaa kiroho.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini haya yote watawatenda kwa
ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21
No hay comentarios:
Publicar un comentario