domingo, 28 de mayo de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 7 YA PASAKA


ALHAMISI WIKI YA 7 YA PASAKA

Somo: Mdo 22:30, 23:6-11

Zab 16:1-2a, 5, 7-8, 9-10, 11

Injili: Yoh 17:20-26

Nukuu:

“Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?” Mdo 23:3

Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako,” Mdo 23:5

“Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu,” Mdo 23:6b

“Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21

“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24

“Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26

TAFAKARI: “Furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, ipo “furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya Kristo.” Kuishi katika dhamira safi ni kuishi maisha yasiyo na hatia, yaani maisha yanayompendeza Mungu. Ni kuishi bila dhambi, ingawa twaweza kudondoka tena na tena katika dhambi. Tuapodondoka katika dhambi tuijongee neema na huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho. Ndugu yangu, neema na huruma ya Mungu kupitia Sakramenti hii ya Upatanisho ni kubwa kuliko dhambi zetu. Kuishi katika dhamiri safi kunatufanya kuwa tayari kwa jambo lolote wakati wowote. Mt. Aloyce wa Zonzaga ni mfano wa mtu aliyeishi katika dhamiri safi muda wote. Wakati fulani alipokuwa anacheza mchezo fulani, mlezi wake alimjia na kumwuliza hivi, “endapo umebakia muda mfupi tu na iwe mwisho wa dunia hii ungefanyaje? “Nitaendelea kucheza mchezo huu,” Mt. Aloyce alimjibu mlezi wake bila wasiwasi. Jibu la Mt. Aloyce wa Gonzaga linaonyesha jinsi gani alivyokuwa tayari katika yote.

Mtume Paulo kwa dhamiri safi aliyokuwa nayo haogopi kuyapokea mateso yote kwa ajili ya Kristo. Paulo anapigwa na kudhalilishwa bila kulijua kosa lake. Wapo pia wengi kati yetu bila kujua makosa yao wanajikuta wakikabiliwa na mateso hata wengine wanapoteza maisha yao.

Kristo anatuombea umoja na amani, akijua ulimwenguni humu tutapatwa na matatizo mengi. “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21. Sala hii ya Bwana wetu Yesu Kristo inaonyesha dhamiri safi aliyokuwa nayo. Dhamiri hii safi ndiyo inayomsukuma pasipo shaka kujongea mateso, na kifo kile cha msalaba.

Tunapoyapokea mateso kwa dhamiri safi tunauhakika wa kuwa pale alipo yeye, yaani, Yesu Kristo baada ya maisha haya ya hapa duniani. Uhakika huu anatupa Yesu anaposali, “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24

Wapendwa wana wa Mungu, yatupasa kuisha ndani ya pendo la Mungu nyakati zote na majira yote. Kuuishi upendo huu wa Mungu ni kutambua pia jina lake ambalo Mwana amefanya bidii zote kutufundisha. Hivyo Yesu anasema, “Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26. Ndugu yangu, kuishi upendo wa Mungu na kutenda yaliyomema huijenga na kuikuza dhamiri safi ndani mwetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24

Tusali:-Ee Mungu Mwenyezi, uniumbie moyo safi uifanye upya roho iliyotulia ndani mwangu. Amina

TAFAKARI: BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI


BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI

Somo: Sef 3:14-18a.

Zab: Isa 12:2-3, 4abc, 5-6

Injili: Lk 1:39-56

Nukuu:

Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15 

Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17

“Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42

Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49

TAFAKARI:Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anatambua ushiriki wa Mama Bikira Maria katika safari nzima ya wokovu wetu, na hivyo anaadhimisha siku hii, tendo lile ya Bikira Maria kwenda kumwamkia mpwa wake Elizabeti. Mama Bikira Maria naheshimiwa sana na kutukuzwa katika Kanisa letu Katoliki siyo kwa sababu ya uzuri wake, au upekee wake wa ajabu kama mwanamke, bali kwa unyenyekevu wake, hasa kwa kuwa tayari kuyapokea yote licha ya kutokujua nini hasa kitakachofuata au tokea katika maisha yake. Bikira Maria anaishinda hofu ile ya sintofahamu. Ukweli huu unajidhihirisha kwa maneno haya mazito ya Bikira Maria, “mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Maneno haya ya Mama yetu Bikira Maria, ni fundisho tosha ya kujiachia pasipo kujibakiza, hasa katika mazingira ya yale tusiyoelewa sawa sawa.

Leo tunaposherehekea siku ile Bikira Maria alipokwenda kumpasha habari Mpwa wake Elizabeti, itukumbushe kudumisha ujirani mwema. Ujirani mwema hudumishwa kwa kuwa na moyo safi, Lk 1:46-47. Moyo usio jilimbikizia maovu. Moyo uliyotayari kuona mazuri mara zote kwa watu wote. Moyo usipungukiwa kiti kwa nyakati zote na shida zote. Moyo uliyo tayari kutaambika kwa ajili ya wengine. Usafi wa moyo huu, ni tiketi ya kuuona uso wa Mungu. Moyo usio na hatia una nafasi kubwa sana kumwaona Mungu. Moyo huu una heri kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo, “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Mama yetu Bikira Maria pamoja na kuhesabiwa haki hiyo ya kuwa Mama wa Mungu, nafasi hiyo haikuwa sababu ya kujivunia, bali kujinyenyekesha katika udogo wa hali ya chini kabisa. Kujinyenyekesha kwake huku kuna kuwa chanzo cha mawasiliano ya kimungu kati ya fumbo lile lilikokuwa limejificha kati ya kile kilichokuwa tumboni mwake, yaani, Neno kufanyika Mwili na kukaa kwetu, na kile kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuitaarisha njia ya Neno hili, yaani, Yohani Mbatizaji. Na mambo yalikuwa hivi, Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake,” Lk 1:41. Huu ni uthibitisha wa ubebaji wa Habari Njema aliyokuwa nayo Mama Bikira Maria. Je, wewe ni habari njema hapo ulipo? Hatuwezi kuwa habari njema kama tu wafuasi wa majungu. Wengi wetu tumebeba mimba za majungu na kwa namna hiyo hatuwezi kuwa habari njema hata kama tutajifungua.

Ndugu yangu, palipo habari njema, Roho Mtakatifu aliye umoja na tunda la upendo wa Mungu Baba na Mwana, hutuunganisha katika umoja wa kweli, na usio na unafiki. Na hivi ndivyo ilivyotokea kwa mpwa wake Bikira Maria, Elizabeti.  “Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42. Roho Mtakatifu ndiye anayezungumzu ndani ya Elizabeti. Ndugu yangu, hata pale ambapo hatuna cha kusema ila tumejiachia bila kujibakiza kwa Kristo Yesu, Roho Mtakatifu utusemea na kutushuhudia. Katika hili Yesu anasema, nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:18-20. Mawasiliano haya kati ya Mama Bikira na Mpwa wake Elizabeti ni mawasiliano yenye Umungu ndani yake.

Naye bila kujibakiza, Bikira Maria anayasema yaliyo moyoni mwake, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49. Mama Bikira Maria kwa tendo hili anaona mpango mzima wa Mungu ndani yake. Pamoja na Mpango huo, Mama Bikira Maria hakuwa na sababu ya kujivuna na kujiinua zaidi ya kujinyenyekesha mbele za Mungu. Tendo hili linamtafakarisha Mama Bikira Maria kuyaona makuu ya Mungu kupitia kwake. Naye anasema, Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Akiwa mnyonge na mwenye kutostahili chochote zaidi ya kuwa mtumishi wa Bwana, Mama Bikira Maria anapata fursa ya kumshukuru Mungu na kulitukuza jina lake daima kwa kuutazama upya unyonge wa watu wake na taifa lake. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele,” Lk 1:54-55. Hakika Mama Bikira Maria ni kielelezo cha fadhila ya unyenyekevu. Hivyo kama kuna sababu ya kujisifu tujisifu kwa mambo ya udhaifu wetu kama asemavyo Mtume Paulo, 2Kor 11:30. Na penye udhaifu ndipo penye nguvu, 2Kor 12:10. Ni kwa unyenyekevu tu tunaweza kuona udhaifu wetu.

Wapendwa wana wa Mungu, unyenyekevu huu kama ulivyo wa Mama yetu Bikira Marian dio unaoweza kutuondolea hukumu ya Mungu pale tunapomkosea Mungu na kuwa tayari kuanza upya Naye kwa njia ya toba ya kweli na majuto. Unyenyekevu wetu huujenga upya ukaribu wetu na Mungu na kwa namna hivyo Mungu yupo tayari kughairi hukumu yake kwetu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15. Mungu kamwe hafurahii kuangamia kwetu kama asemavyo Nabii Isaya, Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Ndugu yangu, Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17. Sifa na Utukufu kwa Mungu wetu ajuaye mwisho wa maisha yetu. Amini.

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15

Tusali:- Ee Mama Bikira Maria, tujalie unyenyekevu wako ili nasi tufumbuliwe siri na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Amina

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA PASAKA


JUMANNE WIKI YA 7 YA PASAKA

Somo: Mdo 20:17-27

Zab: 68:10-11, 20-21

Injili: Yoh 17:1-11a

Nukuu:

Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja,” Mdo 20:22-23

“Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,” Mdo 20:24

“Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu,” Mdo 20:27

Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo,” Yoh 17:3

“Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10

“Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako,” Yoh 17:11a

TAFAKARI: “Uzima wa milele ndio huu; kumjua Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu hapa duniani kaitwa kwa namna mbalimbali na ya pekee kadiri iliyompendeza Mungu. Kuitwa huku na Mungu kwahitaji mwitikio wetu. Hivyo kila mmoja wetu anavyoitikia bila kujibakiza ndivyo anavyojazwa uzima huo wa milele ambao ni tayari katika hatua, na ambao bado katika utumilifu wake. Hapa haijalishi mwitikio huo umechukua taswira gani. Kwa maana nyingine haijalishi wewe ni mlei, matawa, au mkleri. Hivyo basi, mwitikio huu lazima ulenge kumjua Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo.

Ni katika  mwitikio huo kimaisha Mtume Paulo hajuutii kumjua na kumtumikia Mungu aliye hai, na Yesu Kristo. Hivyo Mtume Paulo yupo tayari kwa yote na lolote litakalotokea kuhusu maisha yake na uhusiano wake na Mungu. “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja,” Mdo 20:22-23. Kwa maneno haya ya Paulo Mtume tunakumbushwa kusimama imara hasa nyakati zile za sintofahamu katika maisha yetu kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake.

Mtume Paulo anajua wazi maamuzi yake aliyoyachukua katika maisha msingi wake ni Kristo mwenyewe, na hajuutii uamuzi wake huo. Siri yake ni kwamba, tunapojitoa kwake Kristo bila kujibakiza tunauhakika wa uzima wa milele, na safari yetu kuelekea katika utumilifu huo wa maisha ya umilele ni safari salama na yauhakika. Hivyo, “siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,” Mdo 20:24. Je, wewe na mimi tunao ujasiri huu na kuyatamka maneno mazito haya ya uzima katikati ya kiza kinene cha sintofahamu ya maisha kama Mtume Paulo? Kwetu kama wafuasi hai wa Kristo ni changamoto kubwa!

Wapendwa wana wa Mungu, tufanyapo maamuzi haya katika maisha licha ya magumu tunayokumbana nayo, tunajua mbele yetu yupo Jemedari Mkuu Yesu Kristo aliyeyashinda yote, na asiyeshindwa kwa lolote. Mateso na magumu tunayokutakana nayo katika maisha Kristo anayajua, na ndiye yeye atakayetutoa kwenye mikwamo hiyo kiimani endapo tutaweka matumaini yetu yote kwake kama mweza wa vyote. Katika ukweli huu Yesu achoki kutuombea na kutujaza neema na baraka akisema, “Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10. Je, kwa nini Yesu hauombei ulimwengu? Ulimwengu huu ni kama tanuru la kufulia chuma. Kupata chuma bora na imara lazima kipite kwenye moto mkali sana. Nasi katika kuyashinda mateso haya hapa duniani ndivyo tunavyojiimarisha katika imani na kunyakua taji ile tuliyoandaliwa. Kwa hiyo ulimwengu kama ulivyo ni sehemu ya kukomaza Imani yetu na kukua Kiroho na kimwili.

Ndugu yangu, Je, mateso na maisha yako kwa ujumla yana mwelekeo huo wa uzima wa milele, yaani, kumjua Mungu wa kweli na Yesu Kristo?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,” Mdo 20:24

Tusali:-Ee Mungu, niwezeshe kusimama imara kiimani ili maisha yangu yalenge kukujua Wewe Mungu wa kweli na Yesu Kristo. Amina

 

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 7 YA PASAKA


JUMATATU WIKI YA 7 YA PASAKA

Somo: Mdo 19:1-8

Zab: 68:2-3ab, 4-5acd, 6-7ab

Injili: Yoh 16:29-33

Nukuu:

“Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu,” Mdo 19:4

“Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo 19:6

“Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote,” Yoh 16:29

“Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami,” Yoh 16:32

“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33

TAFAKARI: “Kuongozwa na Roho Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, Roho Mtakatifu hakuwahi kuliacha Kanisa lake tangu zama hizo. Roho Mtakatifu amekuwa kielelezo cha yale yote tuyafanyayo kuliendeleza na kulijenga Kanisa la Kristo pale ambapo Kristo hajajulikana. Roho Mtakatifu amekuwa muhimili mahiri kabisa kuliongoza na kulitakasa Kanisa nyakati za matatizo na migogoro iliyoibuka kwa sababu mbalimbali katika historia ya Kanisa. Roho Mtakatifu aliwaongoza vyema Mitume, Mababa wa Kanisa, na katika shughuli za kimisionari, maamuzi mbalimbali na mafundisho sahihi yaliyokuwa yakifanyika katika mitaguso mbalimbali katika historia ya Kanisa.

Leo kwa namna ya pekee tunasukumwa na neno hili katika tafakari yetu; “kuongozwa na Roho Mtakatifu.” Kuongozwa na Roho Mtakatifu ni kuomba mapaji yake saba ambayo kwayo kwa kuyaishi ni utimilifu wa yale aliyokusudia Mungu kwetu, na ukamilifu wa yale tunayoyatamani katika uzima wa milele. Mapaji hayo ni kama ifuatavyo; Hekima, Akili, Ushauri, Nguvu Elimu, Ibada na Uchaji. Mapaji haya yote yanalenga kumfahamu Mungu, na kuishi katika kweli yake. Tukimfahamu Mungu na kuishi katika kweli yake, maisha yetu hapa duniani yanapata malengo yake halisi, yaani kuelekea uzima wa milele.

Ni kwa sababu hii, Mtume Paulo anawauliza Waefeso, kama walipokea Roho Mtakatifu walipoamini, na walibatizwa ubatizo gani. Maswali haya mawili yana maana sana. Kama tunaimani bila kumpokea Roho Mtakatifu tunaupungufu wa mapaji yake ambayo ndiyo kielelezo sahihi cha kumjua Mungu na kuishi katika kweli yake. Kwa maana hiyo, kama hili halipo, basi hata malengo ya maisha yetu hapa duniani yanakosa mwelekeo sahihi. Jibu la Waefeso ni kwamba hawajawahi kusikia kuhusu Roho Mtakatifu, na ubatizo walioupata ulikuwa wa Yohane Mbatizaji.

Mtume Paulo anatoa ufafanuzi wa ubatizo huo wa Yohane kwa kusema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu,” Mdo 19:4. Ubatizo huu ulikuwa maandalizi ya kumtambulisha na kumwamini yule atakaye kuja baada ya Yohane, ambaye ni Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye ufunuo halisi wa Mungu Baba, na kwa maana hiyo, Yesu anasema, “Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari,” Yoh 16:15. Jambo hili ndilo analojaribu kulisema Yohane, kwamba ukamilifu wa tendo analolifanya yaani ubatizo huo wa toba litakamilishwa na Yesu Mwenyewe.

Mtume Paulo analikamilisha lile lililokamilishwa na Kristo kwa Sakramenti hii ya Ubatizo kwa kuwawekea mikono juu yao. Hivyo, “alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo 19:6. Tunaona baada ya Roho Mtakatifu kuwa ndani yao, mapaji yake yanajionyesha mara kwa kuanza kunena kwa lugha na kutabiri. Haya ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa wale aliowaridhia.

Ni ukweli usio shaka kwamba Mitume hawakufahamu ukweli aliokuwa akiuongelea Yesu alipokuwa akisema ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona,’Yoh 16:16. Kwa sasa Mitume wanaufahamu ukweli aliokuwa akiusema Yesu. “Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote,” Yoh 16:29. Roho huyu Mtakatifu ndiye atakayetufunulia yale tusiyojajua. Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami,” Yoh 16:32. Roho Mtakatifu ndiye mfariji wetu, kwani Kristo kesha ushinda ulimwengu. Ulimwengu huu tutapata matatizo ila Roho Mtakatifu atatufunulia yale yaliyojificha. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33. Wapendwa, tumwombe Roho Mtakatifu na kutushushia mapaji yake saba ili tuzaliwe upya ndani yake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo 19:6

Tusali:- Ee Roho Mtakatifku, utushushie mapaji yako. Amina

sábado, 27 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 7 YA PASAKA-A, KUPAA KWA BWANA


JUMAPILI YA SABA YA PASAKA-A

Sherehe ya Kupaa Bwana

Somo I: Mdo 1:1-11

Zab: 47:2-3, 6-7, 8-9

Somo II: Efe 1:17-23

Injili: Mt 28:16-20

Injili: Mk 16:15-20

Injili: Lk 24:46-53

Nukuu:

“hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu,” Mdo 1:2-3

“Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8

“Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni,” Mdo 1:11

“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye,” Efe 1:17

“akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Mdo 1:22-23

“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,” Mt 28:18

“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari,” Mt 28:19-20

“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16

“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18

Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu,” Lk 24:49

“Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki,” Lk 24:50 

TAFAKARI: “Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”

Wapendwa wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anafanya Sherehe ya Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo Mbinguni. Somo la kwanza na la pili husomwa miaka yote mitatu ya Kanisa kadiri ya liturjia. Hivyo ikiwa leo tupo mwaka “A” wa Kanisa, tutasoma Habari Njema ya Bwana wetu Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili  Mathayo. Mwaka “B” wa Kanisa tulisoma kama ilivyoandikwa na Mwinjili Marko, na Mwaka “C” wa Kanisa tutasoma Habari Njema hiyo ya Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kupaa huku mbinguni ni moja ya sharti ya kuletewa Roho Mtakatifu kama mshauri wetu. Kupaa kwa Yesu Mbinguni kunatuwajibisha kila mmoja wetu, yaani kila mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake kama Sakramenti ya wokovu wetu. Ni Kanisa katika maana hii, akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Mdo 1:22-23.

Hivyo leo tutafakari kwa undani wajubu huu tulioachiwa na Kristo na tuufanye kweli tukitambua jambo hili si la kupita tu, bali li hai kila siku ya maisha yetu kama sehemu muhimu ya ufuasi wetu kwa Kristo. Hivyo basi wazo kuu na tafakari yetu leo ni kwamba, “Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”

Ndugu yangu, katika maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo kuna mambo makuu matatu yanajionyesha: La kwanza kabisa, yeye akiwa ndiyo Habari njema ya mwokovu wetu, jambo hili linakuwa ndicho kipaumbele chake cha kwanza na kielelezo cha maisha yake. Kuhubiri habari njema za Ufalme wa mbinguni. "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili," Mk 1:15. Hii ndiyo ajenda mzito na mahususi Yesu aliyowaachia wanafunzi na Kanisa kwa upana wake kabla ya kupaa mbinguni akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Ujumbe huu mahususi wa ufalme wa Mungu, unaambatana na hukumu kwa Yule asiyeamini. Wajibu wetu, yaani kwa kila mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake ni kulihubiri neno la Mungu bila kukoma. Mwijili Mathayo kalihusisha tendo hili la kuhubiri neno na ufalme wa Mungu na Sakramenti ya Ubatizo. Maana yake, siyo tu kulihubiri neno la Mungu, bali na kuwavuta watu kwa Mungu na kuuonja upendo na furaha hiyo. "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi" Mt 28:19-20.

Jambo la pili lilikuwa kuwachagua wanafunzi wake ikiwa ndiyo mwendelezo wa "Habari njema" kizazi na hata kizazi hadi mwisho wa nyakati. Yesu katika hili anatoa ahadi kwa wanafunzi wake, "Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu," Yoh 14:18.

Na jambo la tatu lilikuwa ni kulitakasa hekalu. Hekali libakie kuwa ni nyumba ya sala. Tunaona mtafaruku wa Yesu hekaluni na wale wavunja fedha. Na hasa pale alipojibu na kusema," livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha," Yoh 2:19. Kwa naama ya ndani zaidi, "Hekalu" ilimaanisha mwili wake mwenyewe na pia ni mwili wa kila mbatizwa. "Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake,"  Yoh 2:21. Mtume Paulo anatuambia miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu. "Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?" 1Kor 3:16.

Ni kwa mtazamo huu, Mtume Paulo anasema 'ole wake asipoihubiri njili,' 1Kor 9:16, na ni pale pia Yesu anawakumbusha umati waliomjia kuwa yampasa kwenda sehemu nyingine pia kwa ajili ya Habari njema za ufalme wa Mungu. "Akawaambia, "twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa HIYO NALITOKEA," Mk 1:38. Ndugu yangu ni kwa maana hiyo na sababu hiyo "YESU KUTOKEA" kwetu-kuhubiri Habari njema za ufalme wa Mungu na wokovu wetu. Tusipolifanya jambo hili kuwa ajenda muhimu kwa kila mmoja kama mbatizwa, na kwa Kanisa kama chombo cha kutuwezesha kuelekea na kuufikia uzima na utakatifu wetu, basi maisha yetu yatakuwa kama upepo tu hapa duniani. Ndugu yangu, jambo la kujiuliza; nini umuhimu wa utume wako? Pili, nini hasa gharama za kutimiza utume wako? Tuanze na hilo la kwanza. Kuna mambo sita muhimu kuhusu umuhimu wa utume wako.

1. Utume wako ni mwendelezo wa utume wa Yesu hapa duniani.

Wapendwa, kama wafuasi wake, tunapaswa kuendeleza kile alichoanzisha Yesu. Yesu hatuiti tu kuja kwake, lakini kwenda kwa ajili yake. Utume wako ni wa muhimu sana kiasi kwamba Yesu anauzungumzia mara tano, katika njia tofauti tano;

-"Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari," Mt 28:19-20.

Hili ndilo Agizo la Yesu;

-"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe," Mk 16:15

-"na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu," Lk 24:47

-"Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi," Yoh 20:21

-"Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu;  nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi," Mate 1:8

Ndugu yangu, maagizo hayo matano, ni kama Yesu anatuambia hivi, "hakika nataka ninyi mwelewe jambo hili!" Agizo kuu la Yesu (Mt 28:19-20), amepewa kila mfuasi wa Yesu, siyo la wachungaji "makleri" na wamishenari peke yao. Hili ni agizo kutoka kwa Yesu, na si la hiari. Haya maneno ya Yesu siyo "pendekezo kuu." Ndugu, kama wewe ni sehemu ya jamii ya Mungu, utume wako ni wa lazima. Kuupuza itakuwa kutotii.

Ndugu, yawezekana ulikuwa hujui kwamba Mungu anakuwajibisha kwa watu wasiomwamini wanaokuzunguka. "Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mikononi mwako," Eze 3:18. Ndugu yangu, sina lengo la kukuogofya, ila ndiyo ukweli wa Mungu. Wewe ni Mkristo pekee ambaye baadhi ya watu watakufahamu, na utume wako ni kuwaambia Habari za Yesu.

2. Utume wako ni upendeleo wa ajabu.

Ndugu yangu, ingawa ni wajibu mkubwa, pia ni heshima kubwa kutumiwa na Mungu. Mtume Paulo anasema, "Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho," 2Kor 5:18. Kwa maana hiyo, utume wako unahusisha upendeleo wa aina mbili: kumtumikia Mungu na kumwakilisha. Tunakuwa na ubia na Mungu katika kujenga ufalme wake. Eneo hili tunahitaji sana hekima ya Mungu na mwongozo wa Roho wake Mtakatifu. Yote yanawezekana tunapojisalimisha kwake, ndani na katika Yeye. Hivyo, Yesu anatuahidia jambo hili anaposema, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye,” Efe 1:17. Hakuna woga wala hofu tuyafanyapo Mapenzi ya Mungu kwani yote hayo si kwa nguvu zetu wenyewe, bali kwa mkono wa Mungu kwa sababu yote ni kwa ajili ya ufalme wake aliyotuandalia.

3. Kuwaambia wengine wanavyoweza kupata uzima wa milele ndiyo jambo kubwa unaloweza kuwatendea

Ndugu yangu, kama jirani yako angeugua KANSA au UKIMWI na ukawa unafahamu tiba, lingekuwa kosa kubwa kutomfahamisha habari hizo za kuokoa maisha. Ni kosa pia kuficha njia ya msamaha, lengo, amani, na uzima wa milele. Tuna habari kuu kuliko zote duniani, na kushirikisha wengine ndiyo wema mkubwa kuliko wote unaoweza kumfanyia mtu.

Ndugu yangu, tatizo moja tulilonalo Wakristo wa muda mfupi ni kwamba tunasahau jinsi tulivyokuwa hatuna matumaini tulipoishi bila Yesu. Lazima tukumbuke kwamba haijalishi watu wanaonekana kutosheka na kufanikiwa kiasi gani, bila Yesu hawana matumaini na wamepotea na pia wanaelekea katika kutengwa na Mungu milele. "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo," Mate 4:12. Ndugu yangu, kila mtu anamhitaji Yesu.

4. Utume wako una umuhimu wa milele.

Ndugu yangu, ufanyacho sasa kitakuwa na matokeo makubwa kwa hatima ya milele ya watu wengine, hivyo utume wako ni wa muhimu kuliko kazi nyingine yoyote, mafanikio yoyote, au lengo lolote utakalolifikia katika maisha yako hapa duniani. Matokeo ya utume wako yatadumu milele; matokea ya kazi yako hayawezi.

Ndugu yangu, hakuna tena narudia, hakuna chochote unachofanya kitalingana na kuwasaidia watu wafanye uhusiano wa milele na Mungu. Ndiyo maana lazima tuwe na juhudi kubwa katika utume wetu. Yesu anasema, "imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi," Ndugu, ukweli ni kwamba saa inakwenda na maisha yako ya utume yanapita. Anza utume wako wa kuwafikia wengine sasa! Tutakuwa na muda wa milele wa kufurahi na wale wote tuliowaleta kwa Yesu, lakini tuna muda mfupi tu wa maisha yetu ili kuwafikia. Yesu anatuambia leo kwamba katika jambo hili la kujitoa muhanga kwa ajili yake, litaambatana na ishara nyingi, na kuufichua umungu wake. “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18Ndugu, jambo hili halimaanishi uache kazi yako ili uwe mwinjilisti wa kudumu. Mungu anakutaka uwashirikishe watu wengine karibu yako Habari njema. Kama mwanafunzi, mama, mwalimu wa shule, mfanya biashara, au meneja, au chochote unachofanya, unatakiwa daima kutafuta watu Mungu anaowaweka mbele yako upate kuwashirikisha Injili. Si lazima kutumia vipaza sauti, bali kwa maisha yako ya kumpendeza Mungu huongea zaidi. Ni kutoa ushuhuda wa ukimya "silence witness" na kuwa barua za kusomwa na wengine. "Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama," 2Kor 3:2-3

5. Utume wako hukupatia umuhimu wa maisha yako.

William James alisema, "Matumizi bora ya maisha ni kuyatumia kwa kufanya kitu kitakachodumu kuliko maisha yako." Ndugu yangu, ukweli ni kwamba, ni ufalme wa Mungu tu ndio utadumu milele. Achana na "viprojekti" vya zima moto! Wakoleze watu Imani. Unacheka!

Kwa sababu hiyo, tunatakiwa kuishi maisha yanayoongozwa na malengo-maisha ya kuabudu, kuwa na ushirika, kukua kiroho, huduma, na utume wetu duniani. Matokeo ya shughuli hizi yatadumu milele. Mipango yetu ya kichungaji ilenge kwenye malengo hayo. "Viprojekti" vyovyote visivyo lenga mambo hayo ni sawa na kupiga mashutu kwa bidii kubwa na ustadi mkubwa pasipokuwa na goli.

Ndugu yangu, kama utashindwa kutimiza utume uliopewa na Mungu hapa duniani, utakuwa umepoteza maisha Mungu aliyokupa. Mtume Paulo anasema, "Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya neema ya Mungu," Mate 20:24

Ndugu yangu, kuna watu katika sayari hii ambao ni wewe tu unayeweza kuwafikia kwa sababu ya mahali unapoishi na jinsi Mungu anavyokufinyanga. "Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako," Zab 119:73

Ndugu yangu, iwapo mtu mwingine atakuwa mbinguni kwa sababu yako, maisha yako yatakuwa yamefanya tofauti ya milele. Anza kuangaza katika maeneo ya utume wako binafsi na usali, "Mungu, nani umemweka katika maisha yangu ili nimweleze Yesu?

6. Ratiba ya Mungu ya kuhitimisha historia inashikamana na ukamilishaji wa agizo tulilopewa.

Siku hizi kuna hamu kubwa ya kujua kuhusu kurudi kwa Yesu mara ya pili na mwisho wa ulimwengu. Swali: Je, itakuwa lini?

Ndugu yangu, kabla Yesu hajapaa mbinguni wanafunzi walimuuliza swali hili hili na jibu lake lilikuwa wazi. Yesu anasema, "si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi," Mate 1:7-8. Wanafunzi wanapotaka kuongea juu ya unabii, Yesu kwa haraka aligeukia uinjilishaji akiwataka wakazanie utume wao ulimwenguni. Anasema jambo hilo akimaanisha, “mambo ya kina kuhusu kurudi kwangu hayawahusu. Jambo la muhimu kwenu ni utume niliowapa. Kazanieni hilo!”

Ndugu yangu, kusikia juu ya muda halisi wa kurudi kwa Yesu Kristo ni upuuzi, kwa sababu anasema, "walakini wa Habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila Baba peke yake," Mt 24:36. Kwa nini wewe unajaribu kuibashiri? Tunachokijua kwa hakika ni kwamba: Yesu hatarudi mpaka kila mmoja Mungu anayemtaka asikie habari njema awe amesikia. Unashangaa! Yesu anasema, "tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja," Mt 24:14. Umeipata hiyo?

Ndugu yangu, kama unataka Yesu arudi haraka tia bidii kutimiza utume wako, siyo kubashiri unabii. Ni rahisi kutiwa wasiwasi, kwa sababu shetani angependa wewe ufanye kitu chochote kuliko kushirikisha watu wengine imani yako. Atakuruhusu ufanye aina zote za mambo mema ili mradi hakuna mtu yeyote utakayempeleka mbinguni. Lakini mara utakapokuwa na bidii katika utume wako, tegemea Ibilisi kukutupia kila aina ya mambo yatakayokuachisha kazi hiyo. Ndugu yangu, inapotokea hivyo, kumbuka maneno ya Yesu, "mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu," Lk 9:62

Je, zipi gharama za kutimiza utume wako?

Ndugu yangu, kutimiza utume wako vyema itakulazimu uache ajenda zako na ukubali mjadala wa Mungu kwa ajili ya maisha yako. Huwezi tu kung'ang'ania mambo mengine yote ambayo ungependa kufanya katika maisha yako. Lazima tuseme kama Yesu, "Ee, Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke, "Lk 22:42.

Hapa unampatia Mungu haki zako, matazamio yako, ndoto zako, mipango yako, na matakwa yako. Acha kuomba sala za kibinafsi kama vile, "Mungu bariki ninachotaka kukifanya." Badala yake sali hivi, "Mungu nisaidie nifanye kile unachokibariki." Unamkabidhi Mungu karatasi tupu yenye jina lako chini na unamwambia ajaze kwa kina sehemu iliyobaki. "bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki." Rum 6:13b

Kama utajitoa kutimiza utume wako katika maisha bila kujali gharama, utapata baraka za Mungu kwa njia ambazo watu wachache huzipata. Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kufanya kwa ajili ya mtu ambaye amejitoa kutumikia ufalme wa Mungu. Yesu anasema, "Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa," Mt 6:33. Tutimize wajibu huu muhimu. Hapa ndipo kwenye KANISA HAI NA LINALOSAFIRI KATIKA NJIA ILIYO SALAMA. Kwa wale tuliobado na ndoto ya kujua Yesu Kristo atarudi lini, tumeambiwa leo; Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni,” Mdo 1:11. Mara baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, wale wanawake walijidamka kwenda Kaburini malaika aliwaambia ujumbe huu, “enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7. Ujumbe mahususi kuhusu Galilaya ni kwamba tutakutana naye katika maisha yetu ya kawaida kila mmoja kadiri ya wito na maagano yake na Mungu. Kwa maana nyingine tunakutana na Kristo mfufuka kwenye utume wetu. Hapo ndipo Galilaya yako. Leo Yesu anavyopaa kwenda Mbinguni anawakumbusha Wagalilaya na sisi pia. Hivyo atakaporudi siku ya mwisho ni vyema akukute vyema kwenye utume wako.

Mzee Masumbuko alijaliwa kuwa na familia kubwa yenye watoto nane, na hivyo kufanya wote kwa ujumla kuwa kumi. Kazi ya Mzee Masumbuko ili ulinzi wa kampuni moja ya wanyama pori. Mara zote alipewa zamu ya usiku, hivyo kumfanya kuanza safari kuelekea lindoni mida ya saa tisa alasiri.

Maisha kwa ujumla kifamilia hayakuwa rahisi. Kipato chake na ukubwa wa familia yake havikuendana kabisa. Jambo hili lilikuwa sababu kubwa ya manung’uniko yake na hata kumlaumu Mungu kwa kutokuwa na usawa. Ila kilichompa faraja mara zote ni tabia njema za watoto wake, na upendo wa watoto wake na mke wake, na juhudi walizokuwa nazo katika masomo. Msingi mkubwa katika familia hii ulikuwa sala. Walimtegemea Mungu kwa kila kitu, na hawakufanya chochote kabla ya kukikabidhi mikononi mwa Mungu.

Siku mmoja akiwa anaelekea kazini akiwa anamenya limao ili ale kwani mchana ulipita mkavu bila kitu, alitazama majumba barabarani huku akivuta harufu nzuri ya vyakula kutoka kwenye majumba hayo, alijawa huzuni na kuanza kumlalamikia Mungu. “Ee Mungu, tazama leo mimi na watoto wangu hatujala, nami naenda huko lindoni sijui kitakachotokea usiku wa leo. Ee Mungu ona, majumba haya na harufu hizi za vyakula, leo familia yangu ni kilio tu,” alijisemea barabarani kama mwendawazimu hivi.

Akiwa anakula lile limao, alitazama nyuma na kuona kuna mtu anaokota yale maganda na kuyala. Tendo hilo lilimfanya asisikie tena harufu za vile vyakula kutoka majumba yale yaliyokuwepo kando ya barabara. Akajiuliza, “Je, kama huyu anakula haya maganda niliyoyatupa, si inanipasa kumshukuru Mungu katika jambo hili? Mimi nakula limao hili na ninakibarua, je, huyu sidhani hata kama kibarua anacho. Ee Mungu unirehemu na nifanye niwe na moyo wa shukrani hata kwa hiki kidogo ninachokipata.”

Ni mara ngapi mimi na wewe tunakuwa kama Mzee huyu Masumbuko?

Tumsifu Yesu Kristo!

Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu,” Lk 24:49

Tusali:- Ee Mungu, tutumie vyema kama vyombo vyako kueneza Injili yako na hasa kwa maisha yetu. Amina

 

lunes, 22 de mayo de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 6 YA PASAKA


JUMAMOSI WIKI YA 6 YA PASAKA

Somo: Mdo 18:23-28

Zab: 47:1-2, 7-8, 9

Injili: Yoh 16:23-28

Nukuu:

Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko,” Mdo 18:24

“Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi,” Mdo 18:26

“Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28

“Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27

TAFAKARI: “Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni siku nyingine tena na kwa neema ya Mungu twalitafakari neno lake la uzima. Leo, kwa namna ya pekee tulitafakari neno hili, “Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi.” Upendo wa Baba kwetu ni matokea ya upendo wetu kwa mwanaye, Yesu Kristo. Kumpenda Kristo ni kushika na kuishi yake aliyotufundisha. Hatuyafanyi hayo kwa ajili yetu binafsi, ila kwa ajili ya wengine. Kristo kautoa uhai wake si kwa ajili yake binafsi, bali kwa ajili yetu sote, na kutufanya huru kutoka kifungo cha dhambi. Kwa sadaka yake pale msalabani sote tumerudishiwa ile hadhi ya kuwa warithi na wana wa Mungu.

Tukiyafanya hayo na kuishi msingi huu wa Imani, ni kielelezo tosha kwa kumpenda Mungu kwa kuishi yale aliyotufundisha Kristo. Tendo hili litatupa uhalali wa kuomba na kupata bila vizingiti vyovyote kwa sababu tumempenda Mwana, ambaye mwana na Baba ni kitu kimoja. “Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27.

Apolo aliyekuwa Myahudi kweli kweli, anaguswa na upendo huu wa Kristo, na anatoa ushuhuda kwa Wayahudi wenzake ambao hawakumkubali Kristo. Huku ni kumpenda Kristo bila kuona haya mbele za watu. Ni kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo. Hata hivyo hatutaweza kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo kama hatumfahamu Kristo. Apolo anamfahamu Kristo kwa kuyasoma maandiko Matakatifu na kuyaelewa. Huwezi ukatoa kile usichokuwa nacho. Kwanza ni lazima ukielewe kitu hicho ndio uwe na mamlaka la kukisema. Imani hukuzwa kwa hatua. Huwezi kukurupuka tu na kuanza kutoa ushuhuda, isipokuwa kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko,” Mdo 18:24. Mkristo mwenzangu inakupasa kuzijua na kuzipitia hatua hizi sita; kulisikia neno la Mungu, kulipokea neno la Mungu, kulisoma neno la Mungu, kulitafakari neno la Mungu, kulishirikisha neno la Mungu, na mwisho kutoa ushuhuda wa neno hilo kwa kuwa shahidi wa neno. Kwa kuanzia, jiwekee utaratibu kila siku wa kusome neno la Mungu. Ukishalisoma jiulize swali hili moja tu: Je, neno hili linasema nini juu ya Maisha yangu?

Kulinena neno na kuliishi kwa ujasiri kama tokeo la kuzipitia hatua hizo sita nilisozitaja hapo juu, hukuzwa pia na wenzetu waliokwisha ijua njia hiyo. Apolo anasaidiwa na Prisila na Akila. Lengo la ndugu hawa si kumdhoofisha Apolo, bali kumtaka awe makini zaidi kuhusu neno la Mungu. Huku ndiko kunakobeba maana halisi ya kushirikishana neno la Mungu. Ni kumfanya Apolo awe hodari zaidi. Ni kumwongezea maarifa ili afanye vizuri zaidi. Hapa tunajifunza pia unyenyekevu wa Apolo kukosolewa na kuwa msikivu. Ni mara chache sana wale ambao wanaojiona wanajua na wakati mwingine kwa kuchukua vigezo vya kuwa na kundi kubwa nyuma yao, kuwa tayari kusikiliza ushauri. Apolo ni tofauti kabisa. “Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi,” Mdo 18:26. Mafanikio yetu katika maisha yasitutie upofu wa kujifunza zaidi.

Utayari wa Apolo kujifunza maarifa zaidi, unamwongezea ustadi wa kile alichokuwa anakijua awali. Kwa sababu hiyo, “aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28. Ndugu yangu, tusichoke kujifunza mambo mapya na hasa pale unaposhauriwa kufanya hivyo na wenzako kwa sifa na Utukufu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28

Tusali:-Ee Bwana Yesu Kristo, uwe njia na wokovu wangu. Amina

 

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 6 YA PASAKA


IJUMAA WIKI YA 6 YA PASAKA

Somo: Mdo 18:9-18

Zab: 47:2-3, 4-5, 6-7

Injili: Yoh 16:20-23a

Nukuu:

Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13

bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15

Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20

Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22

TAFAKARI: “Furaha katika Mateso”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari neno hili kadiri ya masomo yetu ya leo, “Furaha katika Mateso.” Licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti kuhusu mateso kadiri ya Imani zetu, uhalisia wa mateso ni mang’amuzi ambayo kila mmoja wetu anaweza kuuelezea. Wapo ambao wameenda mbali zaidi na kusema kwamba kitendo cha mtoto mdogo kulia baada ya kuzaliwa tu, ni ujumbe kwetu kwamba dunia hii tunayoishi hatuwezi kuitenganisha na mahangaiko na mateso yetu.

Mateso ni hali na pia ni sehemu ya maisha ya binadamu yeyote bila kujali imani yake. Ila "mateso" huwa na maana tu katika sababu na tafsiri yake.

Swali kwako na kwangu: Nini sababu ya mateso yangu? Nini sababu ya uwepo wetu? Je, kuna maana yoyote ya mimi kuwepo? Kama ipo; malengo yake ni nini hasa kwa hali hii niliyonayo sasa? Wapendwa yapo majibu rahisi hasa pale tu tunapojua chanzo chake. Mfano;

1. kuna magonjwa ambayo tunayapata tukijua chanzo chake ni nini, tiba yake, na matokeo yake hujulikana. Hapa mwathirika ni kufuata ushauri wa daktari na yote hueleweka.

2. Yapo pia mateso yatokanayo na magonjwa fulani twajua tu chanzo chake, ila tiba na kupona kwake bado ni kitendawili kikubwa.

3. Yapo pia mateso yatokanayo na magonjwa ambayo hatujui chanzo chake, tiba yake, na mwisho hatujui kupona kwake. Hapa binadamu hupita katika uvuli mzito wa umauti. Hapa pia yawezekana kukawa na mateso tu ambayo si ugonjwa ila ni hali ya "sintofahamu." Unakuta unateseka ila huna maelezo yanayojitosheleza.

Aina hii ya tatu ina ugumu sana kwa binadamu kuipokea. Tunajisikia kutengwa hata kutokuona umaana wa Mungu kwetu kama (upendo wake, uwezo wake na hata umuhimu wake). Bila tafsiri yenye kujumuisha, "sababu, lengo, na uwepo wa Yesu katika historia nzima ya wokovu wetu," ni vigumu kuona maana, lengo, na FURAHA katika mateso yetu kwa ujumla na zaidi kwa kipengele cha tatu.

Ni ndani ya Yesu Kristo, na katika Yesu Kristo twaweza elewa "fumbo" la TESO na siyo "jibu" lake. Ufahamu huu ukiwepo basi ni mwanzo wa FURAHA katika TESO lolote lile.

Jambo la kufahamu:

Teso au mateso si jambo au hali ya kudumu milele likiwa ndani na katika Yesu Kristo. Rejea; Mt 4:24, Mt 16:21, Mk 8:31; Lk 9:22, Lk 16:28, Lk 17:25, Lk 24:26; Rum 8:18; 2 Kor 1:6, 2 Kor 1:7; Flp 3:10; Kol 1:24; 2 Tim 1:12, 2 Tim 3:11; 1 Pet 4:13, 1Pet 5:9; Ufu 1:9.

Kwa kushiriki ubinadamu wetu na katika safari ya wokovu wetu, Yesu Kristo kaondoa umilele wa Teso/mateso yetu na kulipa/kuyapa maana. Akiwa ndiye Njia, ukweli, na uzima (Yoh 14:6), Yesu anachagua njia ya mateso kutupatia wokovu wetu. Hapa ndipo mateso au teso huwa na maana ndani ya Yesu Kristo na kwa ajili ya Yesu Kristo.Twashiriki pia mateso na wengine katika Kristo tukitambua ukweli huu wa fumbo la teso kwa njia ya sala na majitoleo yetu tukiwa katika muunganiko na Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, Mtume Paulo anaburuzwa na Wayahudi mbele ya Mahakama ya Kirumi kushtakiwa kwa kosa la kuwavuta watu ili wamwabudu Mungu. Je, kunakosa lolote kumwabudu Mungu? Kumwabudu Mungu kama tendo la kujisalimisha kwake ndiyo njia pekee ya kujenga mahusiano yetu na Mungu ya karibu. Ndio njia pekee ya kuzijua siri na ufahamu wa Kimungu. Kwa Mtume Paulo mambo yalikuwa kama hivi: “Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13. Kwa vile Mtume Paulo alisimama katika kweli na haki, Galio anawashangaa Wayahudi kwa madai yao juu ya Paulo, naye anasema, “bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15. Tukio hili ni mateso katika furaha. Ni furaha kwa sababu tunajua tunateseka katika kweli, ila hatujui kwa nini tunateswa, na watesi wetu wameingiwa upofu wa kujui kweli. Mtume Paulo analitambua jambo hili kwa undani kabisa na hivyo anasema, “kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18

Kuyaona mateso katika mtazamo huu wa Mtume Paulo ni kukomaa katika Imani, na kujua kusudi la malengo yako hapa duniani. Malengo yetu hapa duniani ni ya muda mfupi, ukilinganisha na umilele baada ya maisha haya. Yesu Kristo anatufumbulia kitendawili hiki katika Injili ya leo kwa kusema, Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Wito wa Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu mateso ni kwamba yatupasa kutazama mbele zaidi, yaani, kile kitakachokuwa baada ya mateso hayo. Kwa hiyo ni lazima kuona na kutambua kiini cha mateso yako, na mahusiano yake ndani na katika Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, furaha halisi na isiyo na kikomo ni furaha ya kuteseka pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye. Kuteseka pamoja na Kristo ni kuyatazama mateso yote ndani na katika Kristo, na kumshirikisha Kristo mateso hayo ambayo kwayo yeshapewa maana na Kristo mwenyewe. Maana ya mateso katika Kristo ni USHINDI. Kristo kayashinda mateso na kwake tu, mateso yana maana. Hivyo basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, baada ya ushindi huu wa mateso ndani na katika Kristo, ni furaha ya kweli na isiyo na kikomo.

Hivyo wapendwa katika Kristo, kamwe tusiyasahau maneno haya mazito ya Bwana wetu Yesu Kristo; “Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26. Kuyakimbia mateso ndani na katika Kristo ni kuukimbia utukufu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22

Tusali:-Ee Bwana wetu Yesu Kristo, tupe uwezo wa kuyapokea yote katika Wewe na ndani ya Wewe ili tupate maana ya furaha katika mateso yetu. Amina