JUMAMOSI WIKI YA 4 YA
PASAKA
Somo:
Mdo 13:44-52
Zab:
98:1.2-3ab, 3cd-4
Injili:
Yoh 14:7-14
Nukuu:
“Bali
Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa
na Paulo, wakibisha na kutukana,” Mdo 13:45
“Paulo na Barnaba
wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu
kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa
hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa,” Mdo 13:46
“Mataifa waliposikia
hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima
wa milele wakaamini,” Mdo 13:48
“Lakini Wayahudi
wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha
watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao,” Mdo 13:50
“Na wanafunzi walijaa
furaha na Roho Mtakatifu,” Mdo 13:52
“Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku
hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe
wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9
“Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu;
lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh 14:10b
“La!
Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11b
Yeye
aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa
kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12
“Nanyi
mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya
Mwana,” Yoh 14:13
TAFAKARI:
“Jumuiya ya kwanza ya wakristo na Changamoto za uinjilishaji; Yote yawezekana
ndani na katika Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo ni jumamosi ambapo kwa namna ya pekee Mama Kanisa anatualika tutafakari
neno hili, “Jumuiya ya kwanza ya wakristo na Changamoto za uinjilishaji; Yote
yawezekana ndani na katika Kristo.” Ni ukweli usio tia shaka kwamba kukua na
kuongezeka kwa Kanisa letu kumekuwa hivyo kama kulivyo kutokana na changamoto
mbalimbali katika huinjilishaji. Tukitazama jumuiya ya kwanza ya Wakristo kama
ilivyo, walikalibiliana na upinzani mkubwa juu ya kile walichoamini sambamba na
tukio zima la ufufuko wa Yesu Kristo. Tendo hili kwa ujumla wake liliweza
kuwaunganisha watu na wakati mwingine kuwatenganisha kutokana na kile
walichokuwa wakikiamini awali juu ya maisha yao na maana halisi ya Masiha.
Kutokana na wimbi hili
la sintofahamu, jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo iliwapasa kusema juu ya Yesu
Kristo waliyemjua, waliyeishi naye, na yale aliyotenda kwa maisha yao na ufunua
mzima wa historia ya wokovu wa mwanadamu kadiri ya Maandiko Matakatifu
yalivyofumbua ukweli huu. Ni katika hali hii ya kumtangaza Kristo kadiri ya
mguso wa maisha ya kila siku ya yule waliyemwamini (Yesu Kristo) na ufunuo wa
Maandiko Matakatifu yalivyoufunua ukweli huu kupingana na ufahamu ya Wayahudi
kuhusu Masiha, Wayahudi hawa hawakuwa tayari kusikia alichokisema Mtume Paulo.
Hivyo Mtume Paulo analazimishwa kukaa kimya na Wayahudi kutokana na wingi wa
watu kuukubali ukweli juu ya Kristo. Hapa ndipo tunapoongelea kuhusu wivu wa
Wayahudi kuhusu ukweli juu ya Kristo. “Bali Wayahudi, walipowaona makutano,
wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na
kutukana,” Mdo 13:45.
Ndugu yangu
tunayesafiri sote katika tafakari hii, aliloanzisha Mungu hatuwezi kulizuia kwa
ufahamu wetu mdogo tuliokuwa nao. Tunapoukataa ukweli wa Mungu, Mungu ufikisha
ukweli huu kwa watu wengine. Licha ya kwamba Taifa la Israeli lilipendelewa
kufanya maagano na Mungu katika safari hii ya ukombozi, Mungu katika kutimiza
hazma yake hakujali kufikisha ujumbe wake wa wokovu kwa wale waliomridhia. Ni
katika namna hii wewe na mimi leo tunahesabiwa haki tunapoishi kweli hii ya
kimungu tuyafanya na kuyatimiza kwa uaminifu yale yampendezayo Mungu. Hivyo, “Paulo
na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe
kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa
hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa,” Mdo 13:46.
Ninapotafakari hazma ya Mungu katika malengo yake ya umilele ndani yetu,
nimegundua kitu hiki; binadamu huweza tu kuchelewesha hazma ya Mungu katika
ukamilifu wake kwa wakati ufahao, ikiwa ni subirá tu ya Kimungu kwa kujali
uhuru aliokuwa nao binadamu kwa kujirudi na kumrejea muumba wake, ila binadamu
huyu hawezi kubadili mpango wa Mungu kwa kile anachoona kinafaa kwa maisha yetu
na malengo yake ambayo kwa wakati wote na nyakati zote ni mema.
Ndugu yangu, ni kwa
namna hii lile aliloazimia Mungu linabaki kuwa na mashiko kwamba, “Mataifa waliposikia hayo wakafurahi,
wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele
wakaamini,” Mdo 13:48. Mara zote ushindi kama huu hauachi kuwa na upinzani.
Unapoona umepita katika msuguano wa kiimani wa mtindo huu, yakupasa kujiandaa
vyema katika hali kinzani kwa kile ulichokisimamia. Nalisema hili si kwa
nadharia ila kwa vitendo kutokana na mang’amuzi yangu ya kichungaji kwa miaka
sita niliyokaa Parokiani kama Paroko mara tu baada ya upadirisho wangu. Kile
ulichokisimamia katika kweli na haki katika Kristo bila tuterereka, yakupasa
kujiandaa katika ukinzani wake. Jambo hili na ukweli huu unawakuta Mtume Paulo
na Barnaba. “Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na
wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa
katika mipaka yao,” Mdo 13:50. Katika hali ya namna hii, wewe kama mchungaji
nikimaanisha mwenye dhamana kiimani mathalani Paroko, yakupasa kusimama imara
katika kweli na haki Kristo akiwa msingi wa yote. Yatakayotokea kutokana na
msuguano huu ni mapito tu. Yatakuja kwa kasi kubwa, ila yatatoweka kama moshi
wa mabua angani. Mwisho wa msuguano huu ni ukamilifu wa kweli ya Mungu, na
furaha ya kweli kwa kile ulichokisimamia kama mpakwa mafuta. Jambo hili
lilitokea pia kwa Mtume Paulo na Barnada. Roho wa Bwana hatoacha kutufariji na
kutujaza matumaini ya kulinena neno la Mungu licha ya magumu tunayokutana nayo.
“Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu,” Mdo 13:52. Kanisa leo na kama
ilivyokuwa mwanzo lapaswa daima kuishi katika ukweli huu wa Kristo ndani na
katika yeye.
Wapendwa wana wa Mungu,
msingi wa haya yote tunayoyaona kutoka jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo
yanatokana na msingi wa imani waliyokuwa nayo juu ya Yesu Kristo na yale aliyoyafundisha.
Ni ukweli usiotia shaka kwamba jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo waliamini
barabara yule wamfuatao na kumshuhudia mbele za watu. Mtume Filipo anapomwuliza
Yesu tuonyeshe Baba nayo yatosha kumwamini, Yesu anamjibu na kusema, “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe
usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe
Baba?” Yoh 14:9. Kristo anafumbua ukweli wa
kumwilishwa kwake, si tu kwa Filipo, hata kwetu pia. Kumwilishwa huku kwa Yesu
Kristo ni ukweli wa Mungu mwenyewe katika fumbo na umbo hili la kibidamu kama
sisi ila utofauti wake ni kwamba hakutenda dhambi kama mwanadamu. Yesu Kristo
anakazia ukweli huu na kusema, “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi
kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh
14:10b. Ufunuo huu wa Mungu kupitia Yesu Kristo ni wa wazi na wakati mwingine wakujificha.
Ila hapana shaka hata kidogo kwa umungu wa Kristo kunakojieleza kwa yale
aliyoyafanya yaani kazi zake.
Wapendwa
wana wa Mungu, Kristo analifumbua jambo hili pale tunapokuwa na shaka juu yake
kwa kusema, “La! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh
14:11b. Imani ya kweli juu ya Kristo ndiyo inayotufanya kuishi na kutenda kama
alivyofanya Yesu Kristo. Ukweli huu anausema Kristo mwenyewe, na wale wote
waliouishi ukweli huu, Kristo amefanya makuu kupitia kwao kwa mkono wake. “Yeye
aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa
kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Matendo makuu
hufanyika kwa mtu huyu aaminiye juu ya Kristo si kwa faida yake binafsi, ila
kwa kupitia mtu huyu Mungu anatukuzwe na kuabudiwa milele ndani ya Yesu Kristo
mwanaye. “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba
atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13. Je, ndugu yangu, hupendi kuwa sababu ya
utukufu huu wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo?
Wapendwa,
jibu la swali hili ndilo kiini cha Imani yetu, na maisha yetu kama Wakristo na
Wafuasi wa Kristo leo katika dunia hii tunayoishi: “KUWA SABABU YA UTUKUFU WA
MUNGU KUPITIA MWANAYE YESU KRISTO, na si vinginevyo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Yeye aniaminiye
mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo
atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12
No hay comentarios:
Publicar un comentario