viernes, 5 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA PASAKA-A


JUMAPILI YA 4 YA PASAKA-A



JUMAPILI YA 4 YA PASAKA-A

Somo I: Mdo 2:14a, 36-41

Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6

Somo II: 1Pet 2:20b-25

Injili: Yoh 10:1-10

Nukuu:

Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38.

“Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie,”  Mdo 2: 39.

Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40.

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo,” Yoh 10:1-2

Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho,”Yoh 10:9

“Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu,” 1Pet 2:20b

“Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake,” 1Pet 2:21

“Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet 2:22

“Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki,” 1Pet 2:23

“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:24

“Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu,” 1Pet 2:25

TAFAKARI: “Wote tumeitwa kama tulivyo; Kristo ndiye Mlango. tumrudie Mchungaji na Mwangalizi wa roho zetu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya mwaka “A” wa Kanisa. Masomo yetu ya leo yanatualika kuyatafakari haya: “Wote tumeitwa kama tulivyo; Kristo ndiye Mlango. Tumrudie Mchungaji na Mwangalizi wa roho zetu.” Hivyo, tendo la ufufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, linatuwezesha na linakuwa neema na baraka kwetu, hasa ule uwezo wa kupokea vipawa vya Roho Mtakatifu pale tu tunapofanya toba ya kweli. Ni kwa dhambi zetu imekua sababu ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, na ni kwa kupitia toba ya kweli kwa dhambi zetu twapokea neema na baraka, na kuhesabiwa tena haki kuwa warithi na wana wa Mungu. Ni kwa sababu hii, leo kwa namna ya pekee tutafakari juu ya neno hili, “Kwa Ufufuko wa Yesu Kristo sote twahesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli; Naam, sote kwa upendo wa Mungu twaitwa wana wake na yeye ni Mungu wetu.”

Mtume Petro, kwa kujaliwa ujasiri na nguvu ya Kristo Mfufuka, haoni haya kuwaambia Wayahudi ukweli kuhusu wokovu wao baada ya kufanya kosa la kumwua mwenye haki-Yesu Kristo. Hata sasa Mtume Petro ananiambia mimi na wewe ambao twahitaji huruma na neema ya Mungu. Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38.

Ndugu yangu, ni kwa jina la Yesu Kristo tu twaweza kupata msamaha wa dhambi, na kupatanishwa tena na Mungu Baba. Na ni kwa njia ya ubatizo tunafia dhambi na kuzaliwa wapya kama ishara halisi ya Ufufuko wa Yesu Kristo. “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu alisiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:13-15. Ili tufaidi neema za Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo, ikiwa ni pamoja na vipawa vya Roho Mtakatifu, yatupasa kufanya toba ya kweli, ikiambatana na kuzaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Toba ya kweli ni kutambua kule kujikwaa kwetu, na kuyaacha maanguko hayo, huku tukifuata njia iliyo sahihi. Yesu Kristo pasipo shaka yo yote, ndiye njia sahihi ya kufuata, kwani kwa Ufufuko wake, yaliyo ya kale, na yasasa, na yajayo yamekwisha eleweka. Tuendako sasa twakujua. “Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu,” Yoh 20:17. Ili tupate mastahili ya kumshika Kristo Mfufuka, yatupasa kufanya toba ya kweli kama nilivyokwisha kusema. Yesu anamwambia Mariamu na kumbumbusha toba ya kweli. Huu ni wito wa kujitakasa kwa yale mambo yanayotukwamisha kuiona sura ya Mungu. Mastahili yetu baada ya kuhesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli, ni maisha ya utakatifu.

Maisha mapya baada ya Ufufuko, ni maisha ya Utakatifu kwa wote wanaoridhia njia ya Kristo. Kuridhia njia hii ni kufanya toba ya kweli. Tendo hili la toba ya kweli ndani na katika Kristo, linatupa mastahili sawa bila kujali historia zetu mbaya, makabila yetu, na hata utaifa wetu. Tendo hili linatupa uhalali wa kuwa wana wa Mungu. “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie,”  Mdo 2: 39. Tendo hili ni upendeleo mkubwa sana kwetu, na upendo wa Mungu wa ajabu. Je, watambua jambo hilo? Je, wayajua mapungufu yako? Na je! waona umuhimu wa kupatanishwa na Mungu Baba kupitia ushindi wa Mwanae dhidi ya uovu na dhambi?

Njia na namna yetu ya kuishi baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo inatusukuma kuishi upya katika kutenda na kunena. Ni maisha ya ushuhuda wa kweli. Kwa maana hii, Mtume Petro anasema, “Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40. Leo tunaisha katika kizazi chenye ukaidi uliokithiri. Leo walio wengi siyo kwamba tu hawaamini, ila pia hawaoni umaana wa maisha yenye uhusiano na Mungu. Wengi wamefikia hatua ya kuona historia nzima ya wokovu wetu kama hadithi za kufikirika tu. Tupo kwenye wakati wa “ponda mali kifo chaja.” Kwa mtu yeyote na hasa kiongozi akikosa hofu ya Mungu ndani yake, maisha na utu wa binadamu hauna tofauti na bidhaa rahisi na isiyodumu kuwahi kutokea. Leo tunashuhudia mauaji ya wazi na kikatili kuwahi kutokea, na hata watu kupotea.

Wapendwa katika Kristo, tunamwitaji Kristo ambaye ndiye Mlango wa kwenda mbinguni. Kristo akiwa nafsi ya pili ya Mungu, katika utendaji ndiye aliye mwokozi kwa kile kilichoanguka. Nafsi hii inapokuwa katika utendaji haimaanishi kwamba kwa wakati huo nafsi nyingine hazifanyi kazi, yaani Mungu Baba na Roho Mtakatifu. Ni vile vile Roho Mtakatifu katika utendaji, uvitakatifuza vyote vilivyokombolewa na Kristo, na kwa namna hiyo hiyo nafsi nyingine, yaani Mungu Baba, na Mungu Mwana hufanya kazi pamoja. Na ndiyo maana Yesu anasema maneno haya, “Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo,” Yoh 10:1-2.

Kristo ndiye Mchungaji wa kondoo na pia ndiye Mlango wenyewe. Kristo ndiye Mlango halisi wa kwenda Mbinguni. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo, Yoh 10:7. Anayempinga Kristo na kutokufuata maagizo yake, ni kwa namna hiyo hiyo anajifungia mlango mwenyewe wa kutokuiona Mbingu. Yesu anasema, Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho,”Yoh 10:9. Kukua kwetu kiroho kunategemea uhusiano wetu na Kristo, na namno tunavyolishwa na neno lake. Ndugu yangu, malisho yako yako kwa nani?

Ingawa ni kweli kwamba tumestahilishwa wokovu na uzima huo wa milele bila mastahili yetu, mimi na wewe yatupasa kuishi upendo ule aliotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo, yatupasa “kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu,” 1Pet 2:20b. Utendaji huu wa wema wapaswa kuendana na utimizaji wa nyajibu tulizopewa na umma kwa uaminifu bila kubaguana kwa namna yoyote ile, “kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake,” 1Pet 2:21. Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu na hitimisho ya yale yote tuyafanyayo leo na sasa. Kwa Kristo ipo njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6.

Kristo Yesu ndiye kielezo na hitimisho la maisha yetu kama ifuatavyo: Moja, Yesu aliishi hali yetu ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na mahangaiko yetu ila “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet 2:22. Kwa mantiki hii, Kristo Yesu ni mwalimu na kiongozi wa kufuata katika maisha mwili na roho. Pili, licha ya kuishi hali yetu ya kibinadamu, hakusukumwa na hisia mbaya katika kuona, kufikiri, kuamua, na kutenda. Kwa maana hiyo, “Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki,” 1Pet 2:23. Kristo Yesu aliishinda hali ile ya kibinadamu na kudhihirisha Umungu wake.

Tatu, Kristo kama kielelezo na hitimisho la maisha yetu kwake Kristo wokovu na uponyaji upo na unawezekana. Hivyo Kristo “…mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:24. Nne, ndani na katika Kristo tu salama kwa sababu tunaye Mchungaji mwema. “Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu,” 1Pet 2:25. Tendo hili, na kweli hii, ni mwaliko kwetu wa kujisalimisha kwa Kristo bila kujibakiza.

Wapendwa katika Kristo kama ilivyo kwa kila mmoja wetu yawezekana kuwa kajisalimisha kwa Kristo au kitu fulani, Janeth Msomi alijisalimisha katika majivuno yake. Hivyo hakuhitaji chochote kwa yeyote isipokuwa ufahamu wake.

Ikiwa ndiyo kwanza tumeanza msimu wa mvua, yaani, masika, Janeth akiwa na gari yake aina ya “Prado Land Cruizer” akielekea vijijini kwao, mvua zilikuwa zinanyesha bila kukatika. Baada ya mwendo wa masaa mawili, Janeth alifika karibu na mto mkubwa na pale daraja lilikuwa limevunjika na kuchukuliwa na maji.

Pembezoni mwa mto ule walionekana wazee wawili wenye mitumbwi yao wakiwa wanaifanyia usafi. Hata hivyo, baada ya kuona gari ile Prado, Mzee mmoja aliondoka na kutaka kujua kama mwenye gari anahitaji masaada. Mzee yule aligonga dirisha la mlango, na Janeth alishusha kioo. “Mwanangu pole kwa safari. Kwa bahati mbaya leo hutaweza kuvuka mto huu kwa gari lako kwa sababu daraja limezombwa na mafuriko. Jambo la kufanya ni hili; ‘waweza kuliacha gari lako nasi tukakuvusha kwa mtumbwi wetu. Gari lako tunalilinda hadi utakaporudi huko uendapo,” Mzee yule alitoa ushauri huo kwa upole.

“Ningehitaji ushauri wako Mzee ningewafuata na kuwauliza. Hivyo, usiniambie kitu chochote kabla ya kukuuliza,” Janeth alimjibu Mzee yule kwa jeuri huku akipandisha kio cha gari lake nusura ya kuvibana vidole vya Mzee yule. Mzee yule aliondoka kwa upole na kurudi kwenye mtumbwi wake.

Watu wengi walifika na magari yao. Waliyaacha magari hayo, na kupakia mitumbwi na kuvushwa ng’ambo ya mto.

Ndugu yangu, kuikamilisha safari yako ya maisha licha ya kufanikiwa kwa mambo mengi kwa nyakati tofauti wahitaji mtumbwi. Mtumbwi huu wawezekana kuwa jirani yako, au yeyote yule utakayekutana naye katika safari ya maisha yako. Ni vyema kuusikiliza ushauri wao na kuepuka kuwahukumu kadiri ya mwono wao. Kristo Yesu kwetu ni zaidi ya mtumbwi.

“Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet 2:22

Tusali:-Ee Yesu na Mchungaji wetu mwema, kwako twajisalimisha. Amina

 
 

No hay comentarios:

Publicar un comentario