lunes, 22 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 6 YA PASAKA


JUMANNE WIKI YA 6 YA PASAKA

Somo: Mdo 16:22-34

Zab: 138:1-2a, 2bc-3, 7c-8

Injili: Yoh 16:5b-11

Nukuu:

Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana,” Mdo 16:22-23

“Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa,” Mdo 16:25-26

Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako,” Mdo 16:31.

“Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo,” Mdo 16:33.

Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu,” Yoh 16:7

“Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu,” Yoh 16:8.

TAFAKARI: “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, yawezekana wewe unayesoma tafakari hii ni Mkristo kwa kubatizwa kwako, na hivyo u mfuasi wa Kristo. Hivyo mimi na wewe ni wafuasi wake Kristo kwa sababu tunamwamini na katika yeye tumekombolewa na kupata uzima mpya. Ni ukweli usiotia shaka kwamba hata leo tunaposimama katika ukweli huu na kutoa ushuhuda huu kwa watu hasa kwa matendo yetu mema, ni kwa namna hiyo hiyo tunauvuruga ufalme wa yule mwovu, yaani shetani. Kuishi huku katika kweli, na kumshuhudia Kristo kwa watu, ndiko kunakowagarimu Mtume Paulo na Sila. “Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana,” Mdo 16:22-23. Lililo watokea Paulo na Sila si geni machoni mwetu. Wapo wengi kati yetu, yawezekana hata wewe mwenyewe imeshakutokea unateswa na kuchukiwa kwa sababu ya kutenda mema. Wakati mwingine tunapokuwa karibu sana na Kristo tunakatishwa tamaa na hata kutungiwa majina ya ajabu.

Wapendwa, tujifunze kwa Paulo na Sila. Licha ya kucharazwa bakora za nguvu, wakiwa gerezani hawakuacha kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu kwa kuimba. Furaha na matumini yao katika kufanya hayo yote inatokana na kumwamini yule wanayemshuhudia kwa watu na kwa maisha yao ya kila siku. Katika ufahamu huu hasa pale tunapokabiliwa na dhiki kubwa, Mungu ufungua njia. “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa,” Mdo 16:25-26. Ni mara ngapi najisikia furaha ninapotendewa maovu kwa kutenda mema? Leo kwa mfano tunapochafuliwa majina yetu kwa kutenda mema baadhi yetu hukimbilia mahakamani ili majina yao yasafishwe kisheria. Yesu anatuambia maneno haya mazito, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Je, maneno hayo ya Yesu yanasema chochote juu ya maisha yako?

Mateso na mahangaiko waliyoyapata Paulo na Sila na kuyapokea kwa furaha kwa sababu walijua ni nani wanayemshudia, yanakuwa somo kwa watesi wao. Baada ya minyororo waliyofungwa kufunguka kwa namna ya ajabu, ikiambatana na milango ya gereza kufunguka, mlinzi wa gereza anataka kujiua akifikiri wafungwa wametoroka. Paulo na Sila hawaachi kumtuliza na kumuhubiria habari njema ya wokovu. Mlinzi huyu wa gereza baada ya tendo hili kuu, anataka kujua hatima ya maisha yake. Hivyo Paulo na Sila wanamwambia maneno haya, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako,” Mdo 16:31. Kuwa huru ni kumwamini Mwana wa Mungu, na huko kuna furaha ya kweli. Neno hili linakuwa ukurasa mpya wa huyu mlinda gereza. Bwana Yesu akishakutembelea hatakuacha hivi hivi. Upendo wa Kristo unatuwezesha kutenda mema hata pale ambapo mwanzo ilikuwa vigumu kufanya hivyo. Ni kumruhusu tu akutumie katika yale ayaonayo yanafaa kwako. Hivyo Mlinzi huyu wa gereza, Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo,” Mdo 16:33. Neema ya Mungu ni ya ajabu. Uvumilivu wa Paulo na Sila umekuwa sababu ya wokovu kwa familia hii. Jambo la kushangaza ni hili, wengi wetu iwe wakati wa neema au dhiki muda wote ni kulalamika tu. Kuanzia asubuhi hadi jioni kulalamika tu. Je, unashindwa kumshukuru Mungu hata kwa ufahamu huo alikupa unaoutumia kwa kulalamika? Acha kulalamika ili Kristo afanye makuu ndani yako.

Wapendwa, wakati mwingine tunakuwa na sababu ya kulalamika hasa pale tunapokosa mwelekeo kabisa wa maisha. Tunabakia kusema kwa nini mimi tu haya yote yatokee kwangu? Katika hali hii, hatuna sababu ya kushindana na Mungu, kwani vita hivyo hata kama ungekesha huwezi kushinda. Kitu cha kufanya nyakati hizi za sintofahumu ni kukubali mapenzi ya Mungu yafanyike ndani mwako kadiri aonavyo yeye. Mara nyingi tunashinda majaribu kama haya tunapojiachia bila kujibakiza kwa Mungu. Huku ni kujisalimisha kuliko kweli. Katika hali hii ya kujisalimisha, Roho Mtakatifu utufunulia yaliyojificha na kutuonyesha njia ya kufuata na kutupa mwanga pale ambapo kiza kinene kimetanda. Hii ndiyo anavyotuahidia Yesu Kristo baada ya kupaa kwake Mbinguni. “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu,” Yoh 16:7. Roho huyu Mtakatifu hutuhakikishia mambo makuu matatu; habari ya dhambi, haki, na hukumu. Mambo haya matatu hayatakuwa kikwazo kwetu kama tunaishi mapaji yake saba: hekima, akili, shauri, nguvu, ibada, elimu, na uchaji wa roho. Hivyo, Yesu anasema, “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu,” Yoh 16:8. Tumwombe mara zote Roho Mtakatifu atujalia mapaji hayo saba ili tusidondoke katika dhambi, tutende haki, na tusije tukahukumuwa vibaya kwa kutokutenda mema.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu,” Yoh 16:7

Tusali:-Ee Roho Mtakatifu, tujalie mapaji yako saba ili tuishi Ukristo wtu vyema. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario