domingo, 31 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-B
1/6/2015
Somo: Tob 1:1a, 2; 2:1-9
Zab: 111:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mk 12-1-12
Nukuu:
            Lakini jirani zangu walinidhihaki, wakasema, “Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia, na kumbe! Anazika maiti tena,” Tob 2:8
Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6
Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7
“Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8
TAFAKARI: “Upendo wa kweli ni kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya wengine.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tulitafakari neno hili; “Upendo wa kweli ni kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya wengine.” Ukomavu wa imani yetu unao endana na Ukristo wetu, hupimwa kwa kiwango cha upendo wetu kwa wenzetu na ule utayari wa kuteseka kwa ajili ya wenzetu. Utayari huu si ule wa kujianda kwa ajili ya kufanya kitu kizuri ya kuwasaidia wengine, bali ni kuwa tayari kwa lolote linalotokea na kujitosa kwenye jambo hilo kwa nguvu zako zote, uwezo wako wote, akili zako zote, na hata muda wako wote.
Tunaona utayari huu kutoka somo letu la kwanza, pale ambapo Tobiti anapotapa habari ya mtu kunyongwa na kutupwa sokoni. Tobiti anapata taarifa hii kupitia mtoto wake ambaye alimtuma kwa nia njema kwamba aende amtafute mtu masikini wa Taifa lao aje ashiriki naye chakula. Badala ya mtu masikini, anapata taarifa ya mtu aliyenyongwa hadi kufa na kutupwa sokoni. Binadamu hueshimiwa kutoka na utu wake, hivyo hata akifariki maiti yake huifadhiwa kwa heshima. Licha la ukweli huu, Tobiti anaenda mbali zaidi, na kufanya maiti huyu kuwa sehemu ya msiba wake. Hivyo kwa heshima zote anamzika na kukubali kuingia unajisi kutokana na upendo huu wa ajabu na kuwajibika. Majirani zake wanambeza kwa tendo hili, na kusema, “Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia, na kumbe! Anazika maiti tena,” Tob 2:8.
Wapendwa wana wa Mungu, si mara moja tumekutana matukio kama haya, na wakati mwingine  na maiti zisizokuwa na ndugu wa karibu. Wapo kati yetu ambao mara tusikiapo habari kama hizi huguswa na kuwajibika kadiri ya uwezo wetu. Wapo wengine wanapokutana na matukio kama haya ujisemea mioyoni mwao, “jambo hili halinihusu, kila mtu na mzigo wake.” Labda nikukumbushe ukweli wa jambo hili. Hakuna binadamu yeyote aliyejizika mwenyewe. Unaweza kufanya maandalizi ya awali, mfano; kuchimba kaburi na kulipamba unavyotaka, kununua sanda, kuchonga jeneza, na mambo mengine katika hatua ya awali ya maandalizi, ila hutoweza kujibeba na kulifunika kaburini ukiwa maiti. Watu wengine lazima wakuhifadhi.
Kwa maana nyingine, tatizo lolote lile linalomkumba binadamu mwenzangu laweza kwa namna hiyo hiyo kunipata mimi mwenyewe. Hivyo hata siku moja usilipige kisogo tatizo la mwenzako. Fanya chochote kile unachoweza kukifanya, na mara nyingine saidia mapema kabla mambo hayajaharibika. Kama ni mgonjwa hangaikia kwa bidii zako zote matibabu yake, na usingoje akifa ndiyo uonyeshe upendo kwa kujitoa. Tunaona maigizo mengi sana ya wakristo ambao uthamini sana maiti kuliko uhai wa mtu. Tupo tayari kujitoa sana kwenye msiba kuliko wakati mtu huyu alipokuwa akiitaji huduma za matibabu. Haya ni maigizo ya upendo.
Katika somo letu la Injili, Yesu anatoa simulizi la historia nzima ya wokovu wetu, na kufunua  mioyoni kwa Wayahudi hitimisho la historia hiyo kwa kifo chake ambacho wao Wayahudi watakitekeleza kutokana na mioyo yao kuwa migumu kwa kutokupokea upendo wa Mungu na kuuishi.
Mungu katika kumkomboa mwanadamu alitumia njia mbalimbali na watu mbalimbali hatua kwa hatua. Lakini hapa mwishoni amemtuma mwanaye mpendwa Yesu Kristo akiamini kuwa huyu tutamsikiliza.Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6 Kinyume chake, tumejitwalia na tunaendelea kujitwalia mambo ya Mungu mwenyewe na kutaka kuwa wamiliki wa kitu ambacho kwa uhalisia na silika yetu hatuwezi.
Njia iliyorahisi mara nyingi kwa mtu mwovu ni kuchukua nafasi ya yule anayemwona kuwa ni kipingamizi chake. Kristo kwa upande wa Wayahudi na sisi sote tusiopenda kupokea na kuuishi upendo wa Mungu ni wapinzani wa ukweli huu. Kuchukua nafasi ya mpenzani wako katika maani niliyoisema ni pamoja na kumfifisha mpinzani wako, ambako mara nyingi huchukua mwelekea wa kukatisha uhali wa mtu yule. Kwa maana, ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yak 1:15. Hivyo Yesu Kristo anatabiri kifo chake na kuwaambia Wayahudi kwa mfano ule wa wakulima, wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7. Nao wakafanya kadiri ya dhamiri zao mbovu. Ila pamoja na hila hizi za kibinadamu na za uovu, hatuwezi kufifisha upendo wa Mungu. Kristo ndiye mpango mzima wa Mungu. Hivyo, Kristo ni, “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni,” Mk 12:10.
Wapendwa wana wa Mungu, kamwe usimtendee binadamu mwenzako ubaya. Binadamu huyu ambaye hujua familia yake, ukoo wake, kabila lake, na taifa lake anachapa ya Mungu ndani yake. Ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kutomtendea wema na haki ni kutomtendea Mungu wema na haki hiyo ambayo ni yake, na kwa kufanya hivyo uku ukijiita mwana shirika fulani la kitume, wana kikundi fulani parokia, mwana maombi, nk, ubakia kuwa upendo wa maigizo ambao mara nyingi wewe na mimi ni waigizaji maarufu.

Tumsifu Yesu Krito!


EE YESU TUJALILE UPENDO WA KWELI, NA TUWE TAYARI KUTESEKA KWA AJILI YA WENGINE. AMINA

sábado, 30 de mayo de 2015

TAFAKARI: SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
31/5/2015
Somo I: Kum 4:32-34, 39-40
Zab: 33:4-6, 9, 18-20, 22
Somo II: Rum 8:14-17
Injili: Mt 28:16-20
Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Nukuu:
Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine,” Kum 4:39
Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele,” Kum 4:40
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu,” Rum 8:14
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:16-17
Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,” Mt 28:18 
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu,” Mt 28:19
TAFAKARI: “Mungu kaufungua upendo wake wa ndani kwetu.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mama Kanisa dominika iliyopita amekamisha umaana wake katika Imani kwa kuvuviwa Kanisa Roho Mtakatifu. Dominika hii tunaielekeza katika tafakari nzito baada ya tukio la Pentekoste katika msingi na kina cha fumbo la Imani, ikiwa ndicho kielelezo sahihi na utambulisho wake popote duniani, kuitangaza Imani hiyo na kuifanya hai. Ni fumbo linalotutaka tuelewe kadiri ya uwezo wetu Mungu ni nani (rejera CCC 738).
Wapendwa, fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini na msingi wa  Imani ya Kikristo na maisha kwa ujumla wake. Ni fumbo la Mungu wenyewe (CCC 234)-ambaye ni mmoja katika nafsi tatu. Kupitia Kristo na Roho Mtakatifu tumekuja kujua kwamba kwa Mungu kuna nafsi tatu; katika umoja wa Kimungu, na utofauti kati ya nafsi hizi ndiyo hufanya uhusiano katika umoja huu Mtakatifu. Agizo la mwisho la Yesu kwa wanafunzi wake, Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,” Mt 28:19. Wanafunzi hawa wanafanywa kuwa hivyo, “mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Ni kwa tendo hili la ubatizo, mbatizwa anafanywa na kushirikishwa ukweli wa Imani hii katika uhasilia wake kwamba, “Mungu ni mmoja, Baba Mwenyezi, Mwanawe wa pekee Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu: UTATU MTAKATIFU” (CCC 233). Kanuni ya Imani katika Utatu Mtakatifu ndiyo inayotufanya sisi kuwa Wakristo. Kwa maana hii, vikundi vya kidini ambavyo hubeba na kumtukuza na kumuheshimu Kristo, na kufikiri wao wenyewe kuwa Wakristo lakini hawakiri Imani ya “Mungu mmoja katika nafsi tatu,” kwa tendo hilo wanakosa uhalali wa kuwa Wakristo katika maana halisi. Mfano: Kundi hili si tu kwa upande wa Waislamu wanaokiri kuna Mungu moja tu bila nafsi hizi tatu, lakini pia ‘Mormons,’ Seventh Day Adventists,’ na ‘Mashahidi wa Jehova.’
Wapendwa, Utatu Mtakatifu ni tendo la Mungu kuufungua upendo wake wa ndani kwetu. Kwa ufunuo huu kwetu wa siri za ndani za Mungu juu ya maisha yake, Mungu anatualika katika upendo wake kiasi kwamba hakuna binadamu yeyote alionao au awezaye kufanya hivyo. Kwa mantiki hii, haijalishi kwa kiasi gani tunajaribu, hatuwezi kufahamu fumbo hili la kujifunua Mungu kwetu kwa namna hii ya ajabu. Kama binadamu twaweza kuongea kuhusu mawazo yetu na hisia zetu kadiri ya mang’amuzi yetu, bali kile tulicho kinabakia kuwa fumbo kwetu. Mungu kwa kinyume chake, yu wazi katika ukamilifu wote kwa yeye mwenyewe. Hata hivyo haikumlazimu kujifunua  hivyo kwetu; tunajifunua wenyewe kwake (kadiri ya uwezo wetu) kwa wachache, na wakati mwingine kwa marafiki wetu wa karibu. Lakini kwa upande wa Mungu sisi si tu viumbe, bali ni marafiki wake wa pekee. Yesu Kristo analifunua jambo hili kwa kusema, “15 Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:15
Wapendwa, nafsi ya kwanza ya Utatu Mtakatifu ni Baba. Hata kwa wazazi wanaojali na kuwajibika, mwanamke ambaye ni zaidi ya kitu kingine chochote ni Mama, na mwanaume kwa yeye kuwa Baba ni zaidi ya kitu kingine chochote wake, hata hivyo haijawa hivyo wakati wote, na haiwezekani kuwa hivyo kila wakati. Ni mara ngapi tumeshuhudia wazazi hawa kuzisaliti ndoa zao na hata familia zao?
Lakini ambacho Kristo amekifunua kuhusu Baba yake, ndiyo uwasilia wa Yeye mwenyewe. Yeye Kristo, “ndiye BABA”-katika mwono wa kuwa kile alicho Baba. Kila anachokifanya Kristo, kila neno analoliongea, kwa kila namna anavyotutazama na kutuchukulia ni kama “Baba.” Ni mara ngapi tunamfikiria Mungu na kusahau ukweli huu! Na ni kwa namna ipi inahathiri maisha yetu tunaposhindwa kuishi katika upendo,-nguvu ya upendo wa Baba ambaye anatupenda zaidi ya namna tunavyojua!
Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu ni  Mwana. Mwana amechukua umbo la kibinadamu na kukaa nasi kutufanya kuwa kama yeye na kuunganika naye kwa kufuata mfano wake, kuwa wana wa Baba (“Filii in Filio”) kwa kila kitu tunachofanya, na kusema, kwa kila namna tunavyomtazama yeye.
Nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu ni Roho Mtakatifu. Upendo kati ya Baba na Mwana ni wa Kimungu. Kwa nguvu na uhimara huo, ni upendo usiotenganishwa. Upendo huo umemwagwa katika mioyo yote kwa kushiriki tendo la kipentekoste kupitia sakaramenti ya Ubatizo. Upendo huo ndiyo unaotuwezesha kuhusiana na Mungu kama Baba, kutambua kwa Kristo ndugu zetu. “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba,” Rum 8:15. Roho Mtakatifu anatupa ushuhuda kwamba sisi ni watoto wa Mungu, na kwa pamoja tu warithi na Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu ni wamilele. Huyu ni Mungu anayetusubiri katika umilele. Je, si wakati wa kumfahamu? Ni kweli hatuwezi kwa kutokea mbali kuelewa fumbo la maisha yake ambayo amekuwa huru kujifunua kwetu. Lakini hatuwezi kusahau kwamba Roho Mtakatifu huishi ndani ya mioyo yetu, na tunapomuhusisha kwenye sala zetu, kuishi Imani yetu katika kweli, tunapata mang’amuzi ya Mungu ambayo huenda zaidi ya huwezo wetu kibinadamu, na kutupa uhakika kwamba twaitaji kumjua yeye uso kwa uso katika umilele.
Wapendwa, Mungu wa uwepo wetu si mwenyewe. Wanaoishi maisha upweke na wajane, wanaojiona kuwa wamesahauliwa, kutengwa, wote hao ni uchaguzi na uangalizi wa pekee wa Mungu. Hawapo wenyewe hata kidogo. Mungu ni tajiri na mwingi wa uhai, hata kabla ya kuziumba mbingu na nchi. Wazee, wasiojiweza/walemavu, wasio na kazi, masikini, wote wanaalikwa na Yeye kutambua kwamba Mungu yupo nao. Unachotakiwa kufanya ni kumtafuta kila siku, na zaidi kama umebatizwa, kwani umewekewa unatajiri wake, uhai wake, na dhamani yake, (utu wa kimungu) uliowekwa na kupigwa chapa ndani yetu. Kwa mantiki hii, sote tuliobatizwa tuna muhuri huu wa Utatu Mtakatifu.
Dada Getrudi ambaye ni Katibu wa Baraza la walei Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu hupenda kula chakula chake cha mchana katika Mgahawa ujulikianao kwa jina la “Utulivu.” Kabla ya kula hupenda kufanya ishara ya Msalaba, ila kwa kujificha, ili asionekana na watu.
Siku moja Paroko wa Parokia hiyo naye katika mizunguko yake alipenda kujipatia chakula cha mchana katika mgahawa huo. Sifa ya mgahawa huu inaendana na jina lake. Hivyo baada ya kuagiza chakula na kuletewa, alimwona jamaa mmoja mwenye ndevu ndefu na kikofia cheupe akimkazia macho meza jirani yake. Mtu huyu alimwogopesha sana kutokana na matukio mbalimbali yenye uhusiano na mtu huyu na hivyo alisita kufanya ishara ya Msalaba. Hivyo ilimlazimu kuifanya ishara hiyo ya msalaba akiwa amegeukia ukutani.
Baba Paroka akiwa katika mahangaiko hayo ya kufanya ishara hilo ya msalaba na baada ya kumalizia, “..na Roho Mtakatifu,” hamadi, akakutana uso kwa uso na Katibu wa Baraza la Walei Parokia akiwa naye akifanya kama alivyokifanya yeye. “Tumsifu Yesu Kristo Baba. Nawa upo hapa? Kulikoni Baba Paroko?” Katibu alisema huku akiwa na hofu. “Huwezi jua usalama wetu upo wapi siku hizi. Ni vizuri kutowakwanza wengine,” Baba Paroko alijitetea kwa kile alichokifanya.
Ndugu yangu, tusisahau maneno haya ya Yesu, “Basi kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu  aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.” Mt 10:32-33. Ni mara ngapi tunalisaliti fumbo hili, na kuukana Utatu huu Mtakatifu?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU KWA UWEPO WAKO NA HASA KUPITIA MASAKRAMENTI YAKO, TUWEZESHE KUISHI FUMBO HILI TAKATIFU. AMINA

viernes, 29 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-B
30/5/2015
Somo: Ybs 51:17-27
Zab: 18:8,9,10,11
Injili: Mk 11:27-33
Nukuu:
“Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyumba yangu ya mafundisho.” Ybs 51:23
Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha,” Ybs 51:17
wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?” Mk 11:28
Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mk 11:30a  
TAFAKARI: “Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyuma yangu ya mafundisho.” Ybs 51:23
Wapendwa wana wa Mungu, umasikini mkubwa kwa binadamu wa nyakati zote ni kule kutokujua kwake.  Kwa maana hiyo, ujinga wa mtu ni mateso yake, na ndiyo umasikini wake. Mjinga ni yule asiyefahamu. Mtu huyu ili kuondokana na karaha hii ya kutokufahamu, yampasa kujifunza. Hata hivyo hakuna binadamu yeyote katika ulimwengu huu anayejua kila kitu. Kwa mizania halisi, hakuna binadamu mwenye kujua moja ya kumi ya kila kitu hapa duniani. Kwa maana hii, kila mmoja wetu ni mjinga wa kitu fulani na kiasi fulani. Je, tufanye nini ili tuishi kwa amani na ufahamu wa kutosha?
Wapendwa wana wa Mungu, jambo la kwanza na la msingi kabisa ni kuyajua mazingira yako. Mazingira kwa maana halisi ya ufahamu, ni kuanzia hapo ulipo na hayo yanayokuzunguka. Je, unaufahamu wa kutosha kuhusu hapo ulipo na mazingira yanayokuzunguka. Usipolijua jambo hili, basi huo ndio umasikini wako mkubwa. Hali hii haijalishi rasilimali na fursa ulizokuwa nazo, wala utajiri uliokuwa nao, iwe ni wako au wakurithi. Waswahili katika hili wanasema, “mali bila daftari, huisha bila habari.” Basi kama ni utajiri wa kurithi utatoweka mara. Ni mara ngapi tunasimuliwa kwamba “familia hii wakati fulani walikuwa matajiri sana, leo ni masikini wa kutupwa.”
Ni katika mtazamo na mwono huu kibinadamu, kijamii, na kimazingira, nawaalika tutafakari neno hili; “Enyi wajinga, munikaribie, na kutua katika nyumba ya mafundisho.” Ybs 51:23. Baada ya kuona maana ya wajinga, sasa tuitazame nyumba ya mafundisho. Elimu aisemayo Mungu kupitia kwa mtumishi wake Yoshua Bin Sira, siyo elimu ya darasani katika tusomavyo leo. Nyumba ya mafundisho ni vile vyote vinavyokuzunguka wewe. Hali ya hewa na mazingira unayoyaishi ni nyumba ya mafundisho. Hali hii ya hewa itakufanya ujenge nyumba ya mtindo upi, uvae nguo za mtindo upi, na hata ulime na kula vyakula vya mtindo upi. Kitu cha kushangaza hata kwa hili ambalo lipo chini ya uwezo wetu hatuwezi kulifanya. Matokeo yake tumebakia kudokolea macho mambo ya wengine na kuyaiga kama kasuku. Vizuri vyote leo ni vile vinavyotoka nje. Lakini hapa wachina wamethibitisha si kweli. Leo matibabu mazuri ni kutoka nje. Hata viongozi wetu wametusadikisha hivyo, kwani hata mafua tu wanaenda nje kutibiwa.
 Watu unaoishi nao ni nyumba ya mafundisho. Je, upo tayari kujifunza kutoka kwa wenzako? Ukweli ni kwamba “anayekimbia mwenyewe mara nyingi hufikiri kwamba yeye ni mkimbiaji bora kuliko wengine.” Yapo mambo mengi tunayojifunza kwa wenzetu na hata kujisahihisha pale tuliposhindwa kufanya vizuri. Maendeleo kwa ujumla wake ni tendo la kujifunza na ushindani. Ila kiroho, ushindani huu huwa tunauchukulia kwa maana hii; “uwe na wifu wa maendeleo.” Kama mwenzako kajenga nyumba na kaezeka bati, basi wewe fikiri juu zaidi. Jenga nyumba yako ezeka vigae. Ushindani huu hata kwa mambo ya kiroho pia twajifunza kwa wenzetu. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuwaheshimu watakatifu. Ila wapo pia kati yetu wanaoishi maisha ya utakatifu kiasi kwamba twataka kujua siri ya mafanikio yao na hofu hiyo ya Mungu walio kuwa nayo. Ila cha kushangaza, badala ya kujifunza mazuri kutoka kwa wenzetu kama changamoto ya sisi kukua kiroho, tunakuwa sababu ya kuwaangamiza kabisa hata wasionekane katika macho yetu. Neema na baraka Mungu azifanyazo kupitia wengine, hatuwezi kamwe kuzifuta machoni mwa Mungu kwa hila zetu za kibinadamu. Roho huyu Mtakatifu afanyaye kazi kupitia wenzetu na kuwatakasa, hatuwezi kumzuia kufanya kazi hiyo kwa kujenga kuza za: wivu, visasi, kukomoana, vipingamizi na hata chuki.
Wapendwa wana wa Mungu, hatuishi kujifunza maovu kutoka kwa wenzetu ili tumwelekee Mungu. Wapo watu wengi miongoni mwetu ni wezi, hasa wa mali za umma wamekuwa mfano wa kuoigwa na kupigiwa debe. Leo vijana wengi wanavutiwa na watu waovu, na wanapenda kuwa kama wao. Vijana wengi leo wanatumika kama njia na ngazi za watu waovu kufikia tamaa zao iwe kisiasa, kijamii, kiuchumi na hata kidini. Ndugu yangu kwa nini watumika vibaya? Hapa ndipo tunapozungumzia “UPUMBAVU.” Upumbavu wa mtu ni saratani ya mtu. Saratani hii umtafuna taratibu, na mwisho wa siku hujikuta hana namna nyingine ya kuishi zaidi ya dada MAUTI. Taifa letu na jamii yetu leo ya Watanzania tunatafunwa na saratani hii-“UPUMBAVU.” Je, mpumbavu ni mtu gani?
Wapendwa, mpumbavu ni yule anayejaribu kukusadikisha usalama wake mchana kweupe akiwa analikata tawi alilokali akiwa juu ya mti mrefu. Kwa maana nyingine, ni mtu anayejifanya anajua kumbe hajui kabisa. Ninapata shida sana, na hata nashindwa kuamini inakuwaje mtu na ufahamu wake kwamba imethibitishwa mtu mfulani amejikoka mabomu {wizi, rushwa, ufisadi, nk}, bado unaenda kumkumbatia na kutaka awe msimamizi wa nyumba yako na shamba lako? Hapa kweli kuna nyumba ya mafundisho? Jambo la kushangaza zaidi hata baadhi ya viongozi wa kidini hawaoni hatari hii baada ya kupata mgao huu wa wizi.
Ndugu yangu, nyumba ya mafundisho ni uwezo wa mtu kuzisoma alama za nyakati. Kuzisoma alama za nyakati ni kufanya tathimini ya namna ulivyoishi jana, unavyoishi leo, na kutokana na mang’amuzi hayo, upate dira ya kuishi kesho. Tulio wengi mtihani huu ni mgumu sana. Ona tunavyojikanganya! Jana ulilaumu hali fulani ya masiha, leo hali ile imejirudia, na kesho unayapigia debe maisha yale ambayo jana uliyalaumu, leo yanakutesa, na kesho unataka yaendelee. Ni kuku tu mwenye ujasiri wa kuishi maisha hayo. Ukitaka kujua ujasiri wa kuku mrushie nyanya utaona uwezo wake wa kufikiri. Kuku anapoiona nyanya huanza kuidonoa ikijiviringisha upande wa pili, kuku yule yule husahau kama ulishaitoboa upande mmoja, hivyo huanza tena kuitoboa upande mwingine. Mungu hajatuumba tuwe kama kuku. Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake. Kwa nini basi tunapenda kuwa kuku? Kwa nini tunamshushia Mungu hadhi yake?
Wapendwa wana wa Mungu, tunapoyakubali mazingira ya kikuku kuku tunapoteza nira na utukufu wa Mungu. Hatuwezi kusema maneno haya; “Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha,” Ybs 51:17. Tunapopoteza nira hii na utukufu huu wa Mungu ndani yetu, hatuwezi kamwe kupata yale tunayomwomba Mungu. Huku ni kuishi bila Mungu, na mateso yake ni kuishi jangwani hadi tutakapotambua tulipoipoteza nira na utukufu ule Mungu aliotupa kwa tendo la uumbaji wetu.
Katika njili ya leo Yesu Kristo anakutana na Wapumbavu wengine. Pamoja na mambo yote aliyoyafanya Yesu ikiwa ni pamoja na miujiza yake, na mafundisho yake yaliyojaa hekima na nguvu ya kimaadili, bado hawajui ni kwa mamlaka gani anayafanya mambo hayo. Wayahudi, na hasa nyakati za Yesu, walikwisha ichakachua Torati kiasi kwamba walichokuwa wanakiishi na kukifuata ilikuwa ni tafsiri ya Torati na masimulizi mbalimbali ya marabi-TALMUD. Hivyo kwa kuitupa Torati kapuni walikosa historia nzima wa wokovu wa mwanadamu, na kilele chake katika fumbo zima la Kristo mwana wa Mungu, akiwa ndiye ufunuo wa wazi kabisa wa Mungu. Hivyo wabishi na “wapumbavu hawa,” wanahoji mamlaka ya Yesu kwa kumwambia, “Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?” Mk 11:28. Yesu hakuwapa jibu la moja kwa moja kuhusu swali lao hili kwani mazingira yalisadifu kabisa kuelewa walicho uliza.
Yesu Kristo hana muda wa kujibizana na wapumbavu. Yesu Kristo anao muda wa kuwafundisha wajinga/wasiofahamu, ili wafahamu siri ya Mungu. Mastahili ya mpumbavu katika maana hii, ni laana na wala si baraka. Wayahudi waliposhindwa kujibu swali alilouliza Yesu, Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mk 11:30a, kwa kujua mtego wake kwamba, “tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi,” na kusema hatujui, naye Yesu hakutoa jibu kwani jibu walikuwa nalo. Huu ndiyo mtazamo wa mtu mpumbavu. Hujiaminisha kujua hata kama hajui.
Wapendwa wana wa Mungu, wenye ufahamu wa kweli, na hofu ya Mungu, tuliombee sana Taifa letu. Taifa letu sasa linaongowa na mihehuko ya wapumbavu ambao wengi sana. Ni sawa na kuwapa vichaa rungu. Je, hapo unategemea nini? Kwa nini jamii yetu leo inawashabikia wezi na mafisadi? Kwa nini wengi wetu leo wamekuwa wapumbavu? Hakika mwendelezo wa upumbavu huu ni mwitikio wa laana ya Mungu. Tusipojikwamua katika mtego huu wa upumbavu, tusishangae mateso makubwa huko tuendapo. Wayahudi walipotaka kuwa na Mfalme kama mataifa mengine ya jirani zao, Mungu aliwapa licha ya kwamba halikuwa chaguo lake. Wakamchagua Sauli. Mfalme Sauli aliwanyoosha vizuri wana wa Israeli hadi pale Mungu alipowachagulia Mfalme Daudi. Je, nasi ndiko tunapoelekea?

Tumsifu yesu Kristo!


EE YESU LITAZAME TAIFA LAKO NA WATU WAKO. AMINA

jueves, 28 de mayo de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 8 YA MWAKA-B

IJUMAA YA WIKI YA 8 YA MWAKA-B
29/5/2015
Somo: Ybs 44:1,9-12
Zab: 149: 1-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Mk 11:11-26
Nukuu:
“Wema wao utawadumia wazao wao, na urithi wao una wana wa wana. Wazao wao wanashikamana na agano, na watoto wao kwa ajili yao,” Ybs 44:11-12
Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa,” Mk 11:12
14 Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako,” Mk 11.14a
Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Mk 11:17
Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu,” Mk 11:22
Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24
Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mk 11:26
TAFAKARI: “Mwaminini Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, kwa kubatizwa kwetu na leo kuitwa Wakristo bila kuishi Imani hiyo hakusadifu chochote. Hata hivyo, imani ya mtu si tu kwa kile anachokiamini kwa nadharia fulani, bali ni kuwa na imani, na imani hiyo ijionyeshe katika maisha mazima yako ya kila siku. Kwa maana hiyo, leo tutafakari neno hili; “mwaminini Mungu.” Maneno haya anayatamka Yesu kwa wanafunzi wake baada ya Petro kumkumbusha kukauka kwa ule mti aliyoulaani kwa kukosa kuzaa matunda kwa wakati wake.
Maneno haya ya Yesu yanatufundisha kwamba, maisha yetu tunayoyaishi yanapoendana na Imani yetu, neema na baraka zitakuwepo na Mungu atajidhihirisha mara zote kwa yale tunayoyaamini. Hivyo tunapoamini kuliko kwa dhati, tutastajabia mengi katika maisha. Mfumo wa maisha ulio kielelezo cha imani thabiti, ndiyo njia pekee ya kurizishana kizazi hata kizazi. Pamoja na utajiri ambao tunaweza kuwaachia watoto zetu na hata wale tunaoishi nao ni pamoja na Imani iliyo thabiti. Kwa imani hii kizazi kitaendele kumcha Mungu na kuneemeka kwa baraka zake. Hivyo, “Wema wao utawadumia wazao wao, na urithi wao una wana wa wana. Wazao wao wanashikamana na agano, na watoto wao kwa ajili yao,” Ybs 44:11-12. Huu ndio urithi utakao tuwezesha kuuona uso wa Mungu.
Wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo kama Mungu na Mwanadamu; aliona njaa kama mwanadamu, hivyo ilimpasa kula. Kama Mungu alijua ni sahihi kabisa kwa kipindi kila na majira yale ya Mwaka, Mtini ule ulipaswa kuwa na matunda. Badala yake hakupata tunda hata moja. Hivyo anaulaani mtini ule kwa kusema, “Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako,” Mk 11.14a. Kulaaniwa kwa mtini huu kunatupa angalisho kwa maisha yetu ya Kiroho. Je, tunatumia fursa tulizokuwa nazo vizuri kukua kiroho?
Wapendwa tendo hili la kulaaniwa kwa mtini huu kwa kutokuzaa matunda wa wakati wake, kunanikumbusha aina fulani ya mawe yajulikanayo kama “songoro,” kwa kichangga. Mawe haya hupatikana mitoni na kwa uhasilia wake huteleza kutokana na kukaa kwenye maji kwa muda mrefu. Kitu cha kushangaza kwa mawe haya pamoja na kukaa muda mrefu kwenye maji kwa maisha yote ya mto huo, ulipasuapo jiwe hili ndani yake ni kavu sana. Hakuna dalili ya unyevunyevu wa maji. Hii ndiyo laana ambayo tunapata kwa kutotumia fursa tuliyonayo na mazingira tuliyonayo kukua kiroho.
Ni katika mtindo huo huo miili yetu kama hekalu la Roho Mtakatifu, tunaona Yesu akiwatawanya waliokuwa wanalinajisi Hekalu la Mungu kama sehemu ya kumsifu, kumwabudu na kuomba wanapolifanya pango la wanyang’anyi kama sehemu ya biashara. “Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Mk 11:17. Hatuwezi kumsifu, kumwabudu Mungu na kusali kwa utulivu kama hatuna utulivu ndani yetu. Kumbe kukaa na kumsikiliza Mungu ni kuwa na utulivu ndani yetu. Na siyo tujitawanya kimawazo.
Zaidi ya hayo, tunasali kwa sababu tunaimani kwa kile tunachokiomba. Kama tunasali kwa sababu ni utaratibu wa familia, jumuiya na kikundi chetu cha sala, sala hiyo haina uhai. Huku ni kupotea kiimani na muda pia. Ndani na katika Kristo tunasali kwa sababu tunaamini tumekwisha pata kile tunachokiomba kwa sababu Kristo ni yote katika yote. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24. Tufanyapo tendo hili kiimani, yatupasa kuwa katika hali ya usafi kimwili na kiroho. Yatupasa kujitakasa kabla ya kutakaswa na kutiwa nguvu na neema kwa yale tuyaombayo. Hivyo hatuwezi kujongea mbele ya Mungu tukiwa na hatia. Yatupasa kujipatanisha na nafsi zetu, wenzetu, na Mungu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mk 11:26.
Wengi wetu, twajipendekeza kwa Mungu, kwa kutimiza ratiba yote kila siku tukisema tuna mpa Mungu haki yake huku upande wa pili hatuishi vyema na ndugu zetu, na jirani zetu. Kusamehe kwa Mkristo ni AMRI. “Utusamehe makosa yetu kama tunavyo wasamehe walio tukosea.”  Maneno haya katika sala ya Baba yetu, yatukumbushe wajibu wetu wa kusamehe.

Tumsifu Yesu Kristo!


NA TUSAMEHANE KILA WAKATI. AMINA

miércoles, 27 de mayo de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 8 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 8 YA MWAKA-B
28/5/2015
Somo: Ybs 42:15-25
Zab: 32:2-3, 4-5, 6-7, 8-9
Injili: Mk 10:46-52
Nukuu:
“Yeye huchunguza vilindi, na moya wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana Aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu,” Ybs 42:18
“Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lolote ambalo limefichwa naye,” Ybs 42:20
“Vyote vinahitilafiana, wala hakufanya chochote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio,” Ybs 42:24-25
Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51
TAFAKARI: Naye ni nani atakayekinai kwa kuutazama utukufu wa Mungu?
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari uzuri wa Mungu kwa vile alivyoviumba. Tunapotazama uzuri huu wa uumbaji wa Mungu, tuanze kwa kutazama maajabu hayo katika uumaji wetu. Hakika tutazamapo uzuri huo tunagundua kwamba, “vyote vinahitilafiana, wala hakufanya chochote kisicho kamili; hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio,” Ybs 42:24-25. Tazama yote aliyokujalia Mungu na ulivyo wa pekee, na anavyokupenda kama ulivyo na anavyotaka uwe kama alivyokuumba ili uwakilishe utukufu wake. Pamoja na upendeleo huo kwako, Mungu anapenda kuuchunguza moyo wako kama unashukrani juu ya upendeleo huo kwako.
Wapendwa, moyo usio na shukrani ukausha mema yote. “Yeye huchunguza vilindi, na moyo wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana Aliye juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu,” Ybs 42:18. Wengi wetu hatuoni sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna anavyotukirimia. Wengi wetu mara tuamkapo kitandani kwa mfano; hatuwezi hata kufanya ishara ya msalaba, kwa kutambua tendo hili la utukufu wa Mungu kwa kutupenda upeo. Mara tufanyapo tendo la Msaba kwa Imani na sauti ya ndani, twatambua na kukiri haya juu ya msalaba: “huu ndio ule mti wa msalaba ambao wokovu wetu umetukikwa juu yake.”
Hata baada ya kulindwa na kuepushwa na majanga mengi katika maisha kwa upendeleo huu wa Mungu, bado hatuoni sababu ya kusema neno asante. Giza lijapo twajirusha kitanbani kama mzingo usio na mwenyewe tukijua tutaamka salama kama tulivyofanya tendo hilo siku ya jana. Je, hatujawahi kusikia ‘alilala salama lakini hakuweza tena kuiona siku ya pili?’ Ndugu yangu, “Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lolote ambalo limefichwa naye,” Ybs 42:20. Mungu wetu ni mvumilivu sana. Ni mvumilivu kwa sababu Yeye ni matumaini kwetu. Matumaini haya ni matokea ya upendo aliokuwa nao kwetu usiokuwa na mfano.
Pamoja na upendeleo huo, Mungu kwa kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, yupo tayari kuyafanya yote ayatakayo Baba yake ili utukukufu wake utawale daima. Tatizo kubwa kwetu sisi tu vipofu na kushindwa kuona utukufu huo wa Mungu kwa vile alivyoviumba ikiwa ni pamoja na wewe wenyewe. Ni mara ngapi tunashindwa kumshukuru Mungu kwa uzuri na mema waliojaliwa rafiki na majirani zetu? Badala yake tumekuwa sababu na vielelezo vikuu kuudhoofisha utukufu huo wa Mungu.
Kama tuna nia ya kubadilika ili tuone vizuri kadiri ya utukufu wa Mungu, yatupasa kufanya hatua ya kwanza sisi wenyewe kama alivyofanya yule mwombaji kipofu kwa kupaza sauti ili asikike na kuponywa na Bwana Yesu. Nasi kutokana na udhaifu huo yanitupasa kusema toka moyoni, ‘Yesu mwana wa Daudi, unirehemu.’ Haya ni majuto ya kweli. Hivyo Yesu anamjibu na kumwambia, “Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51. Kwa tatizo alilokuwa nalo mwombaji huyu kipofu alijibu kadiri ya tatizo lake, yaani anataka kuona. Je, mimi na wewe swali la Yesu linatuhusu? Kama linatuhusu, je unajibu sahihi kutokana na swali la Yesu? Mjibu Yesu tatizo lako na uwe huru kuudhihirisha utukufu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NATAKA KUONA. AMINA

martes, 26 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 8 MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 8 YA MWAKA-B
27/5/2015
Somo: Ybs 36;1-2a, 5-6, 13-19
Zab: 78
Injili: Mk 10:32-45
Nukuu:                                                         
Ee Bwana, uisikilize sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako. Na wote wakaao duniani watajua ya kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele,” Ybs 36:16-17
Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?” Mk 36:38
“Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40
Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42 
Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10:43-44
Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45 
TAFAKARI: “Hamjui mnaloliomba”
Wapendwa wana wa Mungu, sala na maisha ya sala ni vitu viwili tofauti, ila hatuwezi kuvitenganisha tunapozama katika mahusiano na Mungu yaliyo ya karibu na ya kweli. Kwa ufupi, sala ni mwitikio wa ndani ya mtu ulio wa kweli na usio na shaka yoyote kwa Mungu aliye yote katika yote. Mwitikio huu ni tokeo la kiufahamu unaoweka wazi ubinadamu wetu na mipaka yake, na Umungu katika ukamilifu wake. Hivyo, mwitikio huu hujidhihirisha katika namna mbalimbali kadiri ya mguso wa ndani wa mtu juu ya mahusiano haya ya kipekee baina yake na Mungu. Mguso huu wa ndani hujionyesha nje ya mtu kama: Maombi, kusifu, kushukuru, kuambudu/kujisalimisha na ukimya wa kujizamisha ndani ya mafumbo na maajabu wa Mungu.
Hivyo basi, tukiwa na uelewa huu tutafahamu kile/lile tunachokiomba, tunachokisifu, tunaloshukuru, tunachokiabudu, na kule tunapozama katika mafumbo na maajabu ya Mungu. Leo tuelekeze tafakari yetu katika maneno haya ya Yesu, “hamjui mnaloliomba.” Maneno haya Yesu anayatamka kwa Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, ambao walimwomba Yesu wakae mmoja mkono wake wa kushoto na mwingine mkono wake wa kuli. Sala kama maombi, haitoshi tu kuweka mbele matamanio yetu binafsi, bali maombi yetu yawezeshwe kadiri ya mapenzi ya Mungu aliye yote katika yote. Yakobo na Yohana wanatanguliza matamanio yao na ubinafsi wao. Hawakuweza hata kuwakumbuka Mitume wenzao waliobaki, yaani wale kumi. Haya ni maombi yasiyo na ukomavu kiimani. Ni mara baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Yakobo anatambua maana ya maombi, na kusema, “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu” Yak 4:3. Huyu sana ni Yakobo Mtume aliyekomaa kiimani. Kwa sasa anajua kile aombacho.
Wapendwa wana wa Mungu, Yesu ndiye anayetufundisha uhusiano wa maombi yetu na matakwa ya Mungu katika sala yake kule Bustanini Getsemani. “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke,” Lk 22:41-42. Tuliombalo licha ya kwamba latupendeza na tunalihitaji, yatupasa kujisalimisha kwake yeye aliye yote katika yote, naye atupe kadiri ya hitaji letu na mapenzi yake. Huku ndiko Yesu alikomaanisha, kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi” Mk 36:38.
Hivyo Mungu aliye Baba yetu Mwema na anayetujua sisi watoto wake atatupa kadiri ya upendo wake. Hivyo, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:7-11. Hii ndiyo maana halisi ya kile tuombacho na matakwa ya Mungu kwa yale tuyaombayo. Kuhesabiwa haki kwa yale tuyaombayo baada ya kupitia taratibu zote; ni juu ya Mungu mwenyewe kutupa kadiri ya hitaji letu na mapenzi yake. Hivyo, “Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40. Mungu pekee ndiye anayetuhesabia haki.
Wapendwa, kwa kujua ukweli wa jambo hili juu ya namna ya kuomba, twaweza kuyatamka maneno haya kutoka kitabu cha Yoshua Bin Sira, “Ee Bwana, uisikilize sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako. Na wote wakaao duniani watajua ya kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele,” Ybs 36:16-17. Bila kuyafahamu mahusiano yetu na Mungu, na hali yetu ya ubinadamu, sala kama nilivyoelezea hapo juu ubakia katika hali ya ukavu.
Udadisi wa Yohana na Yakobo kutaka sehemu ya pekee kwa Yesu Kristo, kunazua mzozo miongoni mwa Mitume kwa kauli yao hiyo. Ni kama leo tunaposikia baadhi ya Viongozi wakitangaza nia zao za kutaka kugombea urahisi kabla ya wakati. Yesu analiona hili na kulikemea moja kwa moja kabla halijawa tatizo. Kristo hapa anaonyesha ukomavu katika uongozi na anawataka nao Mitume waige mfano huo. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42. Kwa upande wa Mitume hawapaswi kufanya hivyo na wala kuwa hivyo. Mitume wameshafunuliwa siri ya umilele, hivyo waishi katika mwono huo wa umilele. Nasi pia kwa ubatizo wetu tumeshafunuliwa siri hiyo ya umilele, na hivyo yatupasa kuishi kadiri ya mwelekeo huo wa umilele. Naye Yesu anatuambia, Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10:43-44. Maisha ya Mkristo ni kutumika vyema kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu, kielelezo cha  kutumika vyema ni Kristo mwenyewe aliyekuwa mfano hai kwetu na bado ndiye mfano hali kati yetu hasa pale tunapoona ndugu zetu katika jumuiya na familia wanavyojitoa bila kujibakiza na kuwa mfano wa Kristo aliye hai. Katika ukweli huu Yesu anatukumbusha kupitia maisha yake mwenyewe, akisema, kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45. Basi, nitumike vyema katika familia yangu kadiri ya nafasi yangu, nitumike vyema katika jumuiya yangu ya kitawa kadiri ya nafasi yangu, na nitumike vyema katika jamii ninayoishi kadiri ya nafasi yangu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUFUNDISHE NAMNA YA KUOMBA. AMINA

lunes, 25 de mayo de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-B
26/5/2015
Somo: Ybs 35:1-15
Zab: 49
Injili: Mk 10:28-31                                      
Nukuu:
“Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” Ybs 35: 7-9
“Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” Ybs 35:10
Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30
TAFAKARI: “Faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari neno hili; “faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu.” Kwa ulimwengu huu tunaoishi leo wenye mtazamo wa kupata tu FAIDA na kuishi katika hali ya USHINDANI, kwa haraka haraka huwezi ona faida ya kutumika VYEMA kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Tupo kwenye ulimwengu usioguswa na hofu ya Mungu, na hivyo waliowengi siyo tu kwamba hawaamini uwepo wa Mungu, bali pia hawataki kusikia habari zake.
Ndugu yangu kuna faida kubwa sana kutumika vyema kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kuzipata na kuzifikia faida hizi kwa urahisi yakupasa kuzishika amri zake kisawasawa. Kuzishika amri hizi si kwa ajiali ya kuwakonga watu nyoyo zao, bali kuona ni sehemu ya umilele wako, na amri za Mungu kuzishika kwa ufahamu, kutakuongoza katika njia iliyo kweli.
Jambo la pili, ni kuweka amri hizo katika matendo. Na kwa namna ya pekee, Bwana wetu Yesu Kristo amezifupisha amri zote kwa kuziweka katika mihimili miwili, yaani Mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, akili zake zote, na nguvu zako zote. Na muhimili wa pili Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hivyo ukimpenda Mungu kwa kile chote ulicho utafanya haya kadiri ya somo letu la leo; “Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” Ybs 35: 7-9. Jambo hili litakupa wajibu wako mbele ya Mungu. Na utawajibika kumrudishia Mungu kilicho chake. Mara nyingi tunamrudishia Mungu mabaki ya kazi za mikono yetu. Elewa vitu vyote ni mali yake MUNGU.
Mhimuli wa pili wa amri za Mungu ni kumpenda jirani yako kama unavyojipenda wewe MWENYEWE. Hapa utatambua wajibu wako kwa jirani na hasa wahitaji. Utatambua ubinadamu wako na umuhimu wa binadamu mwingine, hasa wale wasiokuwa na fursa katika jamii kutokana na mambo mbalimbali. Hivyo, “Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” Ybs 35:10. Wajibu huu ni muhimu sana kuishi katika hofu ya Mungu. Masikini tunao wengi sana. Kabla ya kuanza kuwatafuta masikini mitaani, masikini hawa tunao kwenye familia zetu, jumuiya zetu za kitawa, jumiya zetu ndogondogo, vigangoni mwetu, na hata parokiani mwetu. Masikini katika hali ya uuitaji wapo wengi sana. Wengine wengependa tu wasikilizwe hiyo ndiyo kiu yao. Wengine wengependa wakusikie tu, hiyo ndiyo kiu yao. Na wengine wangeitaji ufahamu wako katika kuchambua mambo kwa haki na busara.
Wapendwa wana wa Mungu, katika kuyafanya mambo hayo kulingana na miimili hii miwili, hatupotezi chochote zaidi ya kufaidika kwa kutumika vyema. Hakuna anayepoteza muda wake kwa kufanya yale yanayohusu ufalme wa Mungu. Ni furaha kubwa sana mbele za Mungu akiona umewapeleka wengi kwake. Hivyo Yesu anatuambia tunapoyaacha yale ambayo yangetujengea umaarufu hapa dunia usiodumu, kwa namna hiyo hiyo tunajaliwa mengi katika ufalme weke. Hivyo, Yesu anakasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Je, bado unamashaka kwa utume unaoutoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu? Kwa nini hauna furaha katika utume wake? Kwa nini utume wako unawadumaza watu badala ya kuwakuza na kufurahia ufalme wa Mungu? Kwa nini unakuwa sababa ya watu kumchukia Mungu na kuasi njia zake?

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUJALIE TUTUMIKE VYEMA KWA AJILI YA UFALME WAKO. AMINA